Tatizo la kukosa usingizi (insomnia)

Tatizo la kukosa usingizi (insomnia)

Watu wangu wa nguvu wa Mwananchi Scoop, tumerudi tena katika segment yetu ya afya na msimu huu tumekuja kivingine kabisa, mkae mkao wa kula tuko na mada zitakazokupatia mwongozo wa tatizo lako.

Tatizo la kukosa usingizi kitaalamu Insomnia linawapata mamilioni ya watu duniani. Insomnia ni hali ya mtu kushindwa kupata usingizi pale anapohitaji kulala. Kwa kawaida mwanadamu anatakiwa kupumzika kwa muda wa masaa 7 hadi 8. Ukosefu wa usingizi unaweza kuathiri ukosefu wa nguvu, hamu ya kufanya chochote (mood), kuathiri afya na utendaji kazi.

Dalili za tatizo la kukosa usingizi (Insomnia)

  • Kujihisi kuchoka au usingizi muda wa mchana.
  • Kuwa na mawazo, uwoga uliopitiliza na rahisi kukasirika
  • Kuwa vigumu kupata usingizi muda wa usiku
  • Kuamka mapema sana
  • Kuogopa kusinzia
  • Kupunguza ufanisi katika kufanya mambo na kusababisha ajali
  • Kupoteza umakini
  • Kupunguza au kupoteza uwezo wa kukumbuka

Sababu za kupata tatizo la kukosa usingizi (Insomnia)      

Tatizo la ukosefu wa usingizi hutokea kutokana na kuwa na msongo wa mawazo au kuwa na tabia zinazoharibu usingizi mfano; kutumia muda mrefu kwenye mitandao ya kijamii kama FaceBook, WhatsApp na Instagram. Sababu zingine ni kama;

  1. Tabia ya kutokulala vizuri, kutokuwa na ratiba maalumu ya muda muafaka wa kulala, kulala mazingira yasiyo rafiki kama sehemu chafu.
  2. Kula sana muda wa jioni au usiku kabla ya kulala; hii husababisha mtu kujisikia vibaya kutokana na kushiba sana, muda mwingine baadhi ya watu hupata kiungulio na hata kutapika.
  3. Msongo wa mawazo. Mtu akiwa katika hali hii, mfumo wa usingizi unaoongozwa na hypothalamus unashindwa kufanya kazi kwa usahihi na kupelekea kushindwa kulala.
  4. Matatizo ya afya ya akili: kama woga, kuna baadhi ya watu ikifika usiku wanaanza kujitisha wenyewe na wengine kufikiria vitu vibaya mfano kifo n.k
  5. Matumizi ya dawa. Baadhi ya dawa huathiri ukawaida wa upatikanaji wa usingizi kwa mtumiaji, mfano wa dawa hizo ni kama dawa za pumu, dawa za kupunguza msongo wa mawazo (antidepressants) na dawa za shinikizo la damu.
  6. Matatizo ya kiafya; kama kisukari, shinikizo la damu, kansa, ufanyaji wa kazi kupita viwango wa tezi iitwayo thyroid, saratani n.k
  7. Matatizo ya kushindwa kupumua unapolala; tatizo hili hufanya mtu kukosa hewa na kuamka kila mara anapopata usingizi. Wagonjwa wa pumu hukumbana na hili mara kwa mara.
  8. Matumizi ya kahawa, pombe na uvutaji wa sigara. Kahawa humfanya mtumiaji kukosa usingizi pia sigara na pombe humfanya mtumiaji kulala katika hatua za awali na kushtuka katikati ya usingizi.

 

WATU WALIO KATIKA HATARI KUPATA TATIZO LA KUKOSA USINGIZI (INSOMNIA)

  1. Wanawake; kutokana na uzalishwaji wa homoni wakati wa mzunguko wa hedhi na kusimama kwa hedhi (menopause) husababisha tatizo hili. Pia ujauzito ni chanzo cha insomnia ingawa huisha baada ya kujifungua.
  2. Watu wenye umri zaidi ya miaka 60; husababishwa na kubadilika kwa ratiba ya kulala na kudhoofika kwa afya uzeeni.
  3. Watu wasio na ratiba maalumu ya kulala; hii husababisha kuathiri mfumo wa kulala na kuamka.
  4. Watu walio na tatizo la msongo wa mawazo.

ATHARI ZA KUKOSA USINGIZI (INSOMNIA)

  1. Kupata matatizo ya akili kama msongo wa mawazo, woga n.k
  2. Kupunguza ufanisi katika kazi na masomo.
  3. Kuongeza ukubwa wa matatizo ya moyo kama shinikizo la damu.

NJIA ZA KUZUIA TATIZO LA KUKOSA USINGIZI

  1. Hakikisha unaweka ratiba ya kulala na kuamka endelevu.
  2. Epuka kula sana usiku kabla ya kulala.
  3. Yaandae mazingira ya chumba cha kulala kuwa nadhifu.
  4. Epuka unywaji wa pombe na kahawa.
  5. Pata muda wa kupumzika na kufanya mazoezi.
  6. Punguza matumizi ya dawa zinazopelekea tatizo hili.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Detricia Pamba

A Digital Journalist, Content Creation Executive at Mwananchi Communications Ltd and Chief Editor of Mwananchi Scoop. I'm also writes stories around Technology, every Wednesday on Mwananchi Scoop. My other famous segments on Mwananchi Scoop include LISTI and WHO’S HOT.


Latest Post

Latest Tags