
Mbinu Aliyotumia Rayvanny Kuondoka WCB Bila Maneno
Mwanamuziki wa Bongo Fleva nchini Raymond Mwakyusa ‘Rayvanny’ amefichua mbinu aliyotumia kuondoka lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) bila drama yoyote wala maneno huku akimtaja msanii wa Nigeria Wizkid kuwa ndio sababu.
Wakati alipokuwa kwenye mahojiano yake ya hivi karibuni kwenye ‘Afrobeats Podcast’ na Ade Scope, alieleza kuwa uamuzi wa Wizkid kuondoka kwenye lebo yake ya zamani bila kashfa ulimfundisha jambo muhimu na kumsaidia katika safari yake ya kujiondoa Wasafi.
Amefunguka kuwa kabla ya kutaka kujiondoka Wasafi alikutana na Wizkid Zanzibar ambapo nyota huyo wa Nigeria alimshauri sio lazima kuzungumza vibaya juu ya mtu yoyote na kuwa inawezekana kuondoka sehemu kwa Amani ambapo hata ukitaka baadaye unaweza kurudi bila shida.
“Nilijifunza jambo kutoka hapo, na nikajiambia, sawa, si lazima kupigana au kuwa na ugomvi. Unachohitaji ni kuamini kipaji chako. Kuna mtu anaweza kuomba kiasi kikubwa cha pesa, lakini naamini kipaji changu kitarudisha hizo pesa.
Timu yangu na marafiki walikuwa wakiniuliza nitaponea wapi baada ya kulipa pesa zote kwa Diamond, lakini nilikuwa na uhakika kuwa nitaweza kuendelea,” amesema Vanny Boy.
Licha ya kuondoka WCB, Rayvanny alisisitiza kuwa mahusiano yake na Diamond Platnumz bado ni mazuri na hawajawahi kukosana kwa namna yoyote ile tangu aondoke katika lebo hiyo.
“Yeye ni kaka yangu. Tuliongea kwa simu kwa karibu saa moja, na naamini kuwa kwa mawasiliano mazuri na kujiamini, hakuna haja ya kupigana,” ameeleza Rayvanny.
Rayvanny alijiunga na WCB mwaka 2015, akiwa ni msanii wa pili, baada ya miaka sita ya kufanya kazi pamoja, aliachana nao akiwa tayari amefungua lebo yake, iitwayo ‘Next Level Music (NLM)’ ambayo inamsimamia msanii Mac Voice.
Licha ya kuanzisha lebo yake, Rayvanny ameendelea kuwa karibu na WCB na hasa bosi wa lebo hiyo, Diamond na wamewahi kutoa ngoma mbalimbali za pamoja ikiwemo Nitongoze, Salome, Iyena, Mwanza, Tetema, Timua Vumbi, Amaboko na Woza, huku wakiwa wamekutana kwenye ngoma mbili za wasanii wote wa WCB kama Zilipendwa na Quarantine
Leave a Reply