Uongozi ni wito na watu husema hakuna kazi ngumu kama kumuongoza binadamu. Kwa kulitambua hilo kwenye Segment ya Kazi tumeangazia mambo ya kuzingatia unapopata uongozi kazini.
1.Kuwa mtu unayewasiliana vema na wafanyakazi wenzako.
Lazima uwe na uwezo mzuri wa kutoa na kupokea taarifa. Kuwa na uwezo wa kueleza kinagaubaga kitu unachokihitaji na sababu za kukihitaji. Usiwe kati ya wale wapendao kuhitaji tu pasipo uwezo wa kutoa maelezo yoyote wala kutaka kuulizwa. Jenga ujasiri katika kupokea maulizo yawayo yoyote.
Wasifie na kuwapongeza wanaostahili sifa na pongezi. Kama unavyopenda kusifiwa au kusikia habari njema zikiongelewa kuhusu wewe au kuhusu yale aliyoyafanya.
2.Jifunze kuwajengea uwezo wale unaowaongoza
Ziko nyakati ambazo utafatwa na unaowaongoza wakikutaka kuwasaidia kufanya au kutatua jambo fulani. Jifunze kuwasaidia kuona uwezo wao kulishughulikia jambo hilo wenyewe.
Kwa namna hii utakuwa unapunguza moyo au fikra za utegemezi na kukuza fikra za kujitegemea.
3.Wasikilize wote wenye malalamiko, au pande zote mbili za malalamiko kwa uwiano sawa, hata kama kuna upande ambao wewe hauna imani nao.
Iwapo kuna ulazima wa kutoa adhabu jifunze kufahamu nyakati za kutoa adhabu mbele ya wengine na nyakati za kutoa adhabu kimya kimya pasipo wengine kujua. Tumia muda wa kutosha kuchunguza chanzo cha tatizo ili kuzuia chanzo kimoja kusumbua mara kwa mara.
Katika uongozi ziko ambazo unaowaongoza watakufuata wakitaka wazungumze na wewe matatizo yao, kama kiongozi mzuri lazima uwe tayari kwa hili wakati wowote.
4.Gawa majukumu kwa usahihi
Maana halisi ya ugawaji wa majukumu ni kule kumtafuta mtu sahihi awezae kufanya sehemu ya kazi yako kwa usahihi. Mara unapohakikisha uliyempata ni sahihi, kinachofuata ni kumwacha aendelee na kazi pasipo mwingiliano usio lazima.
Viongozi wengi huona shida sana kugawa majukumu na mara wajaribupo kufanya hivi, basi huwa saa zote migongoni mwa aliyeachiwa kazi kuhakikisha inafanywaje, huku ni kukosa imani kwa watendaji wako.
5.Toa mafunzo kwa wafanyakazi wenzako
Wakati wowote ni vizuri mtu au watu kuandaliwa vema kwa utendaji, usidhanie tu kuwa wote wanajua nini cha kufanya, lazima kufahamu nani wanatakiwa kufanya kipi na nini wakijue ili kuwawezesha kufanya kile wanachotakiwa.
Ruhusu muda wa kutosha kujifunza jambo fulani, mfano muda wa maelezo, muda wa maonesho, muda wa mazoezi, muda wa majaribio, muda wa kutahiniwa n.k. katika muda huo kumbuka kutoa wakati wa mapumziko mafupi.
Leave a Reply