Ndoto Za Akon Kujenga Mji Wake Zaota Mbawa

Ndoto Za Akon Kujenga Mji Wake Zaota Mbawa

Ndoto ya msanii na mwigizaji Akon Thiam ya kujenga mji wa kisasa nchini Senegal imeota mbawa baada ya serikali nchini humo kuchukua eneo hilo walilompatia.

Serigne Mamadou Mboup, mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Utalii nchini humo (SAPCO), amethibitisha hilo wakati alipokuwa kwenye mahojiano na BBC akieleza kuwa mradi huo haupo tena.

“Mradi wa Akon City haupo tena. Kwa bahati nzuri, makubaliano yamefikiwa kati ya SAPCO na mjasiriamali Alioune Badara Thiam [anayejulikana kama Akon]. Kile anachokiandaa pamoja nasi ni mradi halisi, ambao SAPCO itauunga mkono kikamilifu,” amesema Mboup

Kwa mujibu wa SAPCO, Akon sasa atashirikiana na serikali katika mpango mpya wa maendeleo ambao utasaidia kukuza sekta ya utalii na uchumi wa ndani. Mradi huo mpya ambao bado haujapewa jina rasmi utatekelezwa kwa ushirikiano wa karibu na taasisi za serikali, ambao utakuwa wa kawaida kabisa tofauti na Akon City uliyopanga kutumia fedha nyingi.

Awali, Akon alieleza kuwa Akon City ungekuwa mji unaotumia teknolojia ya hali ya juu barani Afrika huku kukiwa na vitu tofauti kama sarafu za kidigitali ziitwazo ‘Akoin’, majengo ya kisasa yanayofanana na Dubai, hospitali za viwango, shule, hoteli na uwanja wa ndege. Hata hivyo, tangu uzinduzi wake mwaka 2020, eneo la mradi lilibaki pori bila ujenzi wowote kuanza.

Akon, ambaye jina lake kamili ni Alioune Badara Thiam, alizaliwa Marekani lakini anaasili ya Senegal, lengo la kutaka kuanzisha mradi huo alitaja kuwa ni kuibadilisha Afrika katika teknolojia na kuwezesha maendeleo ya kiuchumi, hata hivyo mradi huo haukuweza kuendelea kufuatia na kukosekana kwa ufadhili.



Aidha kwa sasa, SAPCO imethibitisha kuwa itasimamia kwa karibu maendeleo ya mpango mpya wa Akon na kuhakikisha kuwa kila hatua inalenga mafanikio ya kiuchumi na kijamii. “Tunafurahi kuwa Akon bado ana ndoto ya kuijenga Senegal, lakini sasa anafanya hivyo kwa njia ya kweli,” alisema Mboup.

Mradi huo mpya hautakuwa wa Akon kwani serikali nchini humo ilimpokonya eneo hilo msanii huyo mwishoni mwa mwaka 2024, na sasa serikal imeripotiwa kuwekeza zaidi ya dola 1.2 bilioni kukamilisha mradi huo.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags