Simulizi: Kwa Udi na Uvumba

Simulizi: Kwa Udi na Uvumba

Na Innocent Ndayanse

“…Nilikuwa nimekutengea milioni hamsini ndani, sio za kufuata benki” yalikuwa ni maneno yaliyojirudiarudia kichwani mwake mara kwa mara na kumtia hamasa ya kujipatia pesa hizo siku hiyohiyo, iwe, isiwe. Kama ziko humo ndani kwanini asijitwalie?

Ni kazi ndogo tu, kuwaonyesha mdomo wa bastola yake au ya Panja, itatosha kuwatia jakamoyo.

Kitakachofuata baada ya hapo ni kazi moja tu; upekuzi mkali kila mahali hadi pesa zipatikane. Kwamba, ni hatua ipi itakayofuata baada ya kufanikiwa kuzitia fedha katika milki yake halikuwa jambo lililotwaa nafasi akilini mwake wakati huo. Alijua kuwa mambo yote yatajiweka sawa kadri jambo moja baada ya jingine litakapotekelezwa. Na alitambua fika kuwa Panja alikuwa akisubiri maagizo ya utekelezaji toka kwake. Hivyo aliamua kuutumia muda huo kuanza utekelezaji wa hatua mojawapo.

Aliichomoa bastola yake haraka, akaielekeza usoni pa Nassor Khalfan na kwa sauti nzito lakini yenye kuashiria kifo, alisema: “Usidhani kuwa tunafanya mchezo wa kuigiza. Sema, utatoa milioni kumi au hutoi, biashara imalizikie kichwani mwako.”

Lilikuwa ni tukio ambalo Nassor Khalfan na wenzake hawakulitarajia. Kwa muda waliduwaa wakitazamana na domo la bastola hiyo.

“Nakupa sekunde kumi tu za kutoa tamko,” Kipanga aliendelea. “Zaidi ya hapo tuna hiari ya kufanya chochote kile tupendacho. Upo hapo?”

Nassor Khalfan alifikiri harakaharaka. Mbele yake alitazamana na ‘kifo.’ Kwa jinsi alivyomfahamu Kipanga, kosa lolote dogo lingeharakisha kifo chake. Lakini aliamini kuwa uamuzi wowote unaotokana na woga husababisha majuto baadaye.

Kwamba, kama angekubali kuchukua gari hilo kwa shilingi milioni kumi ilhali amekwishamtamkia kuwa amemtayarishia milioni hamsini kwa ajili ya Benz, isingemwia vigumu Kipanga kumtia risasi kisha kuvivamia vyumba na kuvipekua akizisaka hizo milioni hamsini.

Huenda angeendelea kuifikiria mbinu ya kulitatua tatizo hilo lililozuka ghafla kama asingetupia macho kwa Panja na kukumbana na yaleyale! Domo la bastola!

Kwa fadhaa alijikuta akiropoka: “Msiniue! Nitawapa pesa hiyo…! Tafadhali…!”

Hakumalizia lolote alilotarajia kuongeza. Mlipuko mkubwa ulitokea. Sekunde mbili baadaye milipuko mingine miwili ikatanda. Kipanga alimzamishia Nassor Khalfan risasi ya kichwani kisha akamlisha mmoja wa wale wageni risasi ya kifuani, wakati kwa mara ya kwanza Panja alijaribu kuitumia bastola kwa kumfyatulia risasi Mwarabu mwingine, risasi iliyozaa matunda kwa kuzama kifuani na kuyakatisha maisha yake papohapo 

Kilichofuata baada ya hapo kilichukua muda mfupi zaidi, kitu kama dakika tatu tu. Kipanga alimhimiza Panja aweke ulinzi mlangoni na yeye akatokomea katika chumba kimoja ambako alichakurachakura na kufanikiwa kuliona begi dogo ambalo alilifungua na kushuhudia mafurushi ya noti.

Hakuchelewa, alilibeba begi hilo na kutoka kwa kasi ileile.

“Twende,” alimwamuru Panja.

Wakatoka.

 “Tunakwenda wapi?” Panja alimuuliza wakati Kipanga akiling’oa gari kwa makeke.

Kipanga hakujibu. Mawazo yake hayakuwa hapo tena. Kuna lililokwishajipenyeza kichwani wakati huo na akawa katika fikra za kulipatia ufumbuzi wa haraka. Gari lilizidi kusaga lami ya Barabara ya Morogoro kwa kasi iliyowashangaza waliokuwa kando ya barabara hiyo.

“Vipi, inakuwaje?” Panja alihoji kwa mshangao. “Yaani tunarudi town? Ni noma msh’kaji wangu!”

Kipanga hakutamka lolote, na kuhusu hilo, hakuwa mtu wa kuambiwa chochote. Alitambua fika kuwa kupora gari hilo, kumuua dereva na kuitupa maiti yake kando ya barabara, kisha wakawaua wale Waarabu kule Kibaha, ni matukio ambayo yangelifikia Jeshi la Polisi baada ya muda mfupi sana.

Na hapo ndipo msako mkali utakapoanza, msako ambao aliamini kuwa ungechukua siku chini ya tatu kutoa matokeo. Kwamba matokeo hayo yatakuwa mazuri kwake, hilo halikuwa ni jambo lililopata nafasi yoyote akilini mwake. Alijua kuwa Jeshi la Polisi lingeingia kazini kwa nguvu za kifaru, na lingepata kile linachokihitaji; kuwatia mbaroni na kuwafungulia mashtaka ya mauaji na wizi wa kutumia nguvu.

Lakini alikuwa na sababu iliyomfanya aamue kurudi Dar es Salaam, sababu ambayo hakuwa tayari kuiweka bayana kwa Panja hadi hapo muda mwafaka utakapotimu. Akakaza macho mbele, mikono ikiwa imeushika usukani kwa makini huku mguu wa kulia ukiwa umeganda kwenye kibati cha mwendo, gari likiwa katika kasi ya kutisha.

Sasa walikuwa katika sehemu isiyokuwa na nyumba yoyote, picha iliyomtia matumaini Kipanga katika kutekeleza lile alilodhamiria.

Alianza kupangua gia moja baada ya nyingine, gari likapunguza mwendo taratibu, hatimaye akaliegesha pembezoni mwa barabara. Hatua iliyofuata ilikuwa mithili ya mchezo wa kuigiza au ndoto isiyopendeza kichwani mwa Panja. Kipanga aliichomoa bastola yake na kumwelekezea Panja usoni.

“Hilo kopo nililokukabidhi halina kitu tena,” alimwambia. “Lakini huenda likakusaidia huko mbele ya safari. Pambana na makali ya maisha kwa kutumia kopo hilo. Ukiwa na gololi mbili, tatu hutakosa kupata pesa kutoka kwa mtu yeyote. Kwa sasa teremka, uhusiano wetu umekomea hapa.”

Yalikuwa ni maneno yaliyopenya masikioni mwa Panja kwa usahihi mkubwa. Alisikia, akaelewa lakini hakuamini.

“Teremka! Toka!” Kipanga alifoka. “Nina muda mfupi sana wa kuendelea kukuhurumia. Ukizidi kuchelewa utanipa kazi nyingine ngumu ya kuutoa mzoga wako…”

Panja alimfahamu vizuri Kipanga. Alitambua  jinsi asivyojua kuwa mzaha au utani ni mdudu wa aina gani. Kwa maneno haya aliyoambiwa na Kipanga, hakuhitaji tena kukipa kichwa kazi ya kupambanua kama huo ni mchezo wa kuigiza au ndoto isiyopendeza. Ni dhahiri Kipanga alikuwa hana masikhara.

Taratibu alifungua mlango na kutoka huku akilikodolea macho lile begi aliloamini kuwa  lilisheheni pesa, tena pesa nyingi. Ni kwa kutambua kuwa pesa ziko hapo, ujasiri ukamjia kwa nguvu kubwa kiasi cha kufumbua kinywa na kwa sauti ya chini, sauti nzito na yenye msisitizo mkali  akasema, “Utakuwa mstaarabu sana kama utanipa mgawo wangu…”

“Nini?!” Kipanga alimtazama kwa macho makali na kufuatisha kicheko cha dhihaka. “Hakuna cha mgawo tena hapa! Nimekuachia hiyo bastola ambayo thamani yake ni kubwa sana. Itumie kwa kupata pesa. Sidhani kama utakosa kunishukuru kwa wema huo niliokutendea. Sidhani.”

“Lakini…”

“Hakuna cha ‘lakini’ tena. Toka!”

Panja hakuwa na la kufanya, zaidi ya kujiengua

Panja hakuwa na la kufanya, zaidi ya kujiengua taratibu na kushuhudia gari likiyoyoma machoni pake kwa kasi ya kutisha. Akaachwa kaduwaa. Ikamlazimu kusota akivizia gari hili na lile kwa machale kwani tayari alijua kuwa Polisi watakuwa wakiwasaka, hivyo alipaswa kuwa makini.

Baada ya dakika kumi hivi, basi moja liliutii mkono wake, dereva akaegesha pembezoni mwa barabara. Akaingia kwa unyonge, mfukoni akiwa na shilingi 5,000 tu alizotoka nazo nyumbani.

Itaendelea………………………….






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Detricia Pamba

A Digital Journalist, Content Creation Executive at Mwananchi Communications Ltd and Chief Editor of Mwananchi Scoop. I'm also writes stories around Technology, every Wednesday on Mwananchi Scoop. My other famous segments on Mwananchi Scoop include LISTI and WHO’S HOT.


Latest Post

Latest Tags