Mwigizaji Joyce Mbaga a.k.a Nicole Berry, alipandishwa kizimbani juzi kati na kusomewa mashtaka ya uhujumu uchumi.
Picha lilianza kwa kikundi cha watu kujitokeza wakidai kuwa walikuwa wakicheza mchezo wa upatu na kijumbe wao alikuwa Nicole. Lakini ilipofika zamu yao ya kupokea pesa wakadai Nicole alianza kuwazungusha.
Mara tukasikia Nicole yuko polisi, mara tukasikia amepandishwa kizimbani, mara tukasikia amepelekwa rumande kwa kushindwa kulipa dhamana ya kama Sh46 milioni hivi.
Kama kawaida, kwenye mitandao ya kijamii “chama cha waandika komenti” kilianza kumshambulia Nicole. Watu walihoji ameshindwaje kulipa milioni 46 wakati anasemaga anatembea na milioni tatu kwenye pochi kwa siku na huzimaliza. Wengine wakauliza imekuwaje ashindwe kulipa dhamana wakati anadai kumiliki nyumba ya bilioni?
Na hii si mara ya kwanza kuona komenti za aina hii. Mara nyingi wasanii wanapopatwa na matatizo ikiwamo maradhi huomba michango kwa mashabiki. Lakini mashabiki wamekuwa wakiwashambulia kwa sababu ya anasa wanazoonyesha mitandaoni. Leo msanii anatangaza kujizawadia gari la mamilioni, kesho anaomba msaada wa matibabu.
Kadri ninavyozisoma hizi komenti nagundua kuwa Watanzania wengi hawaelewi biashara ya burudani. Pengine leo niwape darasa japo kwa ufupi kwa sababu ni darasa pana.
Sikieni washkaji; biashara ya burudani ni ya kujiongeza thamani. Msanii anatakiwa kuhakikisha kuwa wateja wake hawamchukulii poa ili wanapomletea madili yawe madili ya maana. Na ninaposema “wateja” simaanishi mashabiki, bali kampuni na taasisi zinazowapa wasanii mikataba ya ubalozi, shoo na matangazo.
Wasanii walishaacha kupata pesa moja kwa moja kutoka kwa mashabiki. Marioo hatarajii wewe utazame video zake YouTube ili apate pesa moja kwa moja kutoka kwako. Hapana! Yeye anategemea wewe ‘usabusikiraibu’ chaneli yake ili aongeze idadi ya wafuasi. Idadi kubwa ya wafuasi ni moja ya sababu za msingi zinazovutia kampuni na taasisi kufanya kazi na msanii husika.
Hizi drama za wasanii kununua magari ya milioni 100, kuposti mijengo mikali, kuvaa vizuri na kuonyesha maisha ya kifahari sio kwa sababu wanakula bata tu. Hapo ndo wapo kazini, wakijijengea ‘brandi’ ili mtu anayekuja kufanya nao kazi ajue anazungumza na mtu wa hadhi kubwa.
Kuna kipindi nilikuwa napiga stori na msanii mmoja akanambia: “Kagambo, mimi nikienda kuongea dili la pesa na kampuni au taasisi niko radhi nikodi Range Rover kuliko kuingia pale na IST. Ukiingia na gari nzuri, umependeza watu wanakuheshimu na wanakulipa pesa ndefu. Ukienda kinyonge watadili na wewe kinyonge hivyo hivyo.”
Siku moja, Diamond Platnumz alikuwa anazungumza kwenye mkutano na mamlaka za usimamizi wa kazi za sanaa Tanzania. Alisema kitu kama hiki: “Jamani, sisi wasanii hatuna pesa yoyote. Hawa mabodigadi kumi kumi tunaotembea nao wasiwadanganye. Kwanza wala siyo mabodigadi ni marafiki zetu wenye miili mikubwa. Tumewakusanya, tumepeana majukumu ili tupate kidogo tugawane maisha yaende.” Na huo ndio ukweli.
Kwa hiyo, next time ukiona Nicole mwingine anajiita Boss Lady na kuposti amenunua gari la milioni 300 wala usianze kumshambulia. Kuna uwezekano mkubwa hilo gari hajanunua — kakodi tu, kapiga nalo picha. Hizo anasa mnazoona wanazifanya sio kwamba wanakula bata, hapana. Hapo ndio wapo kazini, washkaji!

Leave a Reply