Shilole mbioni kufunga ndoa ya nne

Shilole mbioni kufunga ndoa ya nne

Msanii wa Bongofleva, Bongo Movies na mjasiriamali, Zuwema Mohammed 'Shilole', amesema atafunga ndoa na mpenzi wake wa sasa muda si mrefu ujao, ikiwa ni ndoa yake ya nne tangu alipoolewa kwa mara ya kwanza akiwa na umri wa miaka 17.

Shilole ambaye hakutaka kutaja jina la mpenzi wake huyo mpya aliyemtambulisha kwa picha hivi karibuni, ameliambia Mwananchi kuwa kila kitu kuhusui ndoa hiyo mpya atakiweka wazi siku ya ikifika.

Amesema haoni aibu wala haya kuolewa tena au kusemwa na watu kuwa anaolewa na kuachika kila wakati, ila wajue siri kubwa anaijua yeye mwenyewe hivyo watu waendelee kuongea tu, yeye hajali.

"Mimi napenda ndoa na kama mwanaume amejitokeza anataka tufunge ndoa kwanini nikatae wakati ni jambo la heri? Mie siogopi maneno ya watu kuambiwa naolewa sana na kuachika, ila ukweli naujua mimi na ndio maana naolewa tena soon na mchumba wangu wa sasa hivi ambaye watu wananiona naye tu wala hawamfahamu kiundani, japo naona wana hamu ya kumjua tangu nilipomtambulisha."

Mwananchi lilimuuliza Shilole kuhusu kupewa talaka na Rommy 3D ambapo amejibu kila kitu ataweka wazi siku ya ndoa.

"Tulia ndugu yangu, siku ikifika utafahamu kila kitu, haina haja ya kuelezea mambo mengi kwa sasa isije kuharibu mipango yangu."

Shilole akifunga ndoa hiyo itakuwa ni ya nne baada ya awali kuolewa na dereva wa malori wakati akiwa na umri wa miaka 17, ambaye alikuja naye Dar es Salaam akitokea kwao Igunga ambako alikuwa tayari amepata mtoto wa kwanza. Akazaa mtoto mmoja kwenye ndoa hiyo, akiwa ni wa pili kwake. Baadaye mwaka 2009 akaachana na mwanaume huyo kwa talaka akimtuhumu kumpiga hadi kumdhuru mguu wake wa kulia.

Ndoa ya pili, Shilole ambaye pia hujiita Shishi Baby au Shishi Trump, alifunga na Ashraf Uchebe ambaye waliachana baada ya awali kuvuja kwa picha zikimuonyesha akiwa amejeruhiwa usoni kisha akaolewa na aliyekuwa mpigapicha wake, Rommy 3D ambaye wameachana miezi michache iliyopita.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags