Mr Blue kushinda tuzo, amtaja Sugu

Mr Blue kushinda tuzo, amtaja Sugu


Nguli wa muziki wa Bongo Fleva, Mr Blue hatimaye ameshinda tuzo ya kwanza tangu alipoanza kujishughulisha na muziki 2003.

Mkongwe huyo wa Bongo Fleva ameshinda tuzo hiyo ya Entertainmenta Arts Excellence Awards 'EAEA' 2025 kupitia kipengele cha Living Legend of the year.

Akizungumza na Mwananchi, Byser amesema amesema amefurahia kupokea tuzo hiyo kwani baada ya kukosa tuzo kwa muda mrefu ilipelekea akate tamaa.

"Mimi nimefurahi sana kama unavyosema hii ni tuzo yangu ya kwanza ndani ya miaka 22 ya kufanya sanaa. Kiukweli kukosa tuzo mwanzoni nilikata tamaa kwa sababu nilikuwa natoa miziki mizuri tu ambayo inawafikia Watanzania na nimekuwa nikifanya shoo nzuri, lakini sijawahi kupata pongezi zozote za tuzo kwa hiyo ilikuwa inanikatisha tamaa.

"Lakini huwezi amini kukosa tuzo kulinijenga nikawa imara zaidi na kuamini kwamba nina kila sababu ya kuendelea nisikate tamaa. Kwa hiyo nilikuwa nimeshakubali kuendelea na maisha yangu. Miaka imepita na nimepokea tuzo kutoka Kenya, nimefurahi imenipa moyo, imenipa nguvu na imenifundisha kitu," amesema Mr Blue.

Amesema tuzo zilizokuwa zikiandaliwa nchini alikuwa na kila sababu ya kushinda lakini hajui kwanini waandaaji hawakuwahi kumpa tuzo.

"Siwezi kuwazungumzia sababu zao zilizofanya nisipewe tuzo. Lakini nilikuwa na kila sababu ya kupewa tuzo, nilikuwa nakutana na watu wanashangaa kuona sina tuzo, kwa hiyo huenda nilikuwa sifikii vigezo walivyokuwa wanavitaka. Lakini nje ya Tanzania wameona nastahili kupewa,"anasema

Msanii huyo amewashauri waandaaji wa tuzo nchini kutenda haki kwa kuwapatia wasanii wanaostahili kushinda tuzo.

"Sipo hapa kwa ajili ya kumlaumu mtu lakini ninachoweza kusema nawashukuru sana EAEA. Pia wale wanaotoa tuzo Tanzania waweze kutenda haki waangalie watu ambao wanastahili wawape kwa sababu unaweza mkatisha mtu tamaa nakutengeneza wezi na wakabaji kama mtu anastahili apewe tuzo," amesema Byser.

Aidha, ameshukuru mchango wa msanii mkongwe nchini Sugu kwa kumfungulia milango ya tuzo baada ya kumtunuku tuzo ya heshima wakati akipafomu Bongo Fleva Honors usiku wa kuamkia Julai 1, 2023.

"Unajua inategemea unapewa tuzo na nani unaweza kupewa na mwendawazimu lakini mimi Sugu ni moja ya watu ambao nilikuwa nikiwasikiliza na nikitamani kuwa kama yeye. Halafu mtu huyo ndio ananitunukia tuzo, kwangu mimi ni mafanikio makubwa na niliyapokea kwa mikono miwili, inawezekana yeye kufungua mlango mmoja na mingine ikafunguka," amesema Mr Blue.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Masoud Kofii


Latest Post

Latest Tags