Michael Jackson na ishu ya kujichubua, kubadili pua

Michael Jackson na ishu ya kujichubua, kubadili pua

Kwa miaka mingi, mfalme wa pop, Michael Jackson, amekuwa akihukumiwa kwa mabadiliko makubwa ya ngozi yake. Wengi wanadai kuwa alitaka kubadilisha rangi yake na kuwa mzungu.Licha ya kuwa na maneno hayo ukweli ni kwamba mkali huyo alikuwa akisumbulia na ugonjwa wa ngozi uitwao Vitiligo, ambao ulimlazimu kubadilika bila ridhaa yake.

Inaelezwa alirithi ugonjwa huo kutoka kwa babu yake ambaye pia alikuwa nao. Na hata kaka yake, Jermaine Jackson, alithibitisha kupitia kitabu chake cha kumbukumbu kuwa MJ alikua na Vitiligo. Ugonjwa huo pia uliathiri mtoto wake wa kiume, Prince Jackson.

Vitiligo ni ugonjwa ambao huathiri ngozi na unaweza kupoteza rangi yake. Licha ya kuwa kuna dhana zinazodai unaathiri watu wenye ngozi nyeusi pekee, lakini ukweli ni kwamba mtu yeyote unaweza kumkumba.

MJ alithibitishwa rasmi kuwa ana Vitiligo na mtaalamu wa ngozi mwishoni mwa miaka ya 1980. Mbali na ugonjwa huo pia alikuwa na lupus, ugonjwa mwingine wa kinga ya mwili ambao unaweza kuathiri ngozi na kuchochea kupotea kwa rangi.

Ugonjwa wa Vitiligo haikuwa umeeleweka vizuri wakati huo, na ilisababisha shinikizo kubwa kutoka kwa jamii, pamoja na tuhuma zisizo za kweli dhidi yake. Hali hii ilimfanya Michael kuhisi kutokuwa na amani kuhusu mwonekano wake, na hivyo alilazimika kuvaa mavazi yenye mikono mirefu na kutumia vipodozi vikali ili kuficha mabadiliko ya ngozi yake.

Je, Michael Jackson alijichubua ngozi kwa makusudi?
Inaelezwa kuwa alitumia Benoquin, dawa maalum ya kutibu Vitiligo, siyo krimu ya urembo au mafuta ya kujichubua. Benoquin haiwezi kutumiwa na mtu asiye na ugonjwa huo.

Hata hivyo katika moja yake na Oprah Winfrey mwaka 1993, Michael alieleza kuhusu hali yake ya ngozi na kusema hakujichubua kwa hiari, bali ni Vitiligo ilisababisha mabadiliko hayo, pia akielezea jinsi tuhuma za kujichubua zinavyomuumiza.

Aidha aliwahi kufanya upasuaji mwaka 1979, baada ya kupata ajali alipokuwa akicheza na kuumia pua yake. Wakati wa upasuaji wa kurekebisha pua yake, aliomba ipunguzwe ukubwa wake, kwani alijisikia kutokuwa na amani kutokana na matusi aliyokuwa akipokea kutoka kwa baba yake kuhusu pua yake kubwa.

Baadaye, lupus ilianza kuathiri ngozi na tishu za pua, hali ambayo ilisababisha matatizo katika pua yake na kumpa ugumu katika upasuaji. Hii ilisababisha Michael kufanyiwa upasuaji wa mara kwa mara ili kurekebisha pua yake, na wakati mwingine alilazimika kuongeza upana wa pua ili kurejesha umbo lake la awali.

Mama yake, Katherine Jackson, alithibitisha kuwa upasuaji wa Michael ulijikita zaidi kwenye pua na kuongeza dimple (shimo) kwenye kidevu baada ya ushawishi wa daktari wake. Mabadiliko mengine ya sura yake yalitokana na kuzeeka, kupungua uzito, na athari za lupus.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Masoud Kofii


Latest Post

Latest Tags