Vijijambo vinavyoongeza upendo kwa mwenzi wako

Vijijambo vinavyoongeza upendo kwa mwenzi wako

  1. Kumbatio la ghafla kutokea nyuma

Mwanamke huwa anajisikia vizuri sana akikumbatiwa kwa nyuma na mpenzi wake kwa kushtukizwa, labda kwa mfano yuko jikoni anapika halafu mwanaume akanyata na kumkumbatia na kijibusu cha pembeni ya shavu.

Hapo mwanamke lazima ajisikie vizuri kwa sababu kwa mwanamke kukumbatiwa kutokea kwa nyuma, mwanamke anaamini kwamba mwanaume anampenda kupita kiasi.

  1. Kumsifia kwa kutaja kitu kimojawapo kati ya vingi vilivyomfanya kupendeza badala yakumwambaia mwanamke umependeza kijumla jumla, ni vyema mwanaume akataja kitu kimojawapo kati ya vingi alivyovaa ambacho kimempendezesha au eneo mojawapo la mwili wake ambalo lina mvuto au limekuvutia.

Kwa kawaida wanawake hupenda kusifiwa vipande vipande. Kwa mfano ukimwambia mwanamke kwa ujumla wake kuwa yeye nimzuri na amependeza; haoneshi kufurahi, bali ataishia tu kusema ‘ahsante.’Lakini ukimwambia kuwa sehemu au kipande fulani cha mwili wake ni kizuri, mfano macho, nywele, kiuno, makalio, nk.

Hapo atafurahi sana na kutoa kicheko cha aina fulani kuashiria kuwa sasa karidhika, hatimaye jamii imemtambua kuwa yeye ni mwenye kitu fulani bora kuliko wanawake wenzake

  1. Kutembea barabarani mwanaume akiwa pembeni yake

Wapo baadhi ya wanaume anatoka na mkewe kwenda mahali fulani halafu anamwambia atangulie yeye atakuja nyuma au anamwacha hatua kadhaa nyuma anatembea haraka haraka kama anakimbizwa huku mwanamke anakazana kumfuata jasho likimtoka…

Hiyo si sawa, mwanamke anapenda sana mwanaume ambaye wakati wanatembea barabarani iwe wanakwenda mahali fulani au kwa matembezi tu ya jioni kusalimia ndugu jamaa na marafiki au hata kwa mtoko wa kwenda kupata nyama choma na moja moto na moja baridi.

Basi huyo mpenzi wake awe wanatembea akiwa pembeni yake huku wakati mwingine akimshika mkono kuonyesha ishara ya upendo au hata ile kuwa ubavuni mwake humpa mwanamke raha ya pekee, lakini mbio za marathon kama mnakwenda kutoa damu hospitali ili kuokoa maisha ya mgonjwa hiyo haipendezi na wanawake wengi hawafurahii jambo hilo.

  1. Kumshika kiunoni au kumpapasa kwenye mabega wakati wa kusalimiana baada ya kutoka kazini. Mwanaume ametoka kazini anamkuta mkewe nyumbani anaingia tu vuuuum hadi chumbani na salaam anaitoa akiwa huko chumbani au wakati anaingia hapo nyumbani kwa kasi ya ajabu kama ametoka kufukuzwa.

Mwanamke anapenda mpenzi wake anaporudi na anapomkuta nyumbani ampokee mkoba wake na wanaposalimiana, ile kushikwa kwenye nyonga au kupapaswa mabegani kama vile anafanyiwa masaji kunampa raha sana na anajihisi kama kiumbe pekee mwenye bahati ya kupendwa.

  1. Kumshika mkono wakati mnapotembea kwenye mkusanyiko wa watu.

Isiwe ni kama unamburuza au unamlazimisha safari, inatakiwa kumshika mkono kwa namna ambayo itaonyesha kwamba unampenda, unamjali na unamlinda. Lakini pia inaonyesha ni namna gani unajisikia fahari kuwa naye.

  1. Kukumbushia mazungumzo yenu ya siku za nyuma, hususan kuhusu jambo alilowahi kulizungumzia.

Wanawake ni wazungumzaji wazuri, na wanaopenda kusikilizwa. Kwa hiyo jukumu kubwa wanalopaswa kuwa nalo wanaume ni kuhakikisha wanawasikiliza wenzi wao pale wanapozungumzia jambo fulani au wanapohitaji kusikilizwa.

Tatizo kubwa tulilonalo wanaume wengi, ni kutokuwa wasikivu kwa wenzi wetu na kukimbilia kuhitimisha mjadala kwa kujifanya tumewaelewa.

Kuzungumzia jambo ambalo wenzi wetu waliwahi kulizungumza siku za nyuma tunakuwa tumewapa ujumbe kwamba tulikuwa tunawasikiliza na tuliwaelewa, jambo hili linawafurahisha sana wanawake na kuwafanya wazidi kutupenda na kutujali, lakini huu ni mtihani mgumu kwa wengi…… 

  1. Kusema ahsante hata kwa jambo dogo.

Katika mambo ambayo yanawafurahisha wanawake wengi na kujihisi kwamba wenzi wao wanawajali na wanathamini mchango wao ni mwanaume kuonyesha kuridhishwa hata pale wanapofanyiwa jambo dogo. Mwanaume unaamka asubuhi, unakuta umeandaliwa maji ya kuoga na wakati unajizoa zoa kitandani mwenzi wako anakupa taulo mkononi, lakini unalinyakua kama vile unamnyang’anya badala ya kulipokea na kusema ‘ahsante’ kwa upendo. Huo siyo ustaarabu. Ni vyema tukaonyesha uungwana kwa kusema ahsante kwa wenzi wetu hata kama tumetendewa jambo dogo kiasi gani






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Shaban Kaluse

A Sales and Marketing in the hospitality Industry and also a freelance journalist, writing about love and relationships and educative articles which aims for youths, every Tuesday on Mwananchi Scoop.


Latest Post

Latest Tags