Agosti 10 mwaka huu, msanii wa Bongo Fleva,Rayvanny aliandika historia katika muziki na kuitetemesha dunia na wimbo wake wa 'Ooh Mama Tetema'. Wimbo huu ni marudio wa wimbo Tetema alioutoa miaka sita iliyopita na kufanya vizuri.
Wimbo huu alianza kwa kumshirikisha Diamond Platnumz na ukatesa siyo Tanzania tu, bali Afrika na duniani, kabla ya kuwashirikisha baadhi ya wasanii ikiwamo Patoranking na Zlatan na hadi sasa una zaidi ya watazamaji milioni saba na mwaka 2021 akafanya remix nyingine na Maluma raia wa Colombia, ukafanya vizuri na kupata zaidi ya watazamaji milioni 56.
Sasa ameishika tena dunia kwa wimbo huo huo aliourudia mara ya tatu akiwa na wasanii kutoka India, Nora Fatehi na Shreya Ghoshal. Wimbo huu ulishika nafasi ya kwanza duniani kwa video iliyotazamwa zaidi ndani ya saa 24.
Tetema mendelea kuonyesha maajabu na kunka kimataifa baada ya Rayvanny kutumbuiza katika tuzo za MTV Europe Music Awards (MTV EMAs) mwaka 2021, alipopanda katika jukwaa hilo akiwa na Maluma.
Mwaka huo pia akaandika rekodi ya kuwa msanii wa kwanza Tanzania kushika namba moja kwenye chati za Billboard Mexico Airplay kupitia wimbo Mama Tetema (2021), ikiwa ni mara ya pili kuingia chati hizo baada ya hapo awali kutamba Billboard Top Triller Global Chart akiwa na DJ Cuppy wa Nigeria.
Hapa Mwananchi imekuchambulia sababu nne zilizofanya ngoma hiyo kuvunja rekodi ya dunia.
1. Kutazamwa sana
Kwa mujibu wa YouTube na takwimu za muziki wa kimataifa, video hiyo ilikusanya watazamaji 7,402,890 ndani ya saa 24, ikizipita nyimbo kutoka kwa mastaa wa dunia kama Bruno Mars & ROSÉ, Yo Yo Honey Singh na Ed Sheeran.
Hii ni mara ya kwanza kwa msanii wa Tanzania kushika namba moja kwenye orodha ya Most Viewed Videos ndani ya muda huo duniani kote.
Rekodi hii haijapangwa kulingana na bara au nchi, bali kimataifa. Hii inamaanisha video ya Rayvanny ndiyo iliyotazamwa zaidi duniani katika muda huo, mbele ya wasanii wanaosikilizwa zaidi duniani.
2. Ushirikiano kimataifa
Wimbo wa 'Ooh Mama Tetema' umeshirikisha wasanii kutoka Afrika na Asia, kwa Nora Fatehi ambaye ni muigizaji na dansa maarufu India na msanii Shreya Ghoshal ambaye ni miongoni mwa waimbaji bora wa Bollywood.
Ushirikiano huu umeifanya ngoma hiyo kufanya vizuri sio tu Bara la Afrika, lakini duniani.
Ushirikiano na msanii Maluma (Colombia) kwenye wimbo huo mwaka 2021 ulimfanya kuandika rekodi ya kuwa msanii wa kwanza kutoka Afrika kutumbuiza katika tuzo za MTV Europe Music Awards (MTV EMAs).
Kwa mantiki hiyo, ngoma ya Tetema ambayo ilitoka rasmi mwaka 2019, imekuwa na bahati ya kushirikishwa na inaweza kuwa ngoma ya nyota huyo iliyofanya vizuri zaidi na kumfungulia milango zaidi kimataifa.
3. Soko la India
India ni miongoni mwa masoko makubwa ya muziki duniani.
Kupata nafasi ya ngoma ya msanii wa nje kwenye chati za views nchini humo ni mafanikio makubwa kutokana na ushindani wake unaohusisha mamilioni ya mashabiki wa ndani na wale diaspora.
Ngoma hiyo ambayo kwa mujibu wa Rayvanny ni kuwa wasanii hao kutoka India waliomba kolabo naye, hivyo ikawekwa kwenye akaunti ya mauzo ya T-Series ambayo ina zaidi ya wafuatiliaji milioni 300.
Iko hivi, kampuni hizo hutazama zaidi fursa ya ngoma inayofanya vizuri ambayo hata wakiisambaza inaweza kuwaingiza mkwanja mrefu. Mfano, ngoma ya Yimmy Yimmy ya msanii kutoka Ufaransa, Tayc, ilisambazwa na kampuni ya Play DMF nchini humo ndani ya mwaka, ikaingiza watazamaji milioni 257.
Kuwekwa kwenye kampuni hiyo kumeongeza thamani zaidi na kutazamwa zaidi kutokana na ukubwa wa kampuni hiyo kwenye mauzo ya muziki.
Sababu nyingine inaweza kuwa hadhira kubwa ya India. Kwa mujibu wa takwimu, nchi hiyo ina zaidi ya watu bilioni 1.4 na zaidi ya 65% wako chini ya umri wa miaka 35. Hii inamaanisha kuna vijana wengi wanaotumia muziki kila siku.
Muziki wa India uko tofauti na nchi nyingine kwani hufanywa zaidi kama muziki wa filamu, ukisambazwa kupitia Bollywood na asilimia 80 hutokana na filamu; nyimbo huingizwa kama sehemu ya hadithi na kisha kuuzwa kama video na nyimbo pekee.
Waimbaji wanaorekodi wimbo ni mastaa wenye hadhira kubwa kuliko baadhi ya waigizaji. Mfano, kwenye ngoma hiyo Nora hakuimba pekee bali aliigiza sauti ya Shreya ambaye ni mkali wa sauti.
Hii inatokana na ukubwa wa Nora kwenye mitandao ya kijamii na Bollywood, hivyo alitumika kama mchezaji na mrembo aliyeigizia ili kuongeza watazamaji zaidi.
4. Kuvunja rekodi Bongo Fleva
Kwa miaka mingi Bongo Fleva umekuwa ukiuzika zaidi kwenye soko la Afrika Mashariki na Kati na mafanikio yake makubwa mara nyingi yamekuwa Afrika.
Nyimbo zimepenya kwenye chati za Afrika Kusini, Nigeria, Kenya, Uganda na Congo, lakini kuvuka mipaka ya bara hilo na kuingia kushindana na Ulaya kama ilivyo kwa Nigeria na Afrika Kusini imekuwa kwa nadra sana.
Ngoma hiyo inaonekana kubadilisha upepo. Huu si wimbo uliofanikiwa tu Afrika, kwani umeingia kwenye masoko yenye nguvu kubwa duniani kama Hollywood, Bollywood na muziki wa Amerika Kusini (Latin music) na kushika nafasi ya kwanza kimataifa kwenye chati za Most Viewed Videos ndani ya saa 24.
Rayvanny ameweka rekodi mbalimbali kwenye muziki wake. Utakumbuka pia alikuwa msanii wa pili Afrika Mashariki kutazamwa zaidi ya mara bilioni 1, hapo awali Diamond na cHarmonize walishawahi kufanya hivyo.

Leave a Reply