Wanamuziki wa nyimbo za injili nchini Alex Msama na Smart Boy leo Julai 3,2025 wameshinda tuzo ya EAGMA 'East Africa Gospel Music Awards'.
Katika tuzo hizo zilizotolewa na Magreth Chacha ambaye ni Mkurugenzi na Muasisi wa East Africa Gospel Music Awards, Alex Msama amenyakua tuzo ya umahiri katika muziki huo 'Sterling Award For Excellence in East Africa' huku Smart Boy akinyakua katika kipengele cha Wimbo wa Injili Bora wa Mwaka wa Singeli kupitia wimbo wake uitwao 'Singeli ya Yesu'.
Tuzo hizo mbili zimetolewa ikiwa ni mwendelezo wa zile zilizotolewa Juni 28, 2025, Superdome, Masaki, Dar es Salaam. Akizungumza na waandishi wa habari muasisi wa tuzo hizo Magreth amesema,
"Wakati tunatoa zile tuzo na mafanikio yote tuliyopata lakini kulikuwa na mapungufu ya hapa na pale tunaomba mtuwie radhi. Kwa namna hiyo basi katika hilo tatizo la kiufundi kuna tuzo mbili ambazo hazikutolewa kutokana na changamoto ya muda. Kwa siku ya leo naomba nizitangaze rasmi, katika Sterling Award For Excellence in East Africa mshindi ni Alex Msama wa Tanzania.
"Tuzo nyingine ya singeli. Kwa mara ya kwanza gospel singeli imechukuliwa kwa ukubwa sana kwa sababu tunajua wanakonekti na vijana wengi ambao tunajua wanataka kumfuata Yesu. Kwa hiyo tunawaheshimu sana, na tunajua kazi zao ni kubwa tukienda kwenye makanisa yetu watu wanacheza mpaka chini kwa hiyo Best Singeli of The Year in East Africa mshindi ni Smart Boy,"amesema Magreth
Mbali na hayo amesema kwa sasa wanaanza upya safari ya kuanda East Africa Gospel Music Awards 2025-2026 ambazo zitatolewa Agosti, 2026.
"Kwa sasa ifahamike kuwa Agosti 2026, EAGMA itakuwa inatoa tena tuzo. Tunajua kama binadamu sisi hatujakamilika katika hii safari yote tulikuwa na mazuri na mapungufu tunamtukuza Mungu nchi zimefurahi kwa sababu wanasema mwenye haki akitawala nchi inafurahi kwa hiyo haki siku hiyo ya tuzo ilitawala tunamtukuza Mungu kwa ajili ya hiyo furaha,"amesema

Leave a Reply