Kifahamu kitambaa aina ya Durag

Kifahamu kitambaa aina ya Durag

Na Glorian Sulle


Ni kweli suala la mitindo na fasheni ni marudio ya vile vilivyopita , katika kutafuta mitindo mipya  kuna wale wanaogeuza matumizi ya mavazi au mitindo hadi kupelekea ipoteza mvuto machoni pa wengi.

Ngoja nikupe historia fupi ya vazi aina ya “Durag” Kitambaa hiki kilikuwa na kazi maalumu ya kutambulisha watumwa kwa kulivaa kichwani nchini Ethiopia na nchi nyinginezo zilizoathiriwa na utumwa mwanzoni mwa karne ya 19.

Vazi hili lilijizolea umaarufu zaidi miaka ya 1966 baada ya kuchapishwa na jarida maarufu la Akron Beacon nchini Marekani. Jarida hilo lilitafsiri neno “ Do Rag” kama kitambaa kinachovaliwa katika paji la uso na kufunga nyuma kwenye kisogo.

Baada ya jarida la Akron Becon kuchapisha taarifa kuhusu kitambaa hicho , baadhi ya kampuni kama “So many waves” ya nchini Marekani ilitengeneza aina mpya ya vitambaa hivyo na hatimaye kukuza mauzo ya kampuni hiyo baada ya kugeuza matumizi ya vitambaa hivyo.

Kitambaa hiko kilitengezwa na kupewa matumizi mapya ya kutengeneza mawimbi ya nywele kwa wale wanaonyoa minyoo ya chini (low cut”) hasa kwa wanaume wenye asili ya Afrika.

Baada ya kugeuzwa matumizi kutoka kuwa vazi la kitumwa na kuwa vazi la shughuli maalumu, kampuni hiyo ililipa jina la "Tie-down." likiwa na maana ya “funga chini”.

Baada ya kutambulika katika tasnia ya mavazi kwa shughuli maalumu “durag” kitambaa hiki kiliendelea kufanya kazi kikamilifu hadi miaka ya 1990 kilipoanza kuvaliwa na wanamziki maarufu nchini marekani.

Wanamziki wa Hip hop kama Jay-Z, Nelly, 50 Cent na Snoop Dogg waligeuza kitambaa hiki na kukipeleka katika tasnia ya mitindo nchini humo na hatimaye duniani hasa kwa jinsia ya kiume tu.

Mpaka hivi sasa nchi nyingi mtindo huu unatambulika kuvaliwa na baadhi ya wanaume tu, na si wanawake  hali hii imekuwa tofauti kwa hapa nchini Tanzania.

Aidha, mtaalamu wa mitindo Ritha Peter anaelezea ni ipi dhambi ya mitindo katika kitambaa hiki maarufu chenye kila aina ya rangi.

“Kitambaa hiki kina kazi maalumu ya kutengeneza mawimbi kichwani hasa kwa wanaume wanaonyoa minyoo ya chini (low cut)” amesema.

Amefafanua kuwa kitambaa hiki kimekuwa kikivaliwa hata na jinsia za kike hapa nchini na kuleta tafsiri tofauti ambayo siyo nzuri kwa mtoto wa kike.

“Wengi wanaovaa hivi vitambaa hutafsiriwa kama wanawake au mabinti ambao hawajatulia au waswahili na pengine huonekana hawajiheshimu,”amesema

Tafsiri hizi ni kutokana na vitambaa hivi kuvaliwa na wanaume katika nchi za wenzetu na hasa wale wanaoimba Hip hop au wale wenye minyoo ya nywele ambayo inafaa kutengeneza mawimbi.

“Anapovaa mwanamke inaleta mshituko kwa namna moja au nyingine na kutengeneza maswali yasiyo na majibu,”amesema

Mara nyingi vitambaa hivi hutumika saluni za kunyoa na huvaliwa wakati wa kuweka mawimbi kwenye nywele na si muhimu kutembea umevivaa hasa kwa mtoto wa kike, ukitafiti sana utagundua hata wanaume hawavivai tena.

Kwa ushauri wa kimitindo na fasheni tuache vitambaa hivi vitumike saluni kwa shughuli yake maalumu ila tusivivae na kutembea navyo barabarani hasa kwa watoto wa kike maana idadi ni mkubwa ya wanaovivaa.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags