Tasnia ya maigizo ya uchekeshaji wiki hii ilipokea taarifa nzuri baada ya kuzinduliwa kwa tuzo za kwanza za wachekeshaji ambazo zinafahamika kama 'Tanzania Comedy Awards'. Tuzo hizo zimezinduliwa Januari 15, 2025 chini ya muanzilishi ambae ni msanii wa Bongofleva, Ommy Dimpoz kupitia kampuni yake ya The Plug akishirikiana na wadau wengine wa burudani huku Serikali kupitia Wizara ya Sanaa na Baraza la Sanaa la Taifa 'Basata' wakishirikiana na Bodi ya Filamu wakiwaunga mkono ujio wa tuzo hizo.
Tuzo hizo ambazo zitawaniwa Februari 14, 2025 zitakuwa na vipengele 21 ambapo mpaka sasa vimetajwa vipengele 17 ikiwa ni pamoja na Mchekeshaji Bora wa Mwaka, Mchekeshaji Bora wa Kike, Mchekeshaji Bora wa Kiume, Clip Bora ya Mwaka, Clip Bora ya Ushirikiano ya Mwaka, Mchekeshaji Mbunifu wa Mwaka, Kiongozi Mchekeshaji wa Mwaka, Jukwaa Bora la Vichekesho la Mwaka n.k.
Mwananchi Scoop imepata nafasi ya kuzungumza na muanzilishi wa tuzo hizo, Omary Nyembo maarufu Ommy Dimpoz na kuelezea namna alivyopata wazo la kuja na tuzo hizo ambapo amesema alilipata wakati anaumwa kwani alikuwa ni mpenzi sana wa kufuatilia vichekesho na wachekeshaji ili kujifariji na maradhi yaliyokuwa yakimsumbua.
"Unajua nimeumwa kwa muda mrefu mpaka nilikuwa najihisi kama nachanganyikiwa, kwa hiyo kitu pekee kilikuwa kinanifanya ni kuingia kwenye kurasa mbalimbali za wachekeshaji ili nipate faraja nicheke kwa sababu kipindi naumwa nilikuwa nafanyiwa upasuaji mara kwa mara na ilitakiwa nisaini kifo kila upasuaji kwa hiyo nilitumia wachekeshaji kama sehemu ya kujifariji," amesema Ommy Dimpoz.
Dimpoz ameongeza kuwa kwake aliamua kuja na tuzo hizo kama njia ya kurudisha fadhila zake kwenye tasnia ya uchekeshaji kwa sababu ni kama ilikuwa anadaiwa na tasnia hiyo.
Ommy Dimpoz anazitaja tuzo hizo kuwa za kipekee kwani ukiachilia mbali kila mshindi kupata heshima ya kubeba tuzo lakini pia atapata fursa ya kuondoka na pesa taslimu kwa kila mshindi . Mfano ametaja mshindi wa Tuzo ya Mchekeshaji Bora wa Mwaka atapokea tuzo na shilingi milioni 30, Mchekeshaji Bora Wakike na Wakiume watapata tuzo zao pamoja na shilingi milioni 20 kwa kila mmoja na washindi wa tuzo zingine zote watapokea tuzo zao na shilingi milioni 5 kila mshindi.
Upekee wa tuzo hizo ukatusukuma Mwananchi Scoop kuwatafuta baadhi ya wachekeshaji ambao wanafanya vizuri kwenye tasnia hiyo kwa sasa akiwemo Joti ambaye amewapongeza waanzilishi wa tuzo hizo lakini pia kuwapongeza wachekeshaji wa kizazi cha sasa kwa kuwa na bahati kubwa ya kusapotiwa na mitandao ya kijamii.
"Niwape hongera kwa kizazi hiki cha sasa cha uchekeshaji kuwa na bahati sana kwakuwa na mitandao yakijamii, watu wanaweza kuniona mimi kwanini ni wa kitambo lakini naenda sawa na wachekeshaji wa sasa, hiyo ni kwasababu naendana na dunia, najua mashabiki wanataka nini.
"Tunamshukuru Mungu waanzilishi wa hizi tuzo kutuwazia na sisi wachekeshaji maana imekuwa rahisi sana kwa wanamuziki kupata tuzo, imekuwa rahisi kwa watu wa filamu kuwa na tuzo ila kwa wachekeshaji tulisahaulika," amesema Joti.
Mchekeshaji Ndaro Mjeshi Kikofia ni mmoja wa walio hudhuria uzinduzi wa tuzo hizo, Mwananchi Scoop ilipata nafasi ya kuongea naye ameonesha hisia zake ujio wa tuzo hizo za wachekeshaji na kuzungumzia namna gani zitaongeza chachu kukuza tasnia hiyo.
"Tuzo hizi nimezipokea vizuri na natarajia zitakuwa poa kwa sababu ni kitu tumesubiria kwa muda mrefu, tuzo hizi zitaongeza ubunifu na uaminifu kwa wachekeshaji kwa ujumla, watu watapambana sana ili kuongeza ufanyaji wa kazi," amesema Ndaro.
Lakini pia mchekeshaji wa kike anayefanya vizuri kwa sasa, Asmah Majid ametoa shukrani zake za dhati kwa waandaaji wa tuzo hizo kwa kuwashukuru kuzileta na kutambua uwepo wa wanawake wanaofanya tasnia hiyo.
"Kiukweli mmetuona wachekeshaji hususani wa kike lakini yote kwa yote tunashukuru kwa kutusogezea hii fursa na sisi tutaipokea, asanteni," amesema Asmah Majid.
Lakini pia kwa upande wake Coy Mzungu ambaye amekuwa sehemu ya kupambania Sanaa ya uchekeshaji kwa kuanzisha jukwaa la Cheka Tu, amezungumzia kuhusu watu wanaokosoa na kuwataka kuwapongeza wadau waliofanikisha tuzo hizo.
"Kabla hatujafanya chochote tuache kwanza tuzo zifanyike, tusikosoe, tuwaachie Basata na Bodi ya Filamu kufanya kazi yao," amesema Coy Mzungu.
Imezoeleka mara nyingi tuzo zinanazoanzishwa kutokuwa endelevu kutokana na sababu mbalimbali lakini Mwanzilishi wa Tuzo za Comedy Tanzania, Ommy Dimpoz amewatoa wasiwasi akiweka wazi kwamba amejipanga kukabiliana na changamoto zitakazojitokeza ikiwa ni pamoja na wakosoaji wa tuzo hizo.
"Tuzo zote duniani hazijawahi kuacha kukosolewa, niliwaza hili tangu naanza kutaka kufanya tuzo hizi," amesema Ommy Dimpoz
Leave a Reply