Mfahamu Mike ambaye sauti yake inatamba kwenye Kombolela

Mfahamu Mike ambaye sauti yake inatamba kwenye Kombolela


Mwanamuziki Michael James ‘Mike Song’ ameeleza namna tamthilia ya Kombolela na Saluni ya Mama Kimbo ilivyofanya atambulike na kumpa madili kimataifa.

Akizungumza na Mwananchi Mike ambaye wimbo wake unatumika kama 'background' kwenye tamthilia ya Kombolela ameeleza namna alivyokutana na mtayarishaji wa tamthilia ya hiyo, Abdul na jinsi alivyoikubali sauti yake.

“Nilianza na Abdul kwenye Saluni ya Mama Kimbo’ aliyenipeleka ni kaka yangu ambaye ni meneja anayesimamia usafiri kwa waigizaji na timu nzima. Wakati alipokuwa anafanya hiyo tamthilia alikuwa akitafuta wasanii wa singeli akawapa kazi, alikuwa anasema nyimbo alizokuwa amepewa hazikukidhi viwango alivyokuwa anataka yeye.

"Mimi kwa wakati ule sikuwahi kufanya wimbo wa singeli nikakaa nikajaribu kufanya kwa utofauti nikautuma, Abdul akaukubali. Akaniambia nirekebishe kisha nimrudishie tokea hapo tukanza kufanya kazi,” amesema Mike

Mbali na Kombolela na Saluni ya Mama Kimbo msanii huyo sauti yake imesikika kwenye tamthilia mbalimbali za ndani na nje ya nchi ikiwemo Toboa Tobo, Jivu, Zahanati ya Kijiji, na nyinginezo.

“Mwaka 2023 nilipata tuzo katika kipengele cha mtunzi bora wa nyimbo za filamu, kupitia tamthilia ya Kombolela. Pia nilipata nafasi ya kushiriki kwenye tamthilia ambayo inafanyika Uingereza haijatoka bado. Niliingiza sauti hapa Tanzania nikawa nawatumia, nimeweza kuingiza nyimbo tatu kwenye tamthilia iliyofanyika jijini London.

"Pia mwaka 2024 nilifanikiwa kushinda tuzo London katika mashindano ya kufanya nyimbo za filamu. Kuna kampuni ilikuwa inatafuta waimbaji unatuma nyimbo yako inafanyiwa mchakato nilifanikiwa kushinda na tuzo yangu itanifikia mwezi huu,” amesema Mike

Ameongezea kwa kueleza “Nyimbo nilizofanya nje nchi nimefanya kwa lugha ya Kiingereza na Kiswahili kidogo ili kupeleka ladha ya Tanzania kimataifa. Filamu mbili ambazo nimeshiriki lakini siwezi kutaja jina kwa sababu bado sijapewa ruhusa ya kuzitaja nafikiri ni kutokana na bado hazijatoka,” amesema na kuongezea

“Ukizungumzia filamu kutumia nyimbo siku hizi na kuachana na vinanda walivyokuwa wakitumia zamani, nadhani tasnia inaenda kukua tupo katika hatua nzuri. Ninafurahi mimi kuwa mmoja wapo kwa sababu ukitaja majina matatu wasanii watunga nyimbo katika upande wa filamu huwezi kuacha kutaja jina la Mike Song.

Anasema hatua hii inaenda kuchukua taswira mpya katika tasnia ya uigizaji kwani watayarishaji wengi wa filamu sasa wanawekeza nguvu katika kutumia nyimbo kuliko vinanda

Safari yake ya muziki ilipoanzia

“Nilianza muziki muda mrefu ni msanii binafsi ambaye nilikuwa nikijitegemea. Mwaka 2018 nilipata nafasi ya kufanya kazi na lebo kutoka London iitwayo ‘Beating Heart Music’ nilifanikiwa kufanya nao nyimbo kadhaa lakini wimbo uliowahi kutoka unaitwa ‘Temtetion’.

"Baada ya Corona mambo yalikuwa magumu hatukuweza tena kufanya kazi kutokana na wao kupoteza kila kitu ikiwemo ofisi kufungwa pamoja na wawekezaji. Wakati nafanya nao kazi malipo niliyokuwa nayapata nikawaambia wanifungulie studio wakanifungulia na kuanzia hapo nikaanza kujitegemea mwenyewe,” amesema Mike

Mbali na hayo Mike ameeleza matamanio yake katika kuningia kwenye uigizaji.

“Ndio natamani kuingia kwenye uigizaji kwa sababu najiona huko kwani mara kadhaa nimekuwa nikiigiza hata kwenye video zangu za muziki na uwezo huo ninao,” amemalizia Mike






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags