Mwanamuziki wa Kenya, Bien amesema anakoshwa na msanii wa nyimbo za Injili Joel Lwaga na Saluu ambaye ni mshindi wa pili wa mashindano ya Bongo Star Search 2024-2025.
Bien ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam ambapo amekuja kwa ajili ya kutumbuiza kwenye shoo ya Darassa ‘Take Away The Pain Album Tour'.
“Mimi nikiangilia Tanzania 'Live Perfomance' huwa naangalia wale wasanii wenu wa nyimbo za Injili. Kuna mtu anaitwa Joel Lwaga ni mnyama balaa. Gospel kwa Tanzania hata hatuwagusi tukiimba live waimbaji wa Gospel Tanzania waache.
"Halafu kuna Star Search fulani niliona Tiktok kuna kijana alikuwa anaimba nyimbo za Diamond anaitwa Saluu. Huyo jamaa ni mnyama, live mimi sijaona mtu kama huyo Afrika Mashariki," amesema Bien.
Aidha msanii huyo alitia neno katika ishu ya Master Jay aliyodai Alikiba ni mbana pua.
“Master Jay acha kufanya hayo, hayapendezi kabisa, mimi binafsi sikupenda alichokizungumza. Halafu Afrika Mashariki sasa hivi ni muda wa kujenga, miaka mitano ijayo wakina Saluu watakuwa wanatuuliza nyie wazee mlikuwa mnafanya nini. Hatuwezi kuwaambia tulikuwa na bifu, lazima tufanye muziki kwahiyo Master Jay hicho ulichokifanya siyo sawa,” amesema Bien.
Mbali na hayo alifunguka kuhusiana na kinachomfanya aje Tanzania mara kwa mara.
“Mimi ndugu yangu ambaye namfuata ameoa Tanzania, ameoa Moshi, nimeenda mpaka Moshi nimekunywa mtori huko, nimekula nyama ya mbuzi laini. Pia nina stori moja na Ambwene 'AY' lakini hiyo siwezi isema hapa.
"Unajua Tanzania nadhani tulidanganywa na Wakoloni, walituchorea mipaka lakini ukiangalia kiuhalisia Watanzania ni kama Wakenya, chakula cha huku ni kama cha Kenya na kinaweza kuwa ni kitamu kuliko cha Kenya,” amemalizia Bien.

Leave a Reply