Wasanii na mionekano yao

Wasanii na mionekano yao

Mwonekano ni kati ya vitu vinavyoweza kumpa msanii utambulisho wake ingawa wapo baadhi ya watu wamekuwa wakijiuliza kama kuna ulazima wa msanii kuvaa nguo za ajabu, mabwanga, nguo za kuchanika, kunyoa mitindo mbalimbali, na hata kubadili rangi za nywele zao.

Wapo baadhi ya wasanii ambao wamejitengenezea mionekano yao kama ilivyo kwa Burna Boy na Asake kutoka nchini Nigeria, na hata msanii kutoka nchini Marekani Kanye West, ambaye amekuwa akizua gumzo mara kwa mara kwenye mitandao ya kijamii kutokana na mtindo wake wa maisha hasa mavazi.

Bongo pia wapo wasanii kama vile Diamondplatnumz, Jux, Harmonize, Zuchu, Rayvanny na wengineo wenye mionekano ya kipekee na mavazi ya aina yao.
Kutokana na hilo baadhi ya watu ambao wapo nje ya gemu imekuwa ngumu kuelewa mtindo wa maisha ya wasanii na mionekano yao japo wapo wanaovutiwa nao.

Ni lazima msanii kuwa na muonekano wa kipelee tofauti na watu wengine?
Derick Joseph mdau wa muziki, anasema utofauti wa msanii unamsaidia kutangaza ngoma zake na kutosahaulika haraka.
"Utofauti unasaidia kutangaza ngoma zao na kutosahaulika kama ilivyokuwa kwa Jux alikuwa hatoi ngoma lakini watu hawakumsahau kutokana na muonekano wake,"anasema.

Ameongezea kuwa utofauti husaidia msanii kujenga alama na utambulisho wake huku akitolea mfano wasanii kama vile Justin Bieber na Diamond.

"Justin Bieber wakati anatoa albamu yake ya ‘Changes’ mwaka 2020, alirudisha trendi ya kuvaa mabwanga, nguo kubwa na Bongo Diamond alivyofanya ‘Jeje’ alivaa suruali kubwa na viatu vikubwa watu wakavifuatilia na kuanza kuvivaa.

"Zamani watu walikuwa wanabana suruali lakini siku hizi hata mtu akivaa bwanga bado anaonekana yupo kwenye fashion kwa sababu wasanii wana-set trend yaani wanaachana na vitu ambavyo watu wanafanya na kuanzisha vipya ili watu waige,” anasema Derick.

Peter Minja mdau wa muziki kutoka Chang’ombe Dar es Salaam, amesema msanii lazima awe tofauti na watu wengine ili kujitofautisha.

“Msanii ni lazima awe tofauti na watu wengine kimavazi, muonekano na maisha kwa ujumla kwa sababu akiwa kawaida hatokuwa na kitu cha ziada cha kufanya mtu aweze kumfuatilia.

"Ukitazama mtu mpaka unaitwa msanii basi tayari kuna vitu unaweza kuvibadilisha na kuwa kwenye muundo wa sanaa na vikavutia watu wengine,” anasema Peter.

Hakuisha hapo na kuamua kutolea mfano maisha ya baadhi ya wasanii kwenye mtindo wao wa mavazi na picha wanazopiga kwa kudai kuwa wanafanya hivyo ili watu waweze kuvutiwa nao huku akimtolea mfano mavazi ya msanii Diamond na kudai kuwa endapo atavaa suruali za vitambaa na viatu mchongoko basi atakosa mvuto.

Mbali na Peter, mdau mwingine Mariam Jumbe amesema hata kwa wasanii wenye kipato cha chini ni lazima watafute muonekano ambao unaweza kuwatofautisha na watu wengine.

“Tunajua wapo wasanii wenye hali ya chini ila kwenye kujitafuta lazima waoneshe maisha ya namna fulani anayoishi kama msanii ili waweze kuvutia, mavazi wanayotakiwa kuvaa yawe na mvuto kwa jamii yawakilishe sanaa”, anasema Mariam.

Mbali na wadau hao msanii chipukizi wa muziki wa Bongo Fleva, Xouh amesema msanii lazima uweze kuwa tofauti kwani anatakiwa akipita sehemu watu wote wajue msanii amepita.

"Msanii lazima upate pesa kwa ajili ya muonekano wako kwa sababu ukipita sehemu watu wote wanatakiwa kufahamu kuwa msanii kapita, haipendezi kuwa kawaida kama watu wengine,"anasema

Hata hivyo John Lupembe, ambaye ni mdau wa muziki nchini ametoa mtazamo wake juu ya suala hilo.
“Sahihi kuwa na muonekano tofauti ili kuweza kutofautishwa, lakini linapokuja suala la maisha ni wewe uamuzi wako binafsi muda mwingine unakuta msanii hana kipato cha kuishi maisha ya kitajiri ili kukwepa mashabiki kufahamu kuwa hana kipato anaanza kuigiza.

"Msanii unatakiwa kuwa na muonekano tofauti lakini hakikisha utofauti wako usikupelekee kushindwa kuishi maisha yako ya kawaida, na utofauti si tu mavazi hadi kwenye kusaidia jamii, kuwasilisha mawazo na kuwasiliana,” anasema John.

Kwa upande wake Melissa Damian, amesema haoni umuhimu wa msanii wa muziki kuwa na muonekano wa tofauti badala yake wanaotakiwa kufanya hivyo ni wanamitindo.

"Kuwa na muonekano wa tofauti mimi naona labda kwa wanamitindo lakini msanii wa muziki wao cha kuwapa utofauti ni aina ya mistari na siyo kukazania kwenye mavazi," anasema






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags