Wimbo Wa Celine Dion Haukutakiwa Kuwepo Filamu Ya Titanic

Wimbo Wa Celine Dion Haukutakiwa Kuwepo Filamu Ya Titanic

Titanic imekuwa filamu ya kifahari kutokana na ubora wa utayarishaji wake, uigizaji, na wimbo wake maarufu, ‘My Heart Will Go On’, ulioimbwa na Céline Dion.

Hata hivyo, ingawa wimbo huo ulipata umaarufu mkubwa duniani, lakini James Cameron hakuwa na nia ya kuutumia mwanzoni na hii hapa ndio sababu.

Mwaka 1997, miaka mitatu baada ya kutoa filamu ya True Lies, Cameron alirudi na mradi wake mkubwa zaidi wakati huo ambao ni Titanic, filamu ya mapenzi na janga iliyotokana na matukio halisi ya kuzama kwa meli ya RMS Titanic mwaka 1912.

Inaelezwa kuwa kimsingi mpango wa awali ulikuwa kwamba muziki utakaosikika kwenye filamu ya Titanic ulitakiwa usiwe na maneno (purely instrumental), lakini kampuni ya kurekodi ilikuwa na mpango tofauti.

Msimamizi wa muziki, katika filamu hiyo Randy Gerston, aliiambia Billboard kuwa waliingia mkataba na Sony kurekodi albamu ya muziki wa filamu hiyo, ambayo ilipaswa kuwa kazi ya Horner pekee, lakini kampuni hiyo ilitaka wimbo wa mwisho (end-title song) ujumuishwe katika filamu.

Kwa sababu Cameron alikuwa na mawazo yake binafsi kuhusu filamu huku akisimamia msimamo wake wa wimbo utakao tumika usiwe na maneno, lakini Will Jennings (mwandishi wa My Heart Will Go On) aliletwa kwa siri kuandika mashairi ya wimbo huo, ili kuhakikisha unajumuishwa kwenye filamu bila Cameron kujua mapema.

Hata hivyo, Cameron alibadili mawazo baada ya kuusikia wimbo huo. kwa mujibu wa James Horner, alingoja hadi Cameron awe katika hali nzuri kabla ya kumwonyesha wimbo huo.

Licha ya kuukubali wimbo huo lakini alikuwa na wasiwasi kwamba angekosolewa na jamii kuifanya filamu hiyo kuwa ya kibishara zaidi lakini jambo liliishia kuwa uamuzi mzuri.

‘My Heart Will Go On’ haukuwa tu wimbo wa kumtambulisha Céline Dion, bali pia moja ya sehemu zinazokumbukwa zaidi kutoka filamu ya Titanic na ulichangia sana mafanikio ya filamu hiyo. Ambapo mpaka kufikia sasa wimbo huo umetazamwa zaidi ya mara milioni 167 kupitia mtandao wa YouTube.

Titanic ilikuwa filamu ghali zaidi kuwahi kutengenezwa wakati huo, ikiwa na bajeti ya utayarishaji ya dola milioni 200, na hatimaye ikawa filamu iliyopata mapato makubwa zaidi katika historia ikiwa filamu ya kwanza kufikia mauzo ya zaidi ya dola bilioni 1 duniani kote.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags