Washiriki Miss Tanzania, Wataka Uwakala Wa Vipodozi

Washiriki Miss Tanzania, Wataka Uwakala Wa Vipodozi

Washiriki wa mashindano ya Miss Tanzania wameihimiza Serikali kuimarisha zaidi mazingira ya uwakala wa bidhaa za kimataifa za vipodozi ili kupunguza changamoto ya mianya ya bidhaa bandia.

Akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa tawi jipya la CAICA Pharmacy, Mikocheni, Januari 3, 2025 mshindi wa pili wa Miss Tanzania 2023/24, Amina Jigge, amesema wajasiriamali wana nafasi kubwa ya kuboresha sekta ya vipodozi hapa nchini.

“Wajasiriamali wetu wana uwezo wa kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya urembo, lakini wanakabiliwa na changamoto nyingi. Serikali ikirahisisha taratibu za uwakala wa bidhaa, tutaweza kupunguza uingizwaji wa bidhaa bandia na kuwasaidia wateja kupata bidhaa bora na salama,” amesema Amina.

Kwa upande wake Miss Grand Tanzania 2024, Fatma Suleiman, amesema bidhaa bandia zimekuwa chanzo cha madhara kwa watumiaji, akisisitiza umuhimu wa mawakala wa kuaminika kama CAICA Pharmacy.

“Bidhaa bandia zinaleta madhara kwa watumiaji. Tunashukuru CAICA kwa kuhakikisha wanaleta bidhaa moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji. Serikali inapaswa kuwasaidia wafanyabiashara kama hawa ili kuhakikisha bidhaa halisi zinapatikana,” amesema Fatma.

Akizungumza na waandishi, Mkurugenzi wa CAICA Pharmacy, Jackson John, amesema kampuni yake inalenga kuwa mfano wa kuigwa katika sekta ya vipodozi kwa kuhakikisha bidhaa bandia zinadhibitiwa.

“Mbali na huduma za maduka ya dawa, sisi pia ni mawakala wa bidhaa za vipodozi za kimataifa. Tunataka kuhakikisha bidhaa bandia zinatokomezwa kwa kuweka uwakilishi bora wa bidhaa halisi nchini,” amesema.

John aliongeza kuwa makampuni makubwa ya kimataifa yanategemea uwepo wa mawakala wa kuaminika ili kuingiza bidhaa zao katika soko jipya, na ukosefu wa mawakala nchini ni moja ya sababu zinazokwamisha ujio wa bidhaa hizo.

“Hizi kampuni zinahitaji mawakala wa uhakika. Tunataka Tanzania iwe na mawakala wengi zaidi ili kuvutia bidhaa hizi kubwa kuja nchini,” amesema John.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na wadau wa sekta ya vipodozi na urembo, ambao walipongeza juhudi za CAICA Pharmacy, wakisema hatua hiyo ni mwanzo mzuri wa kupunguza changamoto za bidhaa bandia na kukuza sekta ya urembo nchini.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags