Rapa Kanye West ameweka wazi pindi atakapofariki basi angependa msanii mwenzake Drake awe msomaji wa hotuba katika siku hiyo.
Kupitia ukurasa wa X (zamani twitter), Kanye amemuomba msamaha Drake kwa migogoro yao yote iliyotokea hapo nyuma huku akisisitiza awe msomaji wa hotuba yake atakapoaga dunia.
“Niliona video ya Drake akitembea ndani ya nyumba yake na kuonyesha kwamba ana maktaba ya vitabu vya mashairi, jamani, laiti ningeweza kuona na kukumbuka hili wakati wivu uliponizidi nampenda Drake nitasema hili ninapofariki, nataka wewe utoe hotuba kwenye mazishi yangu,” ameandika Kanye.
Aidha mashabiki walifurahishwa na kitendo hicho huku wakitoa maoni mbalimbali yaliyokuwa yakieleza “Tunataka albamu ya ushirikiano kati ya hawa mastaa wawili,”, Na hii ndiyo sababu wewe ni gwiji. Safari kutoka kwenye wivu hadi kwenye upendo? Huo ndio mchakato wa ukombozi tunaouhitaji sote. Kuwa na maktaba ya vitabu vya mashairi ni jambo zuri, lakini kukubali hisia zako ni bora zaidi,”
Huku mmoja akiandika: “Tutamuona huyu jamaa akirudi kugombana na Drake kabla ya majira ya joto kufika,”.
Wawili hao wamewahi kuingia katika migogoro kadhaa miaka ya nyuma na ugomvi wao ulitamatika mwaka 2021 walipokuwa wakijiandaa kuzindua albamu zao, Certified Lover Boy na Donda pamoja na kushirikiana katika Tamasha la Larry Hoover.
Hata hivyo, amani hiyo haikudumu kwa muda mrefu kwani waliingia kwenye mgogoro tena baadaye ambapo mwaka 2024, Kanye alidokeza kuhusu kutengeneza remix ya wimbo wa Future, Metro Boomin, na Kendrick Lamar, Like That, wimbo ambao Drake aliimbiwa yeye na mastaa hao.
Kabla ya migogoro hiyo, West amewahi kuhusaka kwenye kazi kadhaa za Drake ikiwemo kusimamia video ya wimbo wa ‘Best I Ever Had’ wa mwaka 2009, pia alikuwepo kwenye ngoma ya ‘Forever’ vilevile alitayarisha na kuandika wimbo wa ‘Find Your Love’ uliotoka 2010.
Mbali na kushirikiana katika muziki lakini pia waliwahi kuwa majirani huko Hidden Hills, California kabla ya Kanye kusepa katika eneo hilo. Hata hivyo, wakati wa mahojiano na The Source, Drake alifichua kuwa ugomvi wake na Kanye alitaka kumshinda na kuwa bora kuliko.

Leave a Reply