Matendo ya Justin Bieber yazua gumzo

Matendo ya Justin Bieber yazua gumzo

Ikiwa imetimia miezi miwili tangu watu wa karibu wa mwanamuziki Justin Bieber kutangaza kuhofia afya ya akili ya msanii huyo, kutokana na mambo anayopitia na aliyopitia nyuma, hatimaye baadhi ya matendo yake yameanza kuonekana hadharani.

Hayo ni baada ya nyota huyo ambaye alianza kung'aa tangu akiwa na umri wa miaka 15, jana Januari 29,2025 kuonekana jijini New York akikatiza kwa kukimbia katika moja ya mtaa, huku akionekana kama mtu aliye na wasiwasi.



Hakuishia hapo nyota huyo hata alipojaribu kutembea hakutembea kwa hatua za kawaida badala yake alikuwa kama mtu mwenye haraka huku akiwa akishikilia suruali yake inayoonekana kama inataka kumvuka kiunoni na kuanguka chini.

Mkali huyo baadaye alionekana akiwa amevalia kofia yenye rangi nyeusi na kisha kuingia kwenye gari lake la kifahari lililokuwa limegeshwa karibu. Na mkewe Hailey akionekana anatembea peke yake akitoka katika moja ya jumba lililopo eneo hilo.

Utakumbuka kuwa Bieber na Hailey walianza urafiki wakiwa wadogo mwaka 2009 na kuingia rasmi kwenye ndoa mwaka 2019 na Agosti 2024 walibarikiwa mtoto wao wa kwanza wa kiume Jack Blues Bieber.

Kutokana na changamoto za kiuchumi na kiafya anazopitia Bieber, mwanamke huyo mwaka jana aliamua kuanza kuyavaa majukumu ya mumewe. Taarifa iliyotolewa na mtu wa karibu wa familia yao kupitia gazeti la 'In Touch Weekly'.

"Hailey ni shabiki namba moja wa Justin na anaamini kwa dhati kuwa yeye ndiye msanii bora zaidi ulimwenguni. Justin anapojidharau, Hailey hufanya usaidizi kwake ambao huleta maajabu na kurudisha kujiamini kwa Bieber," alisema mtu wa ndani.

Chanzo hicho kilisema, "Hailey anavutiwa sana na ni mtumiaji mzuri wa mitandao ya kijamii huwa anaconnect na mashabiki wa Justin Bieber na kuwauliza wanachotaka kutoka kwa msanii wao kitu ambacho ni muhimu sana linapokuja suala la biashara ya muziki," amesema mtu wa ndani.

Licha ya hayo hivi karibuni Bieber aliwashtua mashabiki baada ya kufuta urafiki na mkewe Hailey kwenye mtandao wa Instagram jambo ambalo liliibua maswali kuhusu uhai wa ndoa yao.

Tabia ya kufuta urafiki haikuwa kwa mkewe tu ulikuwa ni mfululizo wa matukio kama hayo ambayo amekuwa akifanya kwenye mitandao ya kijamii. Ikiwa ni pamoja na kuacha kufuatilia watu wake muhimu akiwemo mwalimu wake kwenye muziki Usher Raymond, meneja Scooter Braun, na hata kum-block baba mkwe wake Stephen Baldwin.

Licha ya umaarufu alionao inafahamike kuwa Bieber amekuwa akipitia changamoto za kifedha na madeni. Ripoti zinaonyesha kuwa anafuatilia hatua za kisheria dhidi ya wasimamizi wake wa zamani wa fedha akiwashutumu kwa usimamizi mbaya wa mali zake.
Ikumbukwe mapema Oktoba,2024 ripoti ya gazeti la The Sun lilifichua kuwa Bieber alilipishwa ushuru wa $380,000 ambayo alikuwa anadaiwa. Na mwaka 2022 aliwahi kuahirisha matamasha yake na kufichua kuwa anaugua ugonjwa wa kupooza uso uliosababishwa na ugonjwa unaoitwa Ramsay Hunt.

“Kama unavyoona jicho langu halikonyezi, siwezi kutabasamu upande huu wa uso wangu. Kwa hiyo kuna kupooza kabisa upande huu wa uso wangu,” alisema kwenye video aliyoichapisha kwenye ukurasa wake wa Instagram.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags