Msanii Mwingine Wa Korea Akutwa Amefariki Nyumbani Kwake

Msanii Mwingine Wa Korea Akutwa Amefariki Nyumbani Kwake

Mwanamuziki wa K-Pop kutoka Korea Kusini, Wheesung, anaripotiwa kukutwa amefariki nyumbani kwake jana Jumatatu Machi 11, 2025. Huku polisi wakichunguza sababu ya kifo chake ambacho kinahusishwa na dawa za kulevya.

Kulingana na ‘New York Times’ mwili wa mwimbaji na mtunzi wa nyimbo huyo ulipatikana ndani ya ghorofa yake jana jioni na maafisa wa Idara ya Zimamoto baada ya mama yake kuita msaada kufuatia na mtoto wake kuanguka ghafla akidhani ni mshtuko wa moyo.

Wheesung ambaye jina kamili Choi Whee-sung (43) alikuwa na historia ya matumizi ya dawa za kulevya na wachunguzi kutoka Kituo cha Polisi cha Seoul Gwangjin walikuwa wakichunguza uwezekano wa kama alikunywa dawa za kulevya kupita kiasi.

Wheesung alianza muziki 2002 akitoa albamu yake maarufu, "Like a Movie," ambayo ilishinda tuzo kadhaa mwaka huo. Lakini alianza kuyumba katika tasnia mwaka 2021 baada ya kuhukumiwa kifungo cha mwaka mmoja kwa kutumia dawa za usingizi ambazo ziliondoa uhai wa Michael Jackson, ‘Propofol’.

Utakumbuka mwezi mmoja uliopita, mwigizaji wa Korea Kusini Kim Sae-ron naye alikutwa amefariki nyumbani kwake akiwa na umri wa miaka 24. Si huyo tuu wapo wasanii wengine akiwemo Song Jae-lim alikutwa amefariki nyumbani kwake akiwa na umri wa miaka 39, huku Moonbin, nyota wa K-pop na mshiriki wa kundi la wavulana la Astro, alikutwa amekufa katika ghorofa yake mwaka 2023, akiwa na umri wa miaka 25.

Wengine kadhaa wa nyota wa K-pop vijana waliofariki katika miaka ya hivi karibuni ni Goo Hara na Sulli mwaka 2019, Minwoo wa kundi la 100% mwaka 2018, na kiongozi wa SHINee, Jonghyun, mwaka 2017.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags