Mahakama Ya Rufaa Yaridhia R.Kelly Kufungwa Miaka 30

Mahakama Ya Rufaa Yaridhia R.Kelly Kufungwa Miaka 30

Mahakama ya rufaa ya shirikisho nchini Marekani, imeunga mkono hukumu ya R. Kelly ya kifungo cha miaka 30 jela iliyotokana na kesi zilizokuwa zikimkabili za biashara ya usafirishaji wa binadamu na unyanyasaji wa kijinsia.

Mapema jana Jumatano Februari 12, 2025 Mahakama ya Rufaa ya Mzunguko wa 2 mjini Manhattan, NY ilitoa uamuzi baada ya kusikiliza kesi hiyo Machi mwaka jana, iliweka wazi kwamba msanii huyo aliitumia umaarufu wake kwa zaidi ya robo karne kuwatendea unyanyasaji wa kingono wasichana na wanawake vijana.

Utakumbuka mwaka 2021, mshindi huyo wa Grammy na mwandishi wa nyimbo wa R&B aliyeuza nakala nyingi, alihukumiwa katika Mahakama ya shirikisho ya Brooklyn kwa mashitaka kadhaa, ikiwemo utapeli na biashara ya usafirishaji wa ngono.

Mahakama hiyo ya rufaa, iliyoongozwa na majaji 3, ilisema kwamba wanachama wa kundi la R. Kelly walimsaidia kumtambulisha msanii huyo kwa wasichana wadogo ambao alihusika kuwafanyia ukatili wa kijinsia.

“Kwa msaada wa kundi la wasimamizi, wasaidizi, na wafanyakazi wengine kwa zaidi ya miaka 25, Kelly alitumia umaarufu wake kuwavuta wasichana na wanawake vijana katika mkono wake. Ushahidi katika kesi ulionyesha kwamba alijitenga nao kutoka kwa marafiki na familia, kudhibiti kila kipengele cha maisha yao, na kuwatendea unyanyasaji wa kisaikolojia, kimwili, na kingono,” ilieleza mahakama hiyo

Msanii huyo alikata rufaa mwaka jana chini ya wakili wake Jennifer Bonjean, huku rufaa hiyo ikikataliwa kwa mara ya pili mfululizo. Kwa sasa Kelly amezuiliwa katika Gereza la Federal Metropolitan Correctional Center (MCC) huko Chicago, Illinois.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags