Mwanasaikolojia aeleza athari malezi na urafiki uliopitiliza wa Kajala na Paula

Mwanasaikolojia aeleza athari malezi na urafiki uliopitiliza wa Kajala na Paula

Amaa! Kweli siku zote mtoto umleavyo ndivyo akuavyo, ni maneno tuu ya Waswahili katika harakati zao za kukifanya Kiswahili kiweze kukua, wengi wetu neno hili tulikuwa tunalisikia tu kama maneno mengine lakini sasa ndiyo tunapata kuona yale yaliyomo kwenye neno hili na maana yake.

Tumeshazoea kuona wazazi wengi wanawapatia watoto wao malezi yaliyo bora na si bora malezi. Hii inasaidia mtoto kukua katika misingi mizuri ya malezi.

Kwa jamii yetu Mama kumfanya mtoto wake kuwa msiri wake kwa kumwambia hadi mambo ambayo mtoto hapaswi kushirikishwa inaonekana ni utovu wa nidhamu.

Kupitia mitandao ya kijamii kumekuwa na minong’ono na shutuma nyingi kuhusiana na suala zima la malezi ya mwigizaji Kajala Masanja kwa binti yake Paula je ni sahihi kwa mama kuwa na ushoga wa kupitiliza kwa mtoto.

Licha ya hayo wengi wao walikuwa wanatolea mifano ya baadhi ya wasanii maarufu kama vile Monalisa jinsi anavyomlea mwanaye Sonia, Shilole anavyowalimiti watoto wake kutojihusisha na mitandao ya kijamii, huku wakilinganisha na malezi ya Kajala kwa binti yake.

Team ya Mwananchi Scoop hatukuamua kulifumbia macho swala hili tukaamua kumtafuta mwanasaikolojia John Ambrose aweze kueleza iwapo Kajala yupo sahihi kwa malezi anayo mpatia mwanaye. 

Kwanza kabisa tulianza na swali ambalo baadhi ya watu ni la kawaida lakini kiuhalisia linahitaji ujuzi kulielewa anaanza kwa kueleza kuwa;

 “ Malezi bora ni malezi yanayozingatia mfumo wa afya, namaanisha misingi mikubwa minne ambayo ni ukamilifu wa mwili, ukamilifu wa akili, ustawi wa jamii, masuala ya imani na kiroho na mwingine ni msingi wa hisia. Haya ndiyo tunazungumza kuwa ni malezi bora. Ukiangalia hiyo misingi niliotaja hapa ndiyo unapata kuwa malezi yanaangalia mila, tamaduni na desturi.”  

Anafafanua zaidi akisema, “Ukiangalia sasa malezi ya mtu mmoja kutoka kwenye familia aidha mama au baba ambaye anaweza akatengeneza desturi yake na tamaduni zake na uelewa wa mawasiliano yao. Kwa hiyo ukimzungumzia mtu kama Kajala namna anavyolea maana yake ametengeneza umbile la malezi kuzingatia mila na desturi yake yeye kwa mwonekano wa shughuli na jamii inayomzunguka.”

 

“Kwa hiyo siwezi kuzungumzia kama malezi yake ni mabaya  au ni mazuri kutokana na aina katika msingi wa malezi mazuri au mabaya inazingatia kutokuwa na uwiano  wa jamii  inayokuzunguka,” amesema mwanasaikolojia Ambrose 

Duh! Mambo ni mengi muda ni mchache, kama kawaida yetu bwana tukamuuliza kuhusiana na suala zima la mtoto kuwa na urafiki (ushoga) wa kupitiliza na mama yake mzazi kama ilivyokuwa kwa Kajala na mwanaye Paula, amefunguka na kueleza kuwa…

“Tukizungumza suala zima la mtoto kumueleza au kuwa na urafiki na mzazi kuhusu yanayomsibu ni jambo la msingi sana hasa katika umri mdogo, kwa sababu mama lazima auvae ule uhusika wenyewe. Tunapo zungumza malezi ni hamisho la uhalisia wa baba au mama au jamii kulisishana kutoka mkubwa hadi mdogo ni kulisishana kihisia, kijamii, desturi na tamaduni.”

“Mtoto anapozaliwa unamrithisha kibaiolojia katika mwonekano wake wa sura na huzaliwa na weupe usiokuwa na lolote na ndio maana unaweza kushangaa mtu kusema hali ugali. Hii ni kutokana na namna ya malezi yako hukumlea katika ulaji wa vyakula hivyo. Kwa hiyo hatuli chakula kwa sababu tunakula ila tunakula kwa sababu tumekuzwa na vyakula hivyo,” amesema.

“Tunarudi palepale kuwa malezi ni lazima wazazi wakae katika uwiano wa watoto ili kuwarithisha yaliyo salama, kumlinda ili asipate maadili ambayo sio msingi wake,” amesema mwanasaikolojia huyo.

Kumekuwa na majadilio mengi kuhusiana na suala zima la afya ya akili, vilevile nasi hatukuwa na hiyana tukaamua kumuuliza Ambose kuhusiana na haya yanayotokea katika mitandao ya kijamii kuhusiana na Kajala kumlea mwanaye, je inaweza kuwa ni sababu ya matatizo ya afya ya akili…? 

“Sasa ni changamoto ya afya ya akili katika hili, malezi na makuzi vinamahusiano makubwa sana kwa sababu anaeenda kukabidhiwa hayo maridhiano, ni akili inakabidhiwa kuratibu mwili. Ustawi wa jamii inaratibiwa kutawala maisha mazima ya mtu na hilo ndio faili kubwa la mtu na akili ndo linabeba hilo faili. 


“Kama faili umelibebesha likiwa limeathirika katika misingi ya matumizi labda ya dawa za kulevya, kukosa utu na maadili, inakufanya unashindwa kuwa mstahimilivu, jasiri. Ni kwa sababu hakuandaliwa lile umbile lake la mwili halikuandaliwa kuwa mwenye hekima na yote niliyo yataja hapo juu,” amefafanua mtaalamu huyo.

Hivyo ukikosa hizo nyenzo, hiyo ni changamoto ya afya ya akili kwa hiyo usipompatia malezi bora mtoto wako yanapelekea kumuangamiza kwa maana kwamba zile nyenzo ambazo zinahitajika katika kukabiliana na maisha ya kila siku zinakuwa hazipo hatimaye sasa unaathirika kiakili,” amesema Mwanasaikolojia John Ambrose.

 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags