Hivi karibuni Jux na mkewe Priscilla kutokeaNigeria wamethibitisha kuwa wanatarajia mtoto wao wa kwanza tangu wamefunga ndoa Februari mwaka huu ikiwa ni takribani miezi nane ya uhusiano wao unaojadiliwa na wengi.
Hata hivyo, Jux naye ameamua kupita njia za mastaa wengi kwa kuhusisha baraka hiyo (ujauzito) na muziki wao kama sehemu ya shukrani na hata kutunza kumbukumbu ya jambo hilo la kipekee.
Jux na Priscilla ambaye ni binti wa mwigizaji maarufu wa Nollywood, Ojo, waliweka wazi uhusiano wao mnamo Julai 2024 ikiwa ni miezi michache tangu mwanamuziki huyo kuachana na aliyekuwa mpenzi wake, Karen Bujulu.
Siku wanatangaza kuwa Priscilla ni mjamzito, ndipo Jux alipoachia wimbo wake mpya, Thank You (2025) ambao anamshukuru mkewe kwa zawadi hiyo ambayo ni mara ya kwanza kuipata maishani mwake.
Katika video ya wimbo huo uliotayarishwa na S2kizzy huku ukiongozwa na Director Kenny, Priscilla anaonekana mwenye furaha sana kwa muziki huo mzuri lakini hasa kile anachotarajia hivi karibuni.
Na hii inakuwa video yake ya nne Jux kwa Priscilla kutokea baada ya kufanya hivyo katika Ololufe Mi (2024), Si Mimi (2025) na God Design (2025) kutoka katika Extended Playlist (EP) yake ya kwanza, A Day To Remember.
Mbali na Jux, mwanzilishi wa chapa ya African Boy, baadhi ya wanamuziki wengine wa Bongofleva waliofanya kitu kama hicho kwao binafsi au kwa niaba ya wenzao wao, ni Nandy, Marioo na Malkia Karen kama ifuatavyo.
NANDY & BILLNASS
Takribani mwezi mmoja baada ya kufunga ndoa na Billnass, hapo Agosti 11, 2022, Nandy aliachia video ya wimbo wake 'Napona' kutoka katika EP yake ya tatu, Maturity (2022) huku akimshirikisha Oxlade kutokea Nigeria.
Katika video hiyo iliyosimamiwa na Director Kenny, Nandy alionekana kufurahia ujauzito wake pamoja na mumewe Billnass ambaye pia alitokea katika video hiyo tangu mwanzo ambapo wanaonekana wakitoka nyumbani kwao na kwenda katika eneo lao la biashara ya chakula.
Nandy na Billnass walijaliwa mtoto wao wa kwanza, Kenaya mnamo Agosti 2022 ila waliamua kumficha mtoto huyo mbele ya mitandao ya kijamii hadi alipotimiza umri wa mwaka mmoja, ndipo sura yake ikaonekana mtandaoni kwa mara ya kwanza.
MAIKIA KAREN
Mwimbaji huyu ambaye kwa sehemu alilelewa na Lady Jaydee, hapo Oktoba 27, 2021 aliwapa mashabiki video ya wimbo wake 'Haji' ambayo ameonyesha ujauzito wa mtoto wake wa kwanza, ila mpaka sasa ana watoto wawili.
Karen ambaye ni binti wa aliyekuwa mtangazaji maarufu marehemu, Gardner G Habash, katika wimbo huo uliotengenezwa na Trone, anamzungumzia mwanaume aliyempenda ila ukauvunja moyo wake, hivyo sasa hana tena haja naye.
Ila Karen hajawahi kuweka wazi ni nani baba mtoto wake, na miezi mitano iliyopita alitoa wimbo wake, Single Mother (2025) akimshirikisha Vanillah wa Kings Music. Katika wimbo huu anasema yeye ni single mother anayepambania maisha yake na sio mapenzi tena!
MARIOO & PAULA
Aprili 25, 2024, Marioo aliachia video (visualizer) ya wimbo wake 'Hakuna Matata' uliotayarishwa na S2kizzy, katika video hiyo iliyoongozwa na Director Joma, mpenzi wake Paula ametokea na kuonyesha matukio muhimu katika safari yake ya ujauzito.
Kwanza Paula na Marioo wameonyesha jinsi walivyopiga picha kwa ajili ya kutangaza kwa mashabiki wanatarajia mtoto, na pili wameangazia tukio la baby shower ambalo lilihudhuria na mastaa kibao Bongo huku likirushwa live.
Wawili hao ambao wamefanya pamoja video nyingine kama Lonely (2023), Tomorrow (2023), Sing (2023) na Unachekesha (2024), mtoto wao Princess Amarah alizaliwa Mei 2024, na Marioo alimtungia wimbo 'My Daughter' unaopatikana katika albamu yake ya pili, The Godson (2025).
KUNA HILI PIA
Ndani ya muda mfupi baada ya mastaa hao au wenzao kujifungua, watoto huanza kupata dili mbalimbali za ubalozi na hata matangazo ambapo mara nyingi hutumia kurasa zao za mitandao ya kijamii.
Mathalani mtoto wa Nandy na Billnass, Naya tayari ana wafuasi zaidi ya 756,000 Instagram. Wakati anatimiza mwaka mmoja, mama yake alisema Naya amepata dili sita za ubalozi ambazo atakuwa anazitangaza katika ukurasa wake.
Mara kadhaa ukurasa wa Naya unaosimamiwa na wazazi wake, umeonekana kutangaza bidhaa kwa ajili ya watoto, na pia anautumia kuonyesha ukuaji na mtindo wake maisha kuanzia nyumbani hadi shule.
Naye mpenzi wa Marioo, Paula baada ya kujifungua tu, ndipo amepata dili nyingi za kutangaza bidhaa zinazohusu watoto ambazo kina mama wengi wanaolea wanazihitaji kila siku.
Ukitazama ukurasa wa Instagram wa mtoto wake Princess Amarah wenye wafuasi zaidi ya 273,000, utaona jinsi ulivyojaa matangazo ya bidhaa za watoto wadogo.
Ikumbukwe Marioo katika albamu yake pili, The God Son (2024) chini ya Bad Nation, alitoa wimbo 'My Daughter' ukiwa ni maalumu kwa ajili ya binti yake huyo ambaye ameonekana katika video yake pamoja na mama yake.
Leave a Reply