Kale ka kijana kakaja mikono mitupu…!

Kale ka kijana kakaja mikono mitupu…!

Ndio nilikuwa nimetia timu jijini Dar kwa mara ya pili mnamo mwaka 1990 baada ya mara kwanza kuja na kuchafua hali ya hewa nikiwa kwa kaka yangu na kupigwa patresheni kijijini. 

Safari hii nilifikia kwa mjomba angu ili kuona kama mjomba ataweza kunisaidia kuendelea na masomo ya kidato cha sita. Basi, nikawa nakaa kwa mjomba maeneo ya Temeke kata ya 14 nikiwa sina shughuli maalum ya kufanya. 

Hapo jirani na kwa mjomba kulikuwa na mzee mmoja Mshihiri  mwenye duka.

Mzee huyo alikuwa na mtoto wa kiume aliyekuwa na umri wa miaka 12 wakati huo, ambaye alikuwa anasoma darasa la tano. Huyu mtoto alinizoea sana na mwisho akaniomba niwe namfundisha. Lakini fundishwa yake ilikuwa ya ajabu, kwani alichokuwa anataka ni kufanyiwa homework  wanazopewa shuleni basi. 

Kila nikimfanyia  homework akawa ananipa kitu kidogo kama shilingi 200 au 300. Nikawa mzee nimepata kibarua. 

Nikiona imepita wiki hajaleta homework namuuliza kulikoni, kama walimu wana malaria au vipi. Iliendelea hivyo mwisho nikawa namwambia anipe hela hata kama simfanyii homework.

Nilimwambia kwamba nasubiri kwenda Chuo Kikuu na kumwahidi kwamba, nikimaliza Chuo Kikuu nitakuwa Mbunge wa Temeke na kwa sababu yeye atakuwa mkubwa wakati huo, nilimwambia nitampa ukuu wa wilaya. 

Kwa sababu ya utoto na somo la Siasa wakati ule kabla ya kubadilishwa jina halikuwa likipanda alikubali. Akaanza kuiba fedha nyingi dukani kwao na kuniletea. Dhambi eh wakati mwingine...! 

Nikiwa hapo Temeke nikaanza uhusiano na binti mmoja Kindengereko aliyeumbwa akaumbika na kalio lililomkaa maridhawa. 

Kwa kuwa nilihisi kutokuwa na viwango vya kumpata nikamghilibu kwamba nasubiri kwenda Chuo Kikuu na kwamba, mambo yangu ni mazuri, vijihela vya chipsi kuku havinisumbui. 

Huyu binti aliniamini na kunikubali nikawa najivinjari naye na kufaidi joto lake la Kindengereko kwa sababu wakati huo pia yule bwana mdogo wa Kishihiri  homework zilikuwa zimeongezeka na mshiko nao ukawa umeongezeka. 

Siku moja yule binti alinifuata Gheto akaniambia ana hamu sana ya chipsi na bia. 

Mzee mzima nilikuwa na kama shilingi mia tu mfukoni. Ilibidi nimwambie yule binti asubiri.

Nilikwenda hapo dukani kwao dogo na bahati nzuri nilimkuta.

Nilimpiga signo na kumwita kando. Nilimwambia nina shida ya kufa na kupona, anitafutie shilingi 1,000. Dogo aliahidi kwamba, baada ya dakika ishirini angeniwezesha.

Aliniambia baba yake akienda kuswali Insha tu, atashughulikia chapchap shida ya mwalimu wake wa tuisheni ya  homework, yaani mimi. 

Nilimwambia naenda kumsubiri kwenye Bar ambayo anaijua, kwani tulikuwa tukienda hapo mara kadhaa kunywa soda. 

Nilimuuliza kama ana uhakika atapata, akasema niondoe hofu kabisa, ni lazima apate, basi nilimpitia demu wangu tukaenda pale Bar. Nilipofika pale Bar niliagiza bia kwa ‘mtoto’ na chipsi. 

Kwa sababu wahudumu walikuwa kidogo wananijua hawakunidai kabla. Tukawa tunapiga stori na ‘mtoto’ huku akijinoma chipsi, kuku na bia. ‘Mtoto’ akamaliza msosi na bia, ikaagizwa bia ya pili, dogo hatokei.

Wasiwasi ukanishika, niliona ni vyema nifuatilie. Ile nasimama, nikamwona dogo akiwa na baba yake na kaka yake fulani mnoko sana na Polisi aliyevaa sare. 

Nilihisi kama vile sipumui na sina mwili. Kabla sijapata muda wa kujiuliza, nilimsikia dogo akisema, ‘ni huyu hapa, huwa nampa kila siku.’ Nilijua kila kitu kimekwenda ndivyo sivyo. Dogo alikuwa menaswa kwenye jaribio lake la kunasua ile elfu. Pale nilikuwa mtuhumiwa namba moja wa kumghilibu mtoto kujipatia mali, halafu hapo mezani chipsi, kuku na bia mbili zinahitaji kulipiwa. ‘Afande mchukue bwana, tapeli mkubwa.’ Yule kaka yake dogo alisema.

 ‘Bwana uko chini ya ulinzi kwa tuhuma za kumtuma mtoto kufanya uhalifu wa wizi dukani. Naomba tufuatane kwenda kituoni.’ Alisema yule Polisi.

Wahudumu wa Bar nao walikuwa wamefika wakitaka kulipwa chapaa zao. Nilimtazama yule demu wangu ambaye siku zote huwa anakunywa na kula chipsi kuku bila kujua kwamba, ni Juhudi za mfadhili dogo.

‘Tunamdai afande, tunaomba atulipe kwanza.’ Mhudumu mmoja alisema.

 

Nilijiuliza ni wakati gani radi huwa zinapiga bila mawingu ya mvua. Ni kwa nini isiwe wakati kama ule? 

‘Lipa bwana twende zetu.’ Afande alifoka. Nilijifanya kupekua mifukoni na kusema, ‘nimezisahau nyumbani.’ 

Baba yake  dogo alisema,  ‘hujasahau chochote, ulikuwa ukisubiri kuletewa, ule na hawara yako. Mimi niwatafutie, nyie mbugie, tena bia! Hapana hiyo haikubaliki.’

Najua mnatamani kujua kilichotokea baadaye. 

Kwa taarifa yenu sikupelekwa Keko wala Ukonga, mambo yaliisha kimya kimya. Na kijijini sikurudishwa, nilipelekwa shule na baadae chuo.

 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Mzee Mtambuzi

A freelance Journalist and also teaching self-empowerment, positive thinking as a means of creating the life you desire including spirituality. He is writing in Mwananchi Scoop every Wednesday Visa na Mikasa.


Latest Post

Latest Tags