Mwanamuziki na staa wa filamu, Teyana Taylor, 32, kutokea Marekani anatarajia kufanyiwa upasuaji mdogo eneo la koo lake ili kuondoa uvimbe ambao umekuwa ukimpa maumivu wakati wa uimbaji.
Teyana aliyevuma na kibao chake, Morning (2019), alifichua mnnamo Jumatano hii, Agosti 6, kwamba atafanyiwa upasuaji wa dharura baada ya madaktari kugundua uvimbe usio wa saratani kwenye nyuzi za sauti (vocal cords).
Alitoa taarifa hiyo kupitia Instagram Story ila aliahidi kuwa ingawa atalazimika kufuta baadhi ya maonyesho na ratiba zake zilizopangwa awali kama vile kuhudhuria kipindi cha podcast na Michelle Obama, maandalizi ya albamu yake 'Escape Room' yataendelea kama kawaida.
"Kwa muda mrefu sasa nimekuwa nikikumbana kimya kimya na changamoto ya sauti. Na baada ya mashauriano mengi na madaktari, nimeambiwa nahitaji kufanyiwa upasuaji mara moja," alisema na kuongeza.
"Wamegundua nina uvimbe usio wa saratani ambao umekuwa ukiharibu sauti yangu na kunisababishia maumivu makali. Kwa bahati nzuri, tumewahi na unaweza kutibiwa lakini inamaanisha lazima nipumzike ili kupona kabisa," alisema.
Mama huyo wa watoto wawili, aliendelea kwa kueleza kuwa jambo hilo linavunja moyo kwa sehemu na hachukulii poa umuhimu wa kuwa karibu na mashabiki wake ili ndio hivyo mazingira yamemlazimisha.
Kitu kingine kikubwa kilichokuwa kikimpa wasiwasi yeye pamoja na mashabiki wake ni kuhusu kutolewa kwa albamu yake inayokuja (Escape Room), ambayo amekuwa akiitayarisha tangu mwanzoni mwa mwaka huu.
Kwa bahati nzuri, amethibitisha kuwa albamu hiyo bado itatolewa kama ilivyopangwa, yaani Agosti 22, lakini atahitaji kuelekeza nguvu zake zaidi kwenye kuhakikisha anapona kwanza na kurejea katika kazi zake.
Akizungumza kuhusu jinsi alivyowekeza nguvu kubwa katika mradi huu mpya wa safari yake kimuziki na jinsi hali yake ya sasa inavyoendana kimaajabu na maudhui ya albamu hiyo, alisema;
"Nimeweka moyo wangu wote kwenye mradi huu mpya, hii ndio kazi ya kipekee zaidi niliyowahi kuifanya. Wakati nilipokuwa tayari kushiriki nanyi, maisha yakanipa 'Escape Room' ambayo sikuitegemea," alisema.
Albamu ya Escape Room inatarajiwa kuwa na nyimbo 22, zikiwemo zilizotangulia kutoka kama Bed of Roses na Long Time.
Ikumbukwe albamu yake ya mwisho kutoa, The Album (2020) ilishika nafasi ya nane kwenye chati ya Billboard 200, na nafasi ya sita kwenyeTop R&B/Hip-Hop Albums.
Mwaka 2025 unaonekana kuwa wenye shughuli nyingi kwa Teyana ambaye anacheza pia filamu ya One Battle After Another (2025) yake Paul Thomas Anderson, akiwa na Leonardo DiCaprio na Sean Penn. Filamu hii inatarajiwa kutoka baadaye mwaka huu.
Jina lake kwenye muziki lilianza kuchomoza alipoachia wimbo wake, Google Me (2008), ila umaarufu ulikuja baada kushiriki bila kutajwa katika nyimbo mbili za Kanye West, Dark Fantasy na Hell of a Life kutoka kwenye albamu, My Beautiful Dark Twisted Fantasy (2010).

Leave a Reply