Vyakula vya kuzingatia ukifikisha miaka 40 na zaidi

Vyakula vya kuzingatia ukifikisha miaka 40 na zaidi

Wanasemaga uzee mwisho Chalinze mjini kila mtu kijana, sasa bwana kama unahitaji kuendelea kuwa kijana ungana nasi ili uweze kupata elimu kuhusiana na vyakula gani vitakufanya ubaki kuwa imara na mwenye nguvu muda wote.

Ikiwa miaka 40 ni umri muhimu sana na hatua muhimu katika maisha ya mtu yeyote, mara nyingi huja na marekebisho ambayo yanahitajika kufanywa ili kuboresha hali ya afya ya mtu binafsi.

Umeshawahi kufikiria ni kwa nini watu wengi kuanzia miaka 40 na kuendelea, huwa wanakumbana na changamoto mbalimbali za kiafya, jambo ambalo ni geni ukilinganisha na miaka ya 90 ambapo matatizo kama ya figo, moyo, kisukari hayakujitokeza kwa wingi kati ya watu wenye umri huo kama ilivyo hivi sasa.

licha ya umuhimu wa lishe bora kwa binadamu bado yapo mambo mengi ya kuzingatia, kati ya watu wenye umri kuanzia 40, kwani wanapaswa kutumia baadhi ya vyakula ambavyo vinafaida ya kujenga miili yao.

Waatalamu mbalimbali wamezungumzia umuhimu wa lishe bora kwa kuainisha ni aina gani ya vyakula watu wenye umri huo wanapaswa kuzingatia katika kuboresha afya zao.

Tovuti ya “Healthy Eating” wameeleza kuwa kwa watu wenye umri kuanzia 40, wanapaswa kutumia vyakula kama maziwa yanayotokana na mimea, karoti, matunda, pamoja na vyakula vya protini kama maharage ya soya.

Hata hivyo tovuti ya “Holmes place” nayo pia imeeleza baadhi ya vyakula ambavyo watu wenye umri huo wanapaswa kuvitumia ni pamoja na matumizi ya brokoli, matumizi mbalimbali ya viungo mfano tangawizi, na hata vyakula vyenye protein.

Hata hivyo licha ya umuhimu wa lishe kwa mwili wa mwanadamu, wataalamu mara nyingi hutoa elimu juu ya faida za lishe bora na kiwango cha chakula ambacho mtu anapaswa kula kwa ajili ya afya yake

Akizungumza na Mwananchi Ofisa Lishe Wilaya ya Temeke DK Charles Malale alisema kwa mtu aliefikisha miaka 40 au zaidi anapaswa kutumia mlo kamili ambao unamchanganyiko wa makundi yote matano ya vyakula.

Pamoja na kuwa mtu huyo atatumia mlo kamili wenye mchanganyiko huo wa makundi yote matano ya chakula lazima awe anatumia zaidi vyakula vinavyo jenga na kuimarisha mwili kutoka katika makundi hayo matano.

“Matumizi zaidi ya mboga mboga kwa watu wenye umri tajwa huwasaidia zaidi kwani huwa na madini na vitamini zinazo saidia kulinda na kuimarisha mwili” alisema Malale

Dk Malale pia alisema kadri umri unavyo zidi kwenda mfumo wa umeng’enyaji chakula (digestion system) utendaji wake wa kazi hupungua, ndio maana watu wenye umri zaidi ya miaka 40 hushauriwa kutumia mara nyingi vyakula ambavyo huwa rahisi kumeng’enywa.

“Matumizi ya nafaka zisizokobolewa kama mahindi, mtama, ulezi, ngano, mimea jamii ya kunde hasa maharage ya soya pamoja na matumizi ya matunda” alisema.

Pamoja na hayo Dk Malale alisema, watu wanatakiwa kupunguza kula vyakula vinavyo hifadhiwa kwenye makopo.

“Kupunguza kiwango cha chumvi katika chakula, hata kupunguza matumizi ya nyama, karanga na siagi” alisema Malale

Kudhibiti matumizi ya dawa za mitishamba au dawa za hospitalini bila maelekezo ya daktari kwani ni hatari kiafya

Hata hivyo Mtaalamu wa Lishe kutoka Hospitali ya Muhimbili Asina Yusuf alisema, mtu mwenye umri kuanzia 40 anahitaji lishe bora ambayo itamfanya kuwa na afya pamoja na nguvu.

“Kwa watu wenye umri kuanzia 40 na kuendelea wanatakiwa kuepuka vyakula vya kukaangwa kwani huleta madhara katika mwili endapo wakitumia kwa wingi” alisema Asina

Matumizi ya vitoweo kuku, samaki, nyama, ndizi, viazi mbadala wa mapishi haya ya kukaanga ni kuoka na kuchoma.

Watu waachae kufurahia ladha ya mafuta mengi badala yake watumie viungo vya chakula kuboresha ladha na wapike kwa mafuta kidogo alisema.

Hata hivyo vyakula vyenye ranti tofauti tofauti humpa mtu mtu virutubishi mbalimbali, hivyo matunda mbalimbali hushauriwa kutumika kwa wingi kwa watu wenye umri tajwa.

Kwa kutumia vyakula hivyo husaidia kupunguza hatari ya kupata magonjwa sugu yasiyo ambukizwa kama kisukari, presha, saratani, pamoja na magonjwa ya moyo.

Pia inashauriwa kupunguza, ikibidi kuacha pombe aina zote za soda na sharubati bandia kwani hivi huongeza hatari ya kupata magonjwa sugu yasio ambukizwa.

“Pamoja na hayo ni muhimu sana kushughulisha mwili na kufanya mazoezi angalau nusu saa kwa siku” alisema. 

 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags