Simulizi: Kwa Udi na Uvumba 04

Simulizi: Kwa Udi na Uvumba 04

Na Innocent Ndayanse

Sehemu ya 04

Panja akakohoa kidogo kisha akamuuliza, “Hushangai kuona mara nipo, mara sipo?”

“Hata nikishangaa itanisaidia nini? Najua kawaida ya mwanaume ni kuhangaikia maisha.”

Panja aliachia tabasamu la mbali, tabasamu ambalo alilikata ghafla na kusema, “Ndiyo, ni kawaida ya mwanaume kufaitia maisha, lakini si kwa mfumo kama huu wangu.”

“Mfumo gani?”

Kwa mara nyingine Panja alimtupia macho Hilda. Nuru hafifu ya rangi ya bluu iliyotoka kwenye globu iliyoning’inia darini iliuongeza uzuri wa mwanamke huyo ambaye wakati huo, zaidi ya nguo laini ya ndani, hakuwa na vazi jingine mwilini. Kulingana na ujenzi bora wa umbo lake teketeke, macho yake malegevu yakisihi badala ya kushinikiza, na kwa jinsi alivyolala kihasara-hasara pale kitandani, isingekuwa rahisi kwa mwanamume rijali aendelee kumtazama hata kwa dakika tano kabla hajamparamia kwa uchu usiokadirika.

Ndiyo, angekuwa ni mwanamume mwingine, siyo huyu Panja ambaye kwa wakati huo, kutokana kuathirika kisaikolojia, hakuwa hata na wazo kuhusu mwili huo mzuri uliokuwa kando yake. Aliendelea kumtazama Hilda kisha akasema, “Kachukue funguo kwenye ile suruali niliyoivua.”

Hilda alijitoa kitandani na kufanya alivyoagizwa.

“Fungua droo ya chini, kabatini,” agizo jingine.

Kama awali, Hilda alitii agizo hilo la pili. Papohapo mshtuko mkubwa ukampata! Ndani ya saraka kulikuwa na kitu kimoja tu, bastola! Akilini mwa Hilda, tangu aanze kuishi na Panja, hakuwahi kubaini kuwa Panja alimiliki chombo hicho.

Taharuki ikiwa imejikita akilini na usoni pake, alikurupuka na kuiacha saraka hiyo wazi, akasimama kando na kumkazia macho Panja, utazamaji uliojitenga na masikhara kwa maelfu ya kilometa. Akawa akihemea juu, juu.

“Ni nini hiki?!” hatimaye alihoji kwa sauti yenye kitetemeshi cha mbali.

Badala ya Panja kujibu, alitabasamu kidogo, akauwasha msokoto wake wa bangi na kuvuta mkupuo mmoja wa nguvu kisha akauzima. Harufu kali ya bangi hiyo lilikuwa ni jambo lililokwishazoeleka kwa Hilda. Haikumkera. Lakini hii bastola!

“Panja ni nini hiki?” aliuliza tena.

“Sidhani kama unaweza kuwa mshamba wa kutokukitambua chombo hicho,” Panja alijibu kwa sauti ya chini, akionesha dhahiri kujiamini kwa kiwango kikubwa.

“Kimefikaje humu?”

“Kimeletwa na jini.”

“Panja, ni silaha hii, Panja!” Hilda alisema kwa sauti ya woga.

“Ndiyo, kwani unadhani mie naichukulia kama toyi?”

Hilda alisonya, kisha akauliza, “Ni ya nani?”

“Ni ya padri mmoja amenipa nimtunzie.”

“Padri?!” Hilda alishangaa. “Panja mbona unaleta mzaha kwa jambo zito kama hili?”

Sasa badala ya kutabasamu, Panja aliachia kicheko hafifu, kisha akasema, “Rudi kitandani tuzungumze. Tatizo lako ni papara. Njoo nikupe ukweli wenyewe, baby.”

Akiwa bado amechanganyikiwa, Hilda alimfuata Panja kitandani ambako sasa alivuta shuka na kuusitiri mwili wake. Wakatazamana tena.

“Iwe ni siri yako,” Panja alisema kwa sauti ya mnong’ono, sauti nzito, yenye msisitizo mkali. “Ikivuja, ndipo utakaponitambua vizuri kuwa mimi ni nani. Sikufichi; kazi yangu ya kunipatia pesa inakitegemea kifaa hicho.”

“Mamaa!” Hilda alibwata kwa sauti ya chini. Hakuhitaji ufafanuzi zaidi wa kauli ya Panja. Sasa aliijua vizuri kazi ya mwanamume huyo. Kwa mbali mapigo ya moyo wake yaliongeza kasi. Alikumbwa na jakamoyo.

“Usishangae,” Panja aliendelea. “Usidhani kila mtu aliyetajirika au kuwa na kiwango kizuri cha maisha amefanikiwa kwa kutumia njia halali tu. Hapana. Kuna wezi wa kalamu, ambao ni wakongwe wa kughushi. Kuna walioanzia kupata pesa kwenye shughuli ndogo ndogo za halali, na Mungu akawajalia hadi wakatajirika. Na kuna waliotajirika kwa kupora mamilioni ya pesa na wasikamatwe, leo hii wanatanua.

“Mimi nimo katika kundi hilo la mwisho, kundi la kufukuzana na dola. Lakini naamini ipo siku nitaiacha kazi hii. Nitaiacha nikiwa tayari n’na pesa inayoeleweka. Kuna haja gani ya kufanya kazi ya roho mkononi kama tayari mtu una kitu kama milioni ishirini au thelathini ndani?”

Akatulia kidogo na kumtazama Hilda sawia.  Akahisi kuwa kwa kiwango kikubwa maneno hayo yamemwingia.

“Unasikia mpenzi,” aliendelea. “Huenda leo nd’o ningechukua uamuzi wa kujipumzisha au kustaafu kazi hii. Ningechukua uamuzi huo kama ningerudi na pesa tulizopata na Kipanga. Na huenda kesho asubuhi ningeripoti kwenye duka la magari na jioni kitu chenye miguu minne kingekuwa kimepaki hapo nje kikilindwa na Mmasai mwaminifu.”

Baada ya ksema hivyo, Panja aliachia kicheko hafifu, kicheko cha uchungu, kicheko ambacho hata Hilda alipomtazama usoni alibaini kuwa ni kicheko kilichoficha hasira kali nyuma yake.

“Panja, mbona sikuelewi? Naona kama unaanza kujifunza kuwa mtunzi wa hadithi au mashairi. Umeingia lini katika fani hiyo?” Hilda alimuuliza huku akimpapasa kifuani.

“Huenda kwako ni mashairi, au labda unaona nakusimulia hadithi ya kubuni. Lakini naomba uniamini; huo ni ukweli mtupu, sio mashairi wala hadithi ya kubuni.”

Mkono wa Hilda ulikuwa umekiacha kifua cha Panja, na sasa ulikuwa ukiendelea kufanya ziara katika sehemu nyingine. “Sikiliza, Panja,” hatimaye alisema kwa mnong’ono. “Tuna usiku mfupi sana na tuna mengi ya kuzungumza na kufanya. Unaonaje, fupisha mazungumzo tufurahi kidogo.”

Panja alicheka kidogo, kicheko kilekile ambacho hakikuwa hata na chembechembe za furaha halisi. Kisha akasema, “Si vibaya kama leo tutaahirisha hayo mengi mengine, na tukakamilisha hili ninalokueleza.”

“Lakini…” Hilda alisema na kusita baada ya Panja kuutoa mkono wake ambao wakati huo ulikuwa mahala fulani ukipapasa kwa namna iliyomtia Panja wazimu wa mbali kiasi cha kujikuta akishusha pumzi ndefu.

Itaendelea……………..

 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Detricia Pamba

A Digital Journalist, Content Creation Executive at Mwananchi Communications Ltd and Chief Editor of Mwananchi Scoop. I'm also writes stories around Technology, every Wednesday on Mwananchi Scoop. My other famous segments on Mwananchi Scoop include LISTI and WHO’S HOT.


Latest Post

Latest Tags