Ronaldo aitoa hoteli yake kuhifadhi manusura wa tetemeko la ardhi Morocco

Ronaldo aitoa hoteli yake kuhifadhi manusura wa tetemeko la ardhi Morocco

Jabali la soka ulimwenguni Cristiano Ronaldo ameamua kuitoa hoteli yake ya kifahari ya Pestana CR7 iliyoko Marrakech nchini humo kuwahifadhi manusura wa tetemeko lililotokea nchini Morocco na kusabababisha maelfu kuaga dunia.

Ronaldo ambaye ni raia wa Ureno amefikia uamuzi huo kufuatia tetemeko la ardhi kutokea nchini Morocco huku likiacha maelfu ya watu kukosa makazi na wengine kujeruhiwa.

Kwa mujibu wa tovuti ya Sports Brief, mwanasoka huyo mashuhuri anayekipiga Al-Nassr ya Saudi Arabia, ana msururu wa hoteli zinazozunguka Ulaya na Mashariki ya Kati, ametoa hoteli hiyo kama ishara ya huruma kufuatia tetemeko hilo baya.

Uwezo wa hoteli hiyo ya kifahari ya Pestana CR7 iliyoko wilaya ya M Avenue Marrakech yenye jumla ya vyumba 174 inaelezwa itasaidia manusura wengi katika eneo la mji wa kale wa jiji hilo la kitalii.

Lakini msaada huo wa gwiji Ronaldo sio pekee kutoka ulimwengu wa soka kusaidia wale walioathirika. Jumamosi timu ya taifa ya Morocco ilichangia damu kusaidia waathiriwa.

Beki wa Morocco Achraf Hakimi aliandika kwenye mtandao wa kijamii kuwa kwa niaba ya wachezaji wenzake anatoa pole kwa wananchi wenzao.

“Tunapitia wakati mgumu kwa wananchi wenzetu wote. Ni wakati wa kusaidiana kuokoa maisha ya wengi iwezekanavyo. Pole zangu kwa wote waliofiwa na wapendwa wao,” alisema Hakimi.

Usiku wa kuamkia Jumamosi tetemeko lenye ukubwa wa 6.8 lilipiga eneo la milima la High Atlas nchini Morocco, karibu na Mji wa Marrakech huku taarifa zikisema mtikisiko ulihisiwa hadi nchi ya jirani ya Algeria.

.
.
#MwananchiScoop
#BurudikaNasi






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Asha Charles


Latest Post