Peter Akaro
Mwanamuziki wa Marekani, John Legend (46) amesema kipindi anarekodi na Lauryn Hill (46) alikuwa ni mwanafunzi wa chuo kikuu na hakutegemea kama kazi hiyo ingejumuishwa katika albamu ya kwanza kutoka kwa rapa huyo tishio.
Legend ambaye ni maarufu pia kwa kupiga piano, alishiriki katika wimbo 'Everything Is Everything' uliowekwa katika albamu, The Miseducation Of Lauryn Hill (1998) na kutajwa katika orodha ya walioshiriki kitu kilichompa msisimko mkubwa.
Albamu hiyo ilifanya vizuri sana duniani, katika tuzo za 41 za Grammy 1999, Lauryn alishinda tano kikiwemo kipengele cha Albamu Bora ya Hip Hop akiwa ni mwanamke wa kwanza katika historia kufanya hivyo.
Katika mahojiano na The Tonight Show Starring Jimmy Fallon wiki hii, John Legend alizungumzia ziara yake inayokuja katika vyuo vikuu ila kubwa zaidi ni jinsi alivyokutana na Lauryn hadi kufanya kazi iliyokuja kuwa na matokeo makubwa.
"Mara ya kwanza nilipokutana na Lauryn Hill, nilikuwa bado mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Pennsylvania huko Philadelphia. Na nilikuwa nikiimba katika kanisa huko, mmoja wa wanakwaya wenzangu alikuwa ni Tara Michel ambaye alisoma sekondari na Lauryn," alisema na kuongeza.
"Kwa hivyo, Tara alisema, 'John, twende wote Jersey, na tutakutana na Lauryn Hill, anarekodi albamu yake ya kwanza kama solo'. Basi nilipokutana naye nilipiga piano kidogo kumuonyesha kile ambacho naweza kufanya, ilikuwa kama majaribio madogo hivi," alisema Legend.
Ndipo Lauryn akamuuliza kama anaweza kupiga piano katika wimbo wake 'Everything Is Everything' ambao alikuwa anaufanyia kazi wakati huo, Legend alikubali na kuitendea haki fursa hiyo ambayo anaitaja ilikuja kwa nadrasa sana.
Anasema kitendo cha kutajwa katika jalada la albamu hiyo kuwa alishiriki kupiga piano kilimfanya kupata fursa nyingine kama hiyo ila albamu hiyo ya Lauryn ndio ya kwanza kwake na ndio ya kwanza kutajwa kwa jina lake la kuzaliwa ambalo ni John R. Stephens.
"Sikujua ikiwa wimbo huo ungekuwepo katika albamu hiyo. Sikujua kama sehemu zangu zingetengeneza albamu. Na kwa hivyo nilikuwa nikingoja kuona ni kipi kitatokea, si unajua tena," alisema Legend na kuendelea.
"Baadaye nikapigiwa simu na Columbia Records ambayo ilikuwa ikimsimamia Lauryn na kuniuliza jinsi jina langu linaandika, kwa utani nilitaja jina langu la kuzaliwa. Ila halikuwa jina zuri la jukwaani hadi kupewa heshima hiyo katika albamu!," alisema Legend.
Ikumbukwe albamu hiyo ya Lauryn Hill ilishika namba moja chati ya Billboard 200 na kumfanya kuwa msanii wa kwanza wa Hip Hop duniani kufanya hivyo, kisha akafuata Foxy Brown, Chyna Doll (1999) na Eve, Let There Be Eve... Ruff Ryders' First Lady (1999).

Leave a Reply