Mabantu walivyompitisha Jay Melody kwenye njia zao

Mabantu walivyompitisha Jay Melody kwenye njia zao

 

Ni wazi kumekuwa na makundi mengi ya muziki ambayo yamevunjika, sio tu Tanzania bali hata sehemu nyingine mfano  kundi la P-Square lililokuwa likiundwa na ndugu wawili Peter na Paul Okoye kutokea nchini Nigeria. 

Lakini licha ya kuwepo na upepo huo mbaya, unaonekana kutowagusa wasanii wa kundi la Mabantu Twaah Kane na Muh Kajo kwani hadi sasa wamedumu pamoja kwenye muziki kwa zaidi ya miaka 12.

Umoja wao unaweza kusema ndiyo chachu ya kuwafanya waachie kazi nzuri kila mara. Na hivi karibuni wametoa wimbo mpya ndani wakiwa wamemshirikisha Jay Melody. 

Akizungumza na Mwananchi Scoop, Twaah Kane ambaye ni mshirika wa kundi la Mabantu amesema licha ya Jay kuzoeleka kwenye miondoka ya R&B na Baibuda walifanikiwa kumweka kwenye njia zao za muziki wa kuchangamka bila kuathiri biashara zao.

"Siku zote zinapokutana biashara mbili tofauti lazima kuwe na ugumu. Vitu kama ratiba na kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa kwa pande zote mbili lakini mwisho wa siku ni biashara tuliangalia ni manufaa gani atayapata yeye na faida pia kwa upande wetu. 

“Na bahati nzuri tumefanya naye kazi zaidi ya moja kwa hiyo wimbo huu ni mradi wa kwanza na zingine zitafuata," amesema Twaah. 

Twaah amesema ufanyaji wao wa kazi kwa bidii umekuwa na matokea makubwa mpaka kufikia kupata show za kimataifa, ambapo mwishoni mwa 2024, walifanikiwa kwenda Berlin nchini Ujerumani kwa ajili ya kutumbuiza.

"Kupata show ya Ujerumani kwanza ni riziki lakini pia tunamshukuru Mungu muziki wetu kupenya ulimwenguni. Kwa sababu kupata tu hiyo nafasi ya kutumbuiza kwenye jukwaa kama lile ni muziki wetu kupiga hatua.

 “Huenda muziki wetu usingekuwa unatambulika hivyo tusingepata nafasi kwenda," amesema Twaah.

Ameongezea kuwa kundi lao kuvuka mipaka ya Tanzania lilianza zamani lakini hawakutaka kuweka wazi. 

"Sisi tumeshaanzaga hizo mbanga toka kitambo. Sema tunapiga chini ya maji kwa hiyo unakutana na matukio kama hayo shows za Ujerumani sio kwamba imetokea kama bahati mbaya ni mipango.

 

“Tumekaa maombi kibao yanaandikwa kwa ajili ya sisi kupata nafasi kutumbuiza usije ukaashangaa kesho kusikia Mabantu watatumbuza kwenye majukwaa mengine kwa sababu hatulali tunatuma sana maombi," amesema Twaah. 

Aidha, amesema kuna muda uliwataka wasifanye nyimbo za kushirikiana na wasanii wa muziki wa Hip-hop lakini mipango yao kwa 2025 ni kuachia collabo nyingi zikiwemo za wachanaji. 

"Kuna muda muziki ndio unakupelekesha msanii. Na sio msanii unaupelekesha muziki. Kuna muda muziki unakuhitaji ufanye ladha fulani au ufanye na msanii fulani.

“Hapa katikati muziki wetu ulikuwa tayari umeshajichagulia ladha yake kwa hiyo huenda collabo na rapa zisingefanya vizuri. Lakini tunaelekea pazuri kwa sasa na moja ya malengo ya Mabantu 2025 ni kuachia collabo nyingi ikiwa ni pamoja na za marapa," amesema Twaah.

 

Kundi la Mabantu limedumu kwa muda mrefu likiwa na wanachama wawili pekee, Twaah akiwa  mwakilishi wa kundi hilo, amesema hawafikirii kuongeza msanii mwingine.

 

"2026 tunafungua lebo ya Mabantu. Ni mapema kuongea lakini siyo vitu vya kukurupuka. Tunaona hata kaka zetu ambao wametutangulia namna wanavyopambana kuhakikisha lebo zao zinasimama.

 

 “Kwa hiyo tunatamani hata na sisi tunapokuja kuingia huko kwenye biashara nyingine tuwe tumejidhatiti kweli kweli. Lakini ni ndoto yetu kuwa na lebo kama sio mwaka huu basi hata mwakani," amesema.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Masoud Kofii


Latest Post

Latest Tags