Mfahamu Udit, mkali wa Masongi filamu za kihindi

Mfahamu Udit, mkali wa Masongi filamu za kihindi

Moja ya vitu vinavyowavutia watazamaji wa filamu za Kihindi ni zile nyimbo ‘Masongi’, ambayo husikika katika filamu hizo zikionesha waigizaji wakiimba.

Licha ya baadhi ya watu kudhani nyimbo hizo huimbwa na waigizaji wa filamu husika. Ukweli wa mambo upo hivi.

Takribani miaka 30 katika filamu za India, sauti ya Udit Narayan ndio imekuwa ikitumika katika filamu kubwa mbalimbali, ambazo zimepata umaarufu duniani.

Udit Narayan alizaliwa Decemba 1, 1955 nchini Nepal. Lakini alipata umaarufu India akiwa kama mmoja wa waimbaji nyuma ya filamu (playback singers) ambao wanatamba katika historia ya Bollywood.

Alianza kuimba mwaka 1980, lakini alipata mafanikio makubwa mwaka 1988 kupitia filamu ya ‘Qayamat Se Qayamat Tak’. Katika filamu hiyo, aliimba wimbo wa ‘Papa Kehte Hain’, ambao ulimtambulisha rasmi kama mmoja wa waimbaji bora wa kizazi hicho.

Mbali na muziki, mchango wake katika filamu za India ni mkubwa kwani kupitia sauti yake amefanikisha kusukuma filamu hasa zile za mapenzi na kuzifanya zitambulike zaidi ikiwemo Kuch Kuch Hota Hai, Dilwale Dulhania Le Jayenge, Raja Hindustani, Lagaan nk.

Hata hivyo kupitia kipaji chake amefanikiwa kunyakuwa tuzo za heshima ikiwa ni pamoja na ‘National Film Awards’ mara tatu na ‘Padma Bhushan’, ambayo ni moja ya tuzo za juu zaidi nchini India.

Sauti ya Udit imewahi kutumika na mastaa zaidi ya 100 katika filamu zao ikiwa ni pamoja na Aamir Khan ‘Qayamat Se Qayamat Tak (1988)’, Shah Rukh Khan ‘Dilwale Dulhania Le Jayenge)’, Salman Khan ‘Hum Aapke Hain Koun’, Akshay Kumar ‘Dastak’, Govinda, Hrithik Roshan, Saif Ali Khan na wengineo.

Pia amefanya kolabo na wasanii wa kike akiwemo Lata Mangeshkar, Alka Yagnik, Kavita Krishnamurthy, Sadhana Sargam, Anuradha Paudwal, nk.

Ili kuendeleza kipaji chake Udit alimwingiza mtoto wake wa kiume Aditya Narayan kwenye tasnia ya muziki unaotumika katika filamu akiwa na miaka 5. Aditya sauti yake ilisikika katika filamu ya Masoom (1996) kupitia wimbo wake wa ‘Chhota Baccha Samajh Ke’.

Aidha dunia ilimtambua kijana huyo wakati alipokuwa na miaka 8 baada ya kuimba na baba yake katika wimbo wa ‘I Love You Daddy’ kupitia filamu ya ‘Akele Hum Akele Tum (1995)’, wimbo ambao ulisaidia filamu hiyo kutambulika zaidi duniani.

Mpaka kufikia sasa, Udit ameimba zaidi ya nyimbo 25,000 katika lugha 36 kama Hindi, Nepali, Bengali, Kannada, Tamil, Telugu, na nyinginezo, huku akifanikiwa kuachia album yake ambayo imejaa Masongi yanayokubalika zaidi.

Mbali na sauti yake ambayo imekuwa ikiwavutia zaidi mashabiki mbalimbali pia ameonekana katika filamu kama Kanoon (1994), Kusume Rumal 2 (2009) na Megha (1996).






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags