Mwigizaji mkongwe wa Bongo Movie, Dude ametoa neno baada ya mechi ya watani wa jadi kati ya Yanga na Simba iliyokuwa imepangwa kuchezwa leo Jumamosi Machi 8, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kuhairishwa.
Kupitia ukurasa wa Instagram wa Dude ameandika “Mpira Wa Kibongo Una Ujinga Mwingi, Imagine watu wameingia gharama, wamejiandaa kwa ajili ya kuangalia hii mechi, wamesafiri kutoka mikoani na nje ya nchi kwa gharama kubwa.
“Una watu wamekopa ili wakafanye biashara siku hii kubwa leo, hizo bidhaa wazifanyaje, kuna vyakula, vinywaji na vingine vingi, maamuzi ya watu wachache wasiofikiri kwa mapana wanaleta shida kwa mamia ya wapenda soka, Ni Nani Atarejesha Gharama Za Hawa Wahanga?,”
Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imetangaza kuahirisha mchezo huo rasmi leo Jumamosi Machi 8, 2025 kutokana na sintofahamu iliyotokea baada ya klabu ya Simba kuzuiwa kuingia uwanjani kwa ajili ya kufanya mazoezi ya mwisho kuelekea mchezo huo.
Kutokana na hali hiyo, Bodi ya Ligi kupitia Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imeamua kuahirisha mchezo huo hadi uchunguzi wa kina utakapokamilika na maamuzi sahihi kufanyika.
Hata hivyo tarehe mpya ya mchezo huo itatangazwa mara baada ya uchunguzi huo kukamilika ili kuhakikisha haki na usawa vinazingatiwa katika uendeshaji wa ligi.

Leave a Reply