Kajala Katika Mafanikio Ya Mb Dogg

Kajala Katika Mafanikio Ya Mb Dogg

Hakuna ubishi kuwa MB Dogg ni miongoni mwa wasanii wachache wa Bongofleva ambao muziki wao ulitikisa vilivyo, ngoma zake zililia sana mitaani na kutawala chati karibia zote za vituo vikubwa vya Radio nchini.

Ametoa albamu mbili, Si Uliniambia (2005) na Akili Yangu (2010), ameshinda tuzo tatu za muziki Tanzania (TMA) na sasa anatajwa kwenye kundi la wasanii walioshiriki kuijenga Bongofleva vilivyo. Mfahamu zaidi,

Baada ya Madee kumueleza Abdul Bonge kuwa MB Dogg ni msanii mzuri na anafanya vizuri mtaani kwenye zile shoo za uzinduzi wa Camp, ndipo Bonge akatoa ruhusa ajiunge Tip Top Connection baada ya yeye pia kuridhika na uwezo wake.

Marehemu Abdul Bonge alimkubali sana MB Dogg kwa wakati huo na ndiye aliyelipia fedha ya kurekodi wimbo wake wa kwanza Bongo Records, pia alimfanya Bonge kujihusisha zaidi na muziki.

Mwanzo MB Dogg alianza muziki kama Rapa, alikuwa anachana sana na hata nyimbo zake awali alikuwa anaandika katika mfumo wa Hip Hop, ila baadaye akabadilika na kufanya RnB, aina ya muziki iliyokuja kumtoa na kuweka jina lake katika ramani.

Latifah ndio wimbo wa kwanza kwa MB Dogg kuachia chini ya Tip Top lakini tayari ulikuwa umesharekodi kitambo kabla ya kujiunga na kundi hilo, viongozi Tip Top walipousikia wakapendekeza ukarudiwe Bongo Records kwa P Funk Majani.

Na hadi sasa Madee anaamini verse yake bora kwa muda wote ni ile aliyochana kwenye wimbo wa MB Dogg, Latifah unaopatikana kwenye albamu yake ya kwanza, Si Uliniambia (2005) yenye ngoma 10.

Tuzo tatu alizowahi kushinda MB Dogg katika muziki ni kutoka Kilimanjaro Tanzania Music Awards (KTMA) kama Msanii Bora Chipukizi 2005, Albamu Bora ya Mwaka (Si Uliniambia) 2006 na Msanii Bora wa Kiume wa Mwaka 2009.

Rapa Mangwair ndiye alitakiwa kuwepo kwenye wimbo wa MB Dogg, Latifah lakini P Funk Majani ambaye ndiye Prodyuza wa wimbo huo akamchugua Madee ambaye kwa wakati huo alikuwa anafanya vizuri.

Hiyo ni sawa na Rama Dee ambaye ndiye alitakiwa kusikika kwenye kiitio cha wimbo wa Nikki Mbishi 'Punchline' badala ya Grace Matata ambaye amesikika pia kwenye ngoma ya Nikki, Nyakati za Mashaka.

MB Dogg ndiye mtu wa kwanza kumpa nafasi Chelea Man katika muziki baada ya kuletewa na rafiki yake na kuambiwa Mshikaji anatokea Mwanza, ana kitu. Dogg akampa nafasi katika ngoma yake 'Mapenzi Kitu Gani' na ukawa mwanzo wa safari na ngoma zake nyingine zilizokuja kutoka chini ya Tip Top.

Siku ya kwanza ambayo Madee anampeleka MB Dogg kwa P Funk Majani, Kajala Masanja ndiye aliyewafungulia geti la kuingia Bongo Records, studio iliyokuja kumtoa kimuziki na mengine sasa ni historia.

Kufanya vizuri kwa nyimbo zake, Latifah na Si Uliniambia ndipo kulipelekea MB Dogg kutoa wimbo, Mapenzi Kitu Gani, kwa ajili ya kuvishukuru baadhi ya vituo vya Radio vilivyokuwa vinacheza kazi zake ila sio rahisi kubaini kutokana na uandishi alioutumia.

Verse ya kwanza yote ya wimbo 'Mapenzi Kitu Gani' ilikuwa kwa ajili ya shukrani, Radio zilizotajwa ni Magic FM, Clouds FM, Times FM, Uhuru FM, Kiss FM, Mlimani FM, Radio Free Africa, Radio One, TBC Taifa na East Africa Radio.

Mchanganuo upo hivi, alipoanza "Uamini miujiza (magic) mchumba" hapa anaizungumzia Magic FM, "Sauti ya nyuki inasikika" hapa ni Clouds FM na Nyuki DJ's kipindi hicho, "Songea karibu baby time zishafika" hapa anaigusia Times FM, "Unipe uhuru dear nikiss ninapotoka" hapa anaigusia Uhuru FM na Kiss FM.

Anaendelea, "Toka mlimani dear niwe free ndani ya kopa" hapa ni Mlimani FM na Radio Free Africa, "Penzi kwa fujo my buba" hapa ni Radio One na Kwa Fujo DJ's enzi hizo, "Raha ya Africa RTD mimi ndio hewani nasikika" hapa ni TBC Taifa, "Hivi kwanini dear moyo wangu unautesa, hivi haushoboki dear inavyonipenda Easta Africa" hapa anamalizia na East Africa Radio.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags