Wachezaji wa kikapu wanaotesa katika tasnia ya muziki

Wachezaji wa kikapu wanaotesa katika tasnia ya muziki

Aloooh, happy new month bwana. Ikiwa tayari tumeingia katika mwezi wa mahaba bwana vipi kinaeleweka au kikubwa pumzi tu? hahahaha karibu sana kwenye makala za michezo na burudani mtu wangu.

Nikwambie tu kuwa wiki hii bwana tumekuandalia wachezaji wa mpira wa kikapu wanaofanya sanaa ya muziki, licha ya kuwa wachezaji maarufu duniani.

Fahamu kuwa katika miaka ya 90, mpiga kinanda na mtunzi wa Kiitaliano, Ludovico Einaudi katika moja ya hotuba zake aliwahi kunukuliwa akisema ‘sanaa daima ni kutafuta kitu cha tofauti, kutafuta hisia mpya, mtazamo mpya, maono mapya.’

Nukuu hiyo ya Einaudi ilipendwa na watu tofauti tena hususani wale ambao walijaaliwa kuwa na talanta ya kufanya mambo mbalimbali. Bwana mmoja nchini Uingereza Edward Stock alisema nukuu hiyo inaelezea uthubutu wa kufanya kitu kipya kujaribu jambo jipya licha ya kuwa katika nafasi fulani.

Bila kupoteza utamu bwana, moja kwa moja tuanze na nguli huyu wa kikapu ambaye anapambania pia kwenye masuala ya muziki ebwana eeeh, hatari huyu hapa Damian Lamonte Ollie Lillard Sr bila utakua unamuelewa mwamba huyu.

 

Damian Lamonte Ollie Lillard Sr

Damian ni mchezaji wa mpira wa kikapu nchini Marekani anayekipiga katika timu ya Portland Trail Blazers.

Amezaliwa Julai 15, 1990, kabla ya kushiriki NBA aliwahi kushiriki mpira wa kikapu wa chuo kikuu kwa Weber State Wildcats na kupata timu ya tatu ya All-American katika 2012.

Damian anadhihirisha nukuu ya mpiga kinanda wa Kiitaliano Einaudi kwamba ‘sanaa daima ni kutafuta kitu cha tofauti, kutafuta hisia mpya, mtazamo mpya, maono mapya.’

Mchezaji huyu kutokea Portland amethibitisha hilo kwa kuendelea kutafuta kitu cha tofauti, ambapo mbali na kuwa mchezaji, ameamua kujikita katika muziki wa miondoko ya kufoka maarufu kama Hip Hop.

Damian Lillard ni msanii wa hip-hop na rapa anayetambulika kwa jina la ‘Dame D.O.L.L.A.’ ambalo linasimama badala ya ‘Different On Levels the Lord Allows’, ikimaanisha ‘Tofauti katika ngazi Mungu anazoruhusu.’

Inaelezwa Damian alianza kurap kipindi ambapo alikua anapendelea kutembea na gari la binamu yake Eugene "Baby" Vasquez, ambaye alihamia Oakland kutoka New York City mapema miaka ya 1990.

Ushawishi mwingine mkubwa katika uimbaji wa rap wa Damian ulikuwa binamu yake Brookfield Duece, ambaye alipata mafanikio fulani katika onyesho la kufoka la Oakland.

Damian alianza kurap katika mtindo wa mitandao ya kijamii unaoitwa "Four Bar Friday" ambapo yeye na yeyote anayechagua kushiriki, huwasilisha video yao wakirap mstari mdogo kwenye Instagram kila Ijumaa na hashtag #4BarFriday.

Ikumbukwe kuwa julai 2015, alitoa wimbo wake wa kwanza unaotambulika kama, "Soldier in the Game", kupitia tovuti ya utiririshaji ya muziki mtandaoni SoundCloud.

Nako Oktoba 21, 2016, Damian alitoa albamu yake ya kwanza ya The Letter O, ambapo mwaka uliofata Oktoba 6, 2017, Damian aliachia albamu yake ya pili iliyotambulika kama ‘Confirmed’ nakupokelewa na mashabiki tofauti wa muziki duniani.

Damian Lillard hakuishia hapo baada ya kuachia albumu zake mbili aliamua kutoa ya tatu ambayo ilitambulika kwa jina la ‘Big D.O.L.L.A.’ Agosti 9, 2019.

Album hiyo ilikua na maingizo mapya ambapo aliamua kushirikisha baadhi ya wasanii maarufu na wenye historia kubwa katika tasnia ya muziki ambapo alimshirikisha Lil Wayne, Mozzy, na Jeremih.

Damian baada ya kujulikana katika tasnia ya muziki wa rap ameamua kuwa na lebo yake ya kurekodi, ambayo inajulikana kama ‘Front Page Music’ ambayo inajumuisha Brookfield Duece katika orodha yake.

Wimbo wa Lillard "Kobe", ambao ulitolewa Septemba 2020 na kuwashirikisha Snoop Dogg na Derrick Milano, ni sehemu ya wimbo wa NBA 2K21 kama kumbukumbu kwa marehemu Kobe Bryant.

 

 

Louis Tyrone Williams

Ukiachana na Damian bwana bado ngoma nzitoo kwa kijana huyu hapa Louis Tyrone Williams kwa sasa anacheza kunako timu ya ‘Atlanta Hawks’ ikiwa ni mara yake ya pili kucheza hapo baada ya kuondoka mwaka 2012, nafasi anayotumikia ni ya ulinzi ambapo timu yake inashiriki ligi kuu ya mpira wa kikapu nchini Marekani.

Williams aliyezaliwa Oktoba 27, 1986, katika timu yake amefanikiwa kuwa mchezaji bora wa mwaka mara tatu wakati huo huo akitambulika kama mmoja wa marapa bora zaidi wa NBA.

Mzaliwa huyo wa Atlanta anauchukulia muziki wake kwa umakini sana na ameupa nafasi ya pili katika maisha yake mbali na talanta aliyokuwa nayo ya kucheza mpira wa kikapu.

Kwa kudhihirisha ukubwa wake katika tasnia ya muziki, Drake alishawahi kumpa shangwe kubwa alipomtaja Williams kwenye wimbo wake "6th Man."

Katika ngoma hiyo Drake alisikika akisema ‘6 man like Lou Will', 2 girls and they get along like I'm (Lou), akimaanisha ‘Wanaume 6 kama Lou Will', wasichana 2 na wanaelewana kama mimi (Lou).

Williams pia amefanya freestyle katika nyimbo, kama vile remix ya Meek Mill na Rick Ross ya 'Ima Boss.'

Mnamo 2019, alitoa wimbo "Rebound," na 'Lemon Pepper Lou' inaendelea kutengeneza nyimbo kati ya michezo.

Williams alitumia misimu saba na Philadelphia kabla ya kusaini na Atlanta Hawks mnamo 2012, akicheza misimu miwili huko kabla ya kuuzwa kwa Toronto Raptors katika msimu wa mwaka 2014.

Alitumia msimu mmoja na Raptors kisha akasaini na Los Angeles Lakers kutoka 2015 hadi katikati ya msimu wa 2016-17 NBA, wakati aliuzwa kwa Houston Rockets. 

Baada ya kumaliza msimu na Roketi, kisha akauzwa katika msimu wa mwaka 2017 kwa Los Angeles Clippers. Williams alirudi tena katika timu yake ya Hawks mwaka 2021 ambapo anaitumikia mpaka hivi sasa. 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Saphinia Suleiman

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, career, skills development and technology.


Latest Post

Latest Tags