Martha Mwaipaja ajibu tuhuma za kumtelekeza mama yake

Martha Mwaipaja ajibu tuhuma za kumtelekeza mama yake

Tunaweza kusema Desemba 17,2024, imeanza vibaya kwa mwimbaji wa nyimbo za injili nchi Martha Mwaipaja, kufuatia tuhuma alizorushiwa na mdogo wake aitwaye Beatrice Mwaipaja, akidai mwimbaji huyo hajali chochote kuhusu mama yao mzazi.

Akizungumza kwenye video inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii, Beatrice amesema Martha amefikia hatua ya kutambulisha mtu baki kama mtoto wake jambo ambalo siyo la kweli.

"Mimi dada yangu mnayemjua Martha Mwaipaja ana uwezo kabisa wa kusaidia watu wengine, lakini siyo mama yake na ndiyo mama aliyetulea katika hali ambayo alipambana tukiwa wadogo. Anatembelea gari ya 100 milioni lakini mtamuona mama yake leo.

"Dada yangu anafungulia watu biashara na kuwanunulia magari. Anaponya watu kwa kuimba kwake lakini yupo nje. Mnamuona dada yangu ametambulisha watu baki kama ndugu zake lakini siyo mimi wala mama yake unafikiri ni akili ya kawaida?," amesema Beatrice katika video hiyo.

Hata hivyo, baada ya tuhuma hizo Mwananchi Scoop imezungumza na Martha kutaka kufahamu ukweli wa tuhuma hizo, lakini Mwanamuziki huyo alijibu kwa ufupi kuwa bora anyamaze kimya kwa kuwa siyo yeye aliyesema.

"Ninachoweza kuzungumza, acha ninyamaze kimya kwa sababu siyo mimi niliyesema. Kuna aliyesema, sasa nikisema haina maana, acha aendelee kusema. Mimi mama yangu anaishi na mume wake ameolewa, siwezi kuongea mengi," Martha ameiambia Mwananchi.

Aidha Sister Joan anayedaiwa kuwa ni mtoto wa Martha Mwaipaja muda mchache baada ya tuhuma hizo aliandika ujumbe kwenye ukurasa wake wa Instagram akimtaka Beatrice kukaa mbali na Martha.

"Unakumbuka laana ya Martha Mwaipaja kwamba utaanza kulia maisha yako yote, ndiyo kwanza asubuhi utalia kila madhabahu, utalia kila kona, unatamani nyota yake haitoshi kumuua, haitoshi unataka mali zake hii dunia itakuliza utalia na kulia umeshindwa kulea watoto wako ukamtelekezea mume wao tafuta hela ulee watoto.

"Bite hatukutaki kwenye familia yetu ishi maisha yako, kaa mbali na mama yangu kaa mbali naye Tafuta pesa zako binti hakuna urithi wa dada,"aliandika binti huyo

Mbali na kauli hiyo, tuhuma hizo zimeonekana kuwakera baadhi ya watu akiwemo mwigizaji Jacqueline Wolper ambaye kupitia ukurasa wake wa Instagram amemkingia kifua Martha.

"Mbona kama kalia uwongo mmh, kipo tusichokijua kuna baadhi ya ndugu wa matha wana roho mbaya sana ndio maana wengi wanashindwa kutambulisha ndugu zako kwa jamii kwa mambo kama haya, hata hiyo nyimbo ya nifundishe kunyamaza mimi inanihusu sana msitufanye tuamini kila anayelia ni mkweli.

"Tukipata muda wa kusikiliza upande wa pili tunaweza mpiga mawe huyo dada au huyo mama kwani ilikuwa ina ulazima gani kuzungumza kama siyo mipango ya shetani kumharibia mtumishi wa Mungu, sijapenda. Fanya kazi usitegemee cha ndugu video yako imejaa chuki na Mungu kakunyima machozi ya kweli,"ameandika Wolper.

Utakumbuka kuwa Martha na mdogo wake Beatrice wote ni waimbaji wa nyimbo za injili. Martha anatamba na vibao kama Sipiganagi Mwenyewe, Nifundishe Kunyamaza, huku Beatrice akitamba na nyimbo kama Usinipite Mwokozi, Moyo Wangu Tulia, Ndoto Yangu na nyinginezo.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags