Bodi ya Filamu Tanzania imemuita msanii wa maigizo Wema Sepetu kwa ajili ya mahojiano kuhusu picha jongefu zilizorushwa kwenye mtandao wa kijamii zikionyesha amevaa mavazi yanayodaiwa kutokuwa ya staha.
Taarifa iliyotolewa na Kaimu Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dk Gervas Kasiga imemtaka msanii huyo kufika katika ofisi za bodi hiyo Mei 22, 2025 saa 4 asubuhi kwa ajili ya mahojiano.
Bodi ya Filamu Tanzania inaendelea kuwasihi wasanii wa filamu kuendelea kulinda maadili ya nchi katika kazi za tasnia pamoja na mienendo yao kijamii.
Taarifa ya wito huo imeandikwa " Mwanatasnia Wema Abraham Sepetu unatakiwa kufika ofisi za Bodi ya Filamu Tanzania. Bodi ya Filamu ni chombo kilichoundwa kisheria kutengeneza na kulinda taswira ya taifa letu pamoja na kuendeleza sekta ya Filamu nchini.
"Katika kutimiza majukumu hayo haiwezi kuacha kusimamia masuala ya nidhamu na maadili kwa wanatasnia wetu.Bodi imesikitishwa na picha jongevu zisizokuwa na maadili zilizorushwa kwenye mitandao ya kijamii zikimuonesha Mwanatasnia Wema Sepetu akiwa katika mavazi yasiyo na staha.
"Hivyo, Bodi inamtaka mwanatasnia husika (Wema) kufika bila kukosa katika Ofisi za Bodi ya Filamu zilizopo Kivukoni - Dar es Salaam Siku ya Alhamisi, Tarehe 22 Mei, 2025 Saa Nne Asubuhi kwa ajili ya mahojiano."
Utakumbuka siku chache zilizopita Wema alionekana akiwa amevaa vazi ambalo linadaiwa kwamba halikuwa na staha kwenye sherehe ya kujipongeza kupata Tuzo ya Thamani nchini Kenya.
Picha hiyo ilipokea maoni mbalimbali kwa watumiaji wa mitandao ikiwemo ya ukosoaji huku wengine wakilitetea vazi hilo.

Leave a Reply