Majaji ambao wanasimamia maamuzi kwenye kesi ya rapa Sean “Diddy” Combs wameripotiwa kufikia uwamuzi kwenye baadhi ya kesi huku kesi ya kufanya uhalifu wa kupanga ikiendelea kutokana na kutokuwa kwa makubaliano baina ya majaji.
Jana Julai 1, 2025, jopo la majaji limepitisha hukumu kuhusu makosa manne kati ya matano yaliyowasilishwa, ambayo ni pamoja na mashtaka ya usafirishaji wa watu kwa ajili ya ngono na unyanyasaji wa kingono. Hata hivyo, bado kuna mvutano mkubwa kuhusu shtaka kuu la kuendesha shirika la kihalifu, maarufu kama racketeering.
Katika hatua hiyo mahakama imeagiza jopo la majaji kurejea tena kujadili kwa kina shtaka hilo moja lililobakia, baada ya kushindwa kufikia kauli moja ambapo leo Julai 2,2025 watakutana kwa ajili ya kuendelea na mchakato wa maamuzi.
Aidha wataalamu mbalimbali wa sheria wanaeleza kuwa, licha ya kutolewa kwa hukumu ya awali katika baadhi ya mashtaka, uamuzi kuhusu shtaka la racketeering ndio utakaobeba hatma nzima ya kesi hiyo ambayo imekuwa ikishika vichwa vya habari vingi duniani kote.
Kwa mujibu wa vyanzo vya karibu na kesi hiyo, Diddy hakupanda kizimbani kujitetea, jambo ambalo linaelezwa kuwa ni mkakati wa kuepuka maswali magumu kuhusu tuhuma hizo nzito.
Kesi hiyo, ambayo imehusisha mashahidi zaidi ya 30 na ushahidi wa video ukimuonesha Diddy akimshambulia aliyekuwa mpenzi wake Cassie Ventura kwenye moja ya hoteli jijini New York.
Diddy anakabiliwa na mashtaka ya usafirishaji wa binadamu kwa ajili ya ngono, njama ya kihalifu, usafirishaji kwa lengo la kushiriki katika ukahaba, kumiliki silaha zisizo na utambulisho na mengineyo.
Sean "Diddy" Combs alikamatwa Septemba 16, 2024 katika hoteli ya Park Hyatt, Manhattan, New York na kupelekwa moja kwa moja katika gereza la Metropolitan huko Brooklyn. Kesi yake ilianza kuzikilizwa Mei 5,2025.
Endapo atapatikana na hatia, anaweza kukabiliwa na kifungo cha muda mrefu jela au cha maisha jambo ambalo litakuwa na athari kubwa si tu kwa maisha yake binafsi bali pia kwa tasnia ya burudani ya Marekani.

Leave a Reply