Na Asma Hamis
Tumezoea kuona mashine za kufulia, kuoshea vyombo na hata za kufanyia usafi majumbani lakini kuhusu mashine ya kuogeshea binadamu hili ni geni machoni mwa watu, tunajua unajua lakini wacha tukujuze zaidi kuhusiana na mashine hiyo.
Akiwa darasa la nne Yasuaki Aoyama, kutoka Japan alivutiwa na uzinduzi wa mashine ya kuogeshea binadamu mwaka 1970 japo haikufanikiwa kibiashara kwa mwaka huo kutokana na teknolojia kuwa ndogo, hivyo sasa ameamua kuitimiza ndoto hiyo iliyoshindikana kwa zaidi ya miaka 50.
Aoyama ambaye sasa ni mwenyekiti wa kampuni ya Science Co inayotengeneza vifaa vya chooni (mabomba vya mvua ya kuogea) yupo mbioni kuzindua mashine ya kuogeshea binadamu aliyoipa jina la ‘Mirai Ningen Sentakuki’.
Kwa mujibu wa tovuti ya Techspot mashinde hiyo si tu kutumika kuogeshea binadamu lakini pia itakuwa na kifaa maalumu kwa ajili ya kuchunguza afya ya mtu, kuchunguza hali ya hisia ya mtu kama anafurahia au laa ambapo mchakato huo wa kuogesha unachukua dakika 15 tu.
Aidha Aoyama ameeleza kuwa uzinduzi wa bafu hilo au mashine hiyo utafanyika Osaka makao makuu ya Science Co huku akiwekawazi kuwa watakaotaka kutumia mashine hiyo watatakiwa kufika makao makuu ya kampuni hiyo kwani bado hawajatengeneza nyingi zaidi kwa ajili ya matumizi ya majumbani.
Mashine hiyo imeshafikia asilimia 70 kukamilika ambapo kampuni hiyo imepanga kuwapa nafasi wageni 1,000 kujaribu kuoga huku uzinduzi huo ukipangwa kufanyika Aprili 2025.
Leave a Reply