Kevin ambaye anasimamiwa shughuli zake za muziki na mama yake mzazi 'Mama Meneja' akizungumza na Mwananchi Scoop amesema kufanya kazi na mama yake kuna umuhimu kwa sababu wanaelewana kama mtoto na mama.
"Kwanza mama sio meneja wangu moja kwa moja. Yupo pale anasimamia masuala ya pesa na kuniwezesha kiuchumi kwenye muziki wangu. Kuna meneja wangu ambaye ni mdada yupo na anahusika na masuala yangu ya kimuziki kiundani. Pia kufanya kazi na mama kuna umuhimu kwa sababu sisi ni watu ambao tunaelewana kama mama na mtoto.
"Sio kwamba hatugombani kuna muda tunapishana mimi nataka mambo yangu yaende hivi yeye anataka yaende vile. Lakini mwisho wa siku hata tugombane lazima tuelewane, changamoto zipo kuna muda nataka mambo yangu yafanyike kwa ukubwa fulani, lakini kiuchumi mama yangu anakuwa hayupo vizuri muda mwingine kwa hiyo tunapambana hapo," amesema Kevin Cash.
Aidha, kwa upande wake mama wa msanii huyo 'Mama Meneja' amesema anaweza kusimama nafasi zote, kama meneja na kama mama.
"Muziki ni biashara najua namna ya kujiweka mimi mwenyewe ikitokea sehemu ya kusimama kama mama nasimama kisawa sawa mimi ni mkali sana. Kingine ambacho napenda wa Kevin ameweza kutofautisha mimi kama mama na kama meneja.

“Kama kuna kazi tunataka kufanya inahitaji hela haijalishi lazima atanambia mama meneja sijui unatafuta pesa wapi, wekeza kwenye kazi iendelee haangalii tena ile huruma ya mama na mtoto kwamba mama hana pesa anaingia kama msanii," amesema Mama Meneja.
Mama huyo amesema anasapoti kipaji cha mtoto wake kwa sababu hata yeye anakipaji lakini hakusapotiwa na wazazi wake.
"Mimi ninakipaji cha kuimba ila familia yangu haikunisapoti. Wazazi wa zamani walikuwa na msisitizo kwenye elimu, kipaji changu kilipotea, lakini nilivyokuja kuona kipaji cha mwanangu nilisema nitakiendeleza.
“Ninapomuona anaimba najiona kama mimi ndio naimba. Kwa hiyo haikuwa ngumu kuendeleza kipaji chake, lakini pia muziki ni biashara haijaniwia ugumu kuwekeza pesa zangu,” amesema Mama Meneja.
Kevin Cash kwa sasa anatamba baada ya kuachia wimbo wake mpya akiwa na Jaivah 'Teketeza' uliyotayarishwa na Kapipo huku Lizer Classic akihusika katika mchakato wa mixing na mastering.
Teketeza inatoka kipindi ambacho Kevin Cash anaendelea kufanya vizuri na ngoma yake ya Fire Burn, yenye ladha ya R&B na Afrobeat, ambayo tayari imepata zaidi ya watazamaji 25,000 kwenye mtandao wa YouTube.
Mkali huyo akiwa na mwaka mmoja tangu aanze rasmi kufanya muziki, tayari ameachia jumla ya nyimbo sita ambazo ni Lolo, Pesa, Koko, Khululek, Fire Burn, na sasa Teketeza.
Ameshafanya collabo na wasanii wakubwa ndani na nje ya mipaka ya Tanzania. Jambo linaloonyesha ukuaji wake wa haraka kwenye gemu ya muziki.
Uwezo wake wa kuchanganya mitindo mbalimbali ya muziki umemfanya kuwa kipenzi cha vijana wengi, hasa kupitia mapokezi chanya kutoka kwa mashabiki wake mtandaoni na majukwaani.
Hii imeonekana kupitia mafanikio ya nyimbo zake pamoja na ushiriki wake kwenye matamasha kama Chuo kwa Chuo, linaloandaliwa na msanii Billnass.
Leave a Reply