Christian Bella alia na machafuko Afrika

Christian Bella alia na machafuko Afrika

Zanzibar. Mwanamuziki mwenye asili ya Congo, Christian Bella, leo Februari 16,2025, amesema viongozi wa Afrika wanatakiwa kushikamana ili kulinda amani.

Bella ameyasema hayo wakati akizungumza na Mwananchi kisiwani Unguja ambako linafanyika tamasha la Sauti za Busara 2025.

"Machafuko ni mengi, nafikiri nchi zote za Afrika zinatakiwa kushikana ili kuepuka matatizo ambayo nchi nyingine inakumbana nazo. Ili kulinda amani Afrika na sisi kama wasanii inatakiwa kufikisha ujumbe kwa njia ya muziki wetu.Viongozi nao wanatakiwa kuwa na sauti moja,"amesema Bella

Kauli ya msanii huyo inakuja ikiwa kuna muendelezo wa machafuko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Kwani baada ya M23 kuteka makao makuu ya Jimbo la Kivu Kaskazini (Goma). Februari 14,2025 waliteka mji wa pili kwa ukubwa katika eneo hilo (Bukavu). Ambao pia ni makao makuu ya Jimbo la Kivu Kusini.

Hata hivyo maneno hayo ya Bella yanaenda sambamba na kaulimbiu ya Sauti za Busara 2025, inayotaka watu kupaza sauti kwa ajili ya kudai amani duniani.

Utakumbuka Februari 14,2025, wakati Mtendaji Mkuu wa tamasha hilo Journey Ramadhan akifanya ufunguzi alisema majadiliano ya amani yanahitajika ili kuepusha migogoro inayoendelea

"Nina ujumbe mdogo kuhusu kwanini tuliamua kuchagua kauli mbiu hii kwa mwaka huu. Katika dunia ambayo migogoro inatisha. Kila mmoja wetu ana nguvu ya kuwa sauti ya amani.

"Hii si tu kuhusu kupinga ukosefu wa haki. Pia ni kuhusu kuhamasisha majadiliano, kuunda nafasi ya kuelewana na kujenga uhusiano kati ya watu wa aina mbalimbali. Amani ya kweli inaanza tunapozungumza kwa huruma na kusikiliza kwa hisia, tukithamini hadithi na mtazamo wa kila mtu," alisema na kuongezea kupitia muziki ni rahisi kupaza sauti kupitia jumbe zinazotolewa.

"Tumeshuhudia migogoro mingi Afrika, kama ninavyosema. Tuache muziki uzungumze kwa sababu sauti za amani zinanza leo hadi tarehe 16 Februari,"alisema

Aidha mbali na hayo Bella ambaye kwa sasa anatimiza miaka 20 kwenye gemu ya muziki, amesema siri ya mafanikio yake ni kutoa kazi zinazogusa kila hadhira.

"Siyo rahisi jina kutosahaulika, lakini nimeweza kufaya ngoma ambazo zinapendwa na watu. Ukiangalia shoo yangu ya Sauti za Busara sijaimba ngoma zote. Zipo za kizazi cha zamani, kizazi kipya hiyo inafanya niteke vijana, wakubwa. Kufanya kwangu ngoma nzuri inanibeba,"amesema Bella






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags