Kwa Udi na Uvumba

Kwa Udi na Uvumba

Innocent Ndayanse

HILDA alibaki kinywa wazi baada ya kuisikia simulizi hiyo ya kutisha. Akamtazama Panja kwa makini na kuigundua hasira iliyojikita moyoni mwake na kutoa taswira halisi usoni pake. Huruma ikamwingia na  kwa mnong’ono akajikuta akisema, “Basi, usijali baby…”

“Hapana, lazima nijali,” Panja alimkata kauli. “Huenda saa hizi tunasakwa na Polisi kama wahaini au magaidi. Na kama ndivyo ilivyo, basi mshenzi yule ana ahueni.”

“Ahueni ki-vipi?”

“Ana pesa,” Panja alisisitiza. “Kwa Tanzania ya leo hakuna kinachoshindikana mbele ya pesa. Kelele za serikali kuhusu eti kupiga vita rushwa na ufisadi ni kelele ambazo hazitofautiani na kumpigia mbuzi gitaa. Unadhani askari gani atakataa milioni moja au mbili kama atakutana na Kipanga na kuonyeshwa kiasi hicho cha pesa? Na kwa Kipanga, milioni moja, mbili ni kitu gani kama tayari ana zaidi ya milioni hamsini? Kwa kifupi, yeye akikamatwa ni rahisi kusevu ngoma, tofauti na mimi ambaye sina mbele wala nyuma. Mimi nikikamatwa nitaozea jela.”

Ukimya mfupi ukatawala. Kisha, kwa unyonge Hilda akauliza, “ Sasa utafanya nini?”

“Nitamsaka!” Panja alitamka kwa msisitizo. “Nakuapia, nitakula nae sahani moja. Na lazima nitampata. Naapa, nitamsaka kwa udi na uvumba mpaka nimpate. Liwalo na liwe. Najua ana ‘cha moto’ na lolote linaweza kutokea nitakapokutana naye. Lakini sijali, ni afadhali aniue kuliko kumwachia hivi-hivi tu atanue na pesa yangu.”

Kilikuwa ni kiapo rasmi toka kinywani mwa Panja, kiapo ambacho hakuwa tayari kukitengua hata kwa mtutu wa bunduki, japo pia hakujua kama atafanikisha azma yake hiyo kabla ya vyombo vya dola havijamtia mbaroni. Lakini ndivyo alivyoamua; ni kwenda mbele daima, kurudi nyuma, mwiko!

KIPANGA hakuwa mjinga. Aliijua hatari ambayo ingemkuta kama angeendelea kuling’ang’ania gari hilo. Hivyo, alichofanya baada ya  kumwacha Panja ni kwenda umbali wa kilometa tatu hivi, kisha akaliegesha pembezoni mwa barabara na kutoka na lile begi lenye pesa.

Hakuendelea kushangaa-shangaa katika eneo hilo, alizunguka nyuma ya nyumba moja kisha akaufuata uchochoro akiwa katika uelekeo uleule wa Dar. Baada ya kutembea umbali mrefu kidogo hatimaye alijitokeza tena barabarani, hiyo ikiwa ni sehemu ambayo kulikuwa na kituo cha mabasi ya abiria.

Kupanda basi la abiria lilikuwa ni jambo ambalo halikumwingia akilini. Alihofia kukutana na mtu ambaye hatakuwa ‘mzuri’ kwake. Angeweza kupanda lori, lakini pia aliona kuwa usafiri wa aina hiyo ungemchelewesha kufika Dar 

‘Acha woga, una silaha, hakuna cha kukubabaisha,’ alihisi sauti ikimwambia. Ujasiri ukamrudia. Akavuka barabara na kupanda basi moja lililotoka mikoa ya Kaskazini mwa nchi. Kitu cha kwanza alichofanya baada ya kupanda ni kuangaza macho kwa kila aliyekuwemo.

Alijivunia  kuwa na uwezo wa kuyasoma macho ya mtu yeyote mwenye harufu ya uaskari, watu ambao hakuwa na fikra za kuja kuwa na uhusiano nao katika maisha yake. Hivyo, macho yake makali yaliyokuwa nyuma ya miwani myeusi yalikuwa na kazi ya kuwatafuta askari ndani ya basi hilo. Dakika mbili za zoezi hilo zilitosha kumpa picha halisi ya abiria wenzake.

Hakukuwa na mtu wa kumtilia shaka. Ndipo akachagua siti ya nyuma kabisa na kutulia. Punde gari likaanza safari. Nusu saa baadaye akateremka Ubungo na kuuvaa uchochoro mmoja baada ya mwingine hadi akaifikia gesti bubu ambayo alikodi chumba na kujifungia kwa minajili ya kuzihesabu zile pesa.

Ni baada ya takriban nusu saa nyingine ndipo alipohitimisha zoezi hilo. Akatabasamu kwa furaha. Alikuwa na sababu ya kuwa katika hali hiyo. Lile begi lilikuwa na shilingi milioni 60! Hazikuwa pesa kidogo kwake! Maishani mwake, tangu aanze kushika pesa na kuitambua thamani yake, hakuwahi kukamata kiwango hicho cha pesa! Hata nusu yake! 

Kwa wiki nzima alijihifadhi katika gesti hiyo, akila kila alichotaka na kunywa kila alichopenda bila ya wasiwasi wowote. Awe na wasiwasi wa nini? Wasiwasi utoke wapi? Aliyafananisha makazi yake hayo na pango lililochimbwa katika mmoja wa milima ya Himalaya, hivyo kumpata ingehitajika teknolojia ya hali ya juu na ujuzi wa kiwango cha juu kwa Jeshi la Polisi, nyenzo ambazo  aliamini kuwa Jeshi la Polisi la Tanzania haliwezi kuwa nazo.

Kwa hali hiyo, hata hisia kuwa huenda ipo siku Panja atamwibukia hapo hazikupata uzito wowote kichwani mwake. Alimhofia Panja kwa kuwa ndiye mwenye uchungu zaidi, siyo Jeshi la Polisi. Na kwa kuwa alimwacha Panja akiwa hoi bin taaban kisaikolojia na kiuchumi, hakuwa na cha kuhofia tena.

Hakutishwa na kauli za Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani na mwenzake wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, kuwa msako mkali dhidi ya majambazi wanaosadikiwa kumuua dereva teksi na Waarabu watatu, unaendelea.

Hakubabaishwa na kauli hiyo!

Huo ndio utaratibu wa Polisi; uchunguzi na msako. Lakini siyo lazima uchunguzi ukatoa matokeo mazuri au msako ukazaa matunda. Akilini mwa Kipanga, msako na uchunguzi wa Polisi ni sehemu ya ajira yao. Kuonekana wakihangaika hapa na pale mitaani, silaha mikononi, wakimhoji mara huyu mara yule, kumtia makofi huyu na kumpiga teke yule huwafanya waonekane wakilipwa mshahara halali.

Na kitafikia kipindi ambacho litazuka tukio jingine, tukio zito zaidi, na hapo ndipo jalada hili litawekwa kando na kuchukuliwa jalada jingine. Huo, huenda ukawa ndio mwisho wa uchunguzi au msako wa tukio la jana. Kazi itaanza upya. Kazi mpya kuhusu tukio la leo.

Imani hiyo ilimfanya Kipanga asiwe na wasiwasi wowote. Ilipita wiki moja, zikakatika wiki mbili, hatimaye mwezi ukaisha akiwa hapohapo gesti akila raha. Hakukuwa na chochote cha kumtia jakamoyo. Pesa anazo, kwa nini asifurahie maisha?

Ni kiburi cha pesa hizo kilichomfanya kila siku abadili mwanamke wa kustarehe naye usiku baada ya kugida bia. Akawa akifanya hivyo huku akihakikisha kuwa mwanamke anayechukuliwa ni yule mwenye sifa za uzuri wa hadharani, mwanamke ambaye macho ya rijali yeyote lazima yamtazame kwa uchu mkubwa.

 

 

 


Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Detricia Pamba

A Digital Journalist, Content Creation Executive at Mwananchi Communications Ltd and Chief Editor of Mwananchi Scoop. I'm also writes stories around Technology, every Wednesday on Mwananchi Scoop. My other famous segments on Mwananchi Scoop include LISTI and WHO’S HOT.


Latest Post