Fahamu njia nne za kuishi na watu

Fahamu njia nne za kuishi na watu

Ni wasaa mwingine tena mzuri aliyoupanga mwenyezi Mungu kutukutanisha pamoja katika dondoo hii ya karia ili tuweze kujifunza mambo mbalimbali.

Hii ni fursa nyingine ambayo unapata kuisikia sauti yangu ikiongea na wewe kupitia maandishi haya. Ni matumaini yangu unaendelea vizuri na masomo yako hapo chuoni na kujifunza kila siku.

Basi leo katika karia tutaangazia njia nne za kuishi na watu vizuri. Ni ukweli usiofichika kwamba kila mtu anahitaji watu. Huwezi kuishi bila watu.

Kuna wakati unakutana na mtu haelewani na mwenzie hapo chuoni na kujiuliza tatizo ni nini, ni ule msemo kwamba ana damu ya kunguni au lah! Ukweli ni kwamba kuna tabia huwa zinatatiza mahusiano baina ya watu.

Baadhi ya tabia hizo nimejaribu kuzieleza hapa chini. Twende sasa

  1. Usiwe mwepesi wa kukosoa, kulalamika au kulaumu

Utakubaliana na mimi kuwa hakuna binadamu aliyekamilika na kila  mtu ana udhaifu wake. Kwa kujua hilo hata wewe mkosoaji una mapungufu na madhaifu yako pengine makubwa kuliko yeye.

Usijaribu kutoa kibanzi kwenye jicho la mwenzako na wakati huo kwako kuna boriti. Usiwe wa kwanza kurusha jiwe kwa mwenzako kwa sababu tu makosa yake yamewekwa hadharani ili hali ya kwako yakipata nafasi ya kujulikana utatamani ardhi ipasuke uingie.

Pia usiwe mtu wa kulalamika na kulaumu kwa kila kila kitu hata ambayo wewe ndiye msababishi. Usiwe mtu wa kukashifu na kutoa maneno ya ovyo.

Beba msalaba wako mwenyewe na uupeleke Goligotha, acha kuhukumu, kukosoa na hata kulaumu wengine. Amini usiamini hakuna mtu anayependa mtu mwenye tabia hizo na mara nyingi watu wa hiyo huogopwa na kukwepwa kama ukoma.

Kama mtu kakosea tafuta namna ya kumwambia makosa yake naye kama ni muungwana atakuelewa.

  1. Toa pongezi za dhati

Kila mtu huhitaji pongezi pale anapofanya kazi nzuri. Kumbuka ninaposema pongezi za dhati namaanisha zile pongezi ambazo kweli zinatoka moyoni mwa mtu na si zile za kumvisha mtu sifa zisizofaa ambazo waswahili wana msemo wao wa ‘’Kuvika kilemba cha ukoka’’ au ‘’kupaka mafuta kwa mgongo wa chupa.

Pongezi za kinafiki hazisaidii ila kama umedhamiria kutoa pongezi zitoe moyoni hata kama huyo mtu humkubali lakini jaribu kuikubali kazi yake.

Kwa jinsi hii utaweza kukaa na kila mtu na kuishi vizuri na watu na hata kupunguza idadi ya maadui na kuongeza marafiki.

  1. Toa msaada kwa watu wengine

Kila mtu duniani ni msafiri na katika safari yake anategemea kufika kituoni siku moja. Kwa kuwa njiani kuna dhoruba nyingi huhitaji msaada wa watu wengine. Kama wewe ndiye uliyefikwa na wajibu huo usisite kutoa msaada.

Mtu anayesaidia wengine huwa na mahusiano mazuri na watu na hata yeye kusaidiwa pale anapopata majanga. Kumbuka msaada mzuri ni ule unaoutoa bila kutegemea malipo yoyote, na kama unataka kusaidia basi msaidie yule ambaye unajua hana uwezo wala jinsi ya kukulipa.

Hii itakupa faraja na utajenga jina lako na wasifu wako kwa watu. Neno msaada lina maana pana sana, linaanzia katika vitu mpaka hali. Kuanzia hela, ushauri, kufundisha, kuelimisha na mambo yanayofanana na hayo.

  1. Toa faraja kwa watu

Kuwa mtu mwenye kufariji na kutia moyo wengine. Usiwe mtu mwenye kukatisha tamaa watu wengine.  Usiwe mtu wa kuumiza mioyo ya watu wengine, usiwe mtu wa kunyooshewa vidole kila kona kwamba una hasara nyingi kuliko faida.

Kuna msemo unasema kama huwezi kuwapa faraja kwa watu basi usiwaumize. Kama mtu amekuambia jambo na unaona huwezi kumshauri au kumpa faraja yoyote ni bora umpe pole na ujiondokee zako na si kumuumiza kwa kumwambia maneno yenye kujeruhi.

Kumbuka kuwa ukisha sema neno halirudi tena kinywani, hivyo basi fikiria kwanza kabla ya kuongea na pia jaribu kuvaa uhusika wa unayemwambia.


Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post