Msanii Mavokali atapeliwa na kampuni ya Uingereza

Msanii Mavokali atapeliwa na kampuni ya Uingereza

Meneja wa mwanamuziki Mavokali, Jembe One ameweka wazi hali ya kiafya ya msanii wake kwa kusema alipatwa na tatizo la afya ya akili ingawa kwa sasa anaendelea vizuri.

Jembe ameiambia Mwananchi kuwa msanii wake alipata tatizo hilo baada ya kutapeliwa na kampuni moja ya Uingereza inayofanya kazi ya usambazaji muziki ambayo hakutaka kuitaja jina. Huku akiahidiwa kufanya kolabo na wasanii kama Shakira, Maluma na Beyonce.

“Hali yake kwa sasa anaendelea vizuri. Sio vibaya sana tunaendelea kupambana naye ili aweze kukaa sawa, akiwa peke yake ndio anakuwa na mawazo sana. Kwa hiyo madaktari wamemsaidia kwa kiasi chake ili aweze kuwa sawa, kwa sababu alikuwa anapenda kukaa peke yake."

Meneja huyo amesema Mavokali aliingia mkataba na kampuni inayojihusisha na kusambaza kazi za wasanii nchi tofauti tofauti, huku wakimuahidi kufanya kolabo na mastaa mbalimbali bila mafanikio.

“Kampuni hiyo ilimuahidi remix ya wimbo wa ‘Mapopo’ kwa sababu tumeshafanya na Rayvanny, tukategemea kupata International Artist. Walikuja na gia ya kwamba wanataka kumpa msanii ambaye atafanya naye remix.

"Wakaja na majina ya wasanii baada ya hilo tukaona ni kitu kizuri tufanye nao kazi. Changamoto ni kwamba wasanii ambao waliwataja wakashindwa kuwafikia. Wakaja na wasanii wengine ambao kwenye mkataba hawapo kwahiyo tulipoanza kuhoji ndio changamoto ilipoanza,"amesema

Amesema baada ya kutokuwa na maelewano. Kampuni hiyo ilichukua hatua ya kuzifungia akaunti zote za msanii huyo.
“Hiyo ishu imekaa kisheria zaidi. Msaada ambao tunautegemea ni wakisheria. Wanasheria ndiyo wanapambana ili hii ishu iweze kuisha, kwa sababu siyo ishu ya jana au juzi ni ishu ambayo inafika mwaka wa pili sasa.Vitu vinazidi kuwa vigumu. Wale watu wamezuia hela zetu tumeamua kuongea ili jamii iweze kuelewa ,”amesema.

Aidha Jembe amesema ni ngumu kwa msanii huyo kuanzisha akaunti mpya kutokana na mkataba walioingia na kampuni hiyo ambayo inamiliki akaunti zake zote.

"Muziki ndio biashara yake kubwa ambayo anaitegemea inapofikia hatua unafanya muziki na unategemea muziki wako ndio uendeshe maisha halafu ukafungiwa akaunti zako. Inazofanya upate pesa kidogo lazima ikutie stress.

“Kwenye hili ambacho nimejifunza makampuni mengi yanayokuja si kama yanakuja na ukweli. Kwa hiyo tukubali kufanya kazi na kampuni ambazo zinamuwakilishi wao yupo Tanzania ili ikitokea kitu chochote basi ujue unaanzia wapi.

"Ile kampuni ilituma mwakilishi wao kuja hapa Dar lakini huyo jamaa ambaye tunamjua, mpaka sasa hivi kazi amefukuzwa kwa hiyo sisi tunapambana na kampuni lakini yule jamaa hayupo tena,"amesema

Aidha amesema kwa sasa wanachotaka kufanya ni kulifikisha jambo hilo Baraza la Sanaa la Taifa.
“Tumepanga kwenye BASATA wiki ijayo ili tuweze kuzungumza nao tuwafikishie jambo letu tuone na wao watatusaidia vipi. Kwa sababu tunaamini wao ndio Baraza la Sanaa na wana mamlaka ambayo wataweza kutusaidia,"ameamalizia Jembe.

Mavokali amewahi kutamba ngoma mbalimbali kama Mapopo, Hamjasema, Comando, Pwi Pwi, Densi na nyinginezo.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags