Aunty Ezekiel aomba radhi kuchapisha picha chafu

Aunty Ezekiel aomba radhi kuchapisha picha chafu

Msanii wa filamu nchini, Aunty Ezekiel amesema kilichopelekea aitwe na Bodi ya Filamu nchini ni kuchapisha picha chafu kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Akizungumza na waandishi wa habari muda mchache baada ya kikao na bodi hiyo, kilichofanyika leo Julai 10, 2025, Aunty amesema,

"Nilichoitiwa ni baada ya kuposti picha ambazo hazikuwa na maadili mazuri. Kama Mtanzania sikustahili kuchapisha picha zile kwa hiyo ndiyo maana niliitwa hapa," amesema Aunty.

Amesema wasanii kuna muda wanajisahau na kuweka maudhui ambayo ni kinyume na maadili kitu ambacho hupotosha kizazi kijacho.

"Kama wasanii kuna muda tunajisahau na kuposti vitu ambavyo havipendezi, hata wanaotamani kuwa kama sisi. Tunawapotosha kidogo lakini kilichopo kikubwa ni maadili nadhani tukijiweka vizuri kwenye maadili kila kitu kitakuwa sawa," amesema Aunty.

Aidha, Aunty amesema baba watoto wake Kusah hapendelei kumuona amepiga picha za namna hiyo. Na ndio alikuwa mtu wa kwanza kumwambia azifute mtandaoni baada ya kuzichapisha.

"Kusah ni mtu ambaye kwanza kupiga picha na nguo kama ile hapendi. Na sio vile tu kuna baadhi ya nguo hapendi kwa hiyo hata vingine mimi nafanya tu. Lakini kuna muda nalazimisha kama msanii, kama ingekuwa amri yake ningekuwa navaa nguo ndefu asubuhi mpaka jioni," amesema Aunty.

Hata hivyo, Aunty amewaomba radhi mashabiki zake na kuwaambia ataendelea kuposti picha lakini katika njia sahihi bila kukiuka maadili ya Mtanzania.

"Kwanza niseme nimewakosea wanisamehe na tuanze upya nitaposti picha sitoacha kufanya matangazo yangu lakini katika njia sahihi bila kuvunja maadili," amesema Aunty.

Utakumbuka Aunty Ezekiel aliandikiwa wito huo na Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dkt Gervas Kasiga Julai 7,2025 akimtaka msanii huyo kuwasili leo Julai 10,2025.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Masoud Kofii


Latest Post

Latest Tags