MAHUSIANO: Wazee wetu walikuwa na sababu ya kuzuia wachumba kukutana kimwili kabla ya ndoa

MAHUSIANO: Wazee Wetu Walikuwa Na Sababu Ya Kuzuia Wachumba Kukutana Kimwili Kabla Ya Ndoa

Ni kweli kwamba, siku hizi vijana wengi huamini kuwa baada ya kukutana kimwili, ndipo wanapoweza kudai kwamba, wamewafahamu wapenzi wao vizuri na kwamba kukutana kimwili ndiyo mapenzi au kupendana kwenyewe. Wanapokutana kimwili na kuvutiwa na tendo la kujamiiana, huamini kabisa kwamba, uhusiano nao utakuwa mzuri. Kwao, tendo la kujamiiana ndiyo kipimo cha uimara wa uhusiano wao.

Baada ya kufanya mapenzi, wapenzi huamini kwamba, sasa wanaweza kujitoa kwenye uhusiano huo na kwamba, wanaweza kuwa na nguvu nao. Suala hili, wataalamu huliita mtego wa kimapenzi. Huitwa hivyo kwa sababu huwafanya wapenzi kutoangalia sifa nyingine na badala yake kuweka nguvu kwenye mwili, yaani tendo la kujamiiana.

Upofu hutokea kutokana na kuzalishwa kwa kemikali nyingi mwilini, zenye kumfanya mtu asiweze kujiuliza kuhusu maeneo mengine ya kimaisha ya binadamu zaidi ya mwili. Kinachotokea ni miili kuvutwa na wale tunaodai tunawapenda kwa kuzalisha homoni inayofahamika kama phenylethylamine au PEA kwa kifupi.

Kemikali au homoni hii pamoja na nyingine kama vile dopamine na norepinephrine (ambazo huchochea hali ya kimwili) na testosterone (ambayo huongeza hamu ya kujamiiana), huzalishwa baada tu ya kukutana kimwili. Baada ya kuzalishwa kwa homoni hizi, akili ya mtu huona mwili tu, yaani mapenzi na siyo sifa nyingine.

Hapa ndipo ambapo, mtu anajikuta hawezi kujizuia kukutana tena kimwili na mpenzi wake, mara baada ya kukutana naye mara moja. Baada ya kufanya mapenzi na kufika kileleni, huzalishwa homoni iitwayo oxytocin (ambayo huhusika na mihemko), homoni hii humfanya mtu kujikuta anapenda kuwa karibu na kujifunganisha na mtu aliyefanya naye mapenzi. Naweza kusema ukaribu kwa wapenzi wawili huongezeka na unakuwa ni ukaribu wa mwili zaidi.

Kuzalishwa kwa homoni hizi, ni jambo ambalo mtu hawezi kulizuia na huwa linakuja kwa nguvu sana, kiasi kwamba, mtu huwa kama amepoteza ufahamu wa maeneo mengine ya kimaisha isipokuwa mapenzi tu. Wale waliowahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi kabla ya ndoa au wale wanaotoka nje ya ndoa zao kwa kuvutwa kimwili na wapenzi wengine wanajua inavyokuwa.

Lakini homoni hizi, hatimaye huanza kupungua na mtu huanza kuhisi kwamba, alikosea. Haoni tena au kuhisi kama ilivyokuwa awali. Sasa haoni kuwa mpenzi wake ni mzuri au anayefaa kama alivyokuwa anaona awali. Kwa sababu, homoni zile zimeshuka sana, mwili unakuwa hauna maana tena. Kwa bahati mbaya kile kilichokuwa kinaitwa upendo kilikuwa kimefungiwa kwenye mwili na homoni hizo ambazo sasa hazipo. Hivyo, wapenzi hawana tena cha kushika ambacho, wataweza kukiita mapenzi.

Naamini sasa unajua ni kwa nini tangu kale kabisa suala la wachumba kukutana kimwili kabla ya ndoa lilikuwa linapingwa sana na wazee wetu. Ni kwamba, watu wanapokutana kimwili , uwezo wa kukaguana tabia unakuwa umefungwa kutokana na kufumuka kwa homoni hizi ambazo hubadili hali ya mtu na hisia zake kwa ujumla.

Hebu jiulize, ni kwa nini mapenzi yanayoanza kwa moto sana huzimika haraka au kwa kishindo sana? Ni kwa sababu yamejengwa juu ya msingi usioaminika, yaani kutokana na mihemko ya kimapenzi! Penzi linalokuwa polepole na lisilotanguliza kukutana kimwili ndilo lenye kushika, kwani halina msingi wa mwili.


Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Shaban Kaluse

A Sales and Marketing in the hospitality Industry and also a freelance journalist, writing about love and relationships and educative articles which aims for youths, every Tuesday on Mwananchi Scoop.


Latest Post