Jose Chameleone Arudi Kazini

Jose Chameleone Arudi Kazini

Mwanamuziki kutoka nchini Uganda, Jose Chameleone anatarajia kufanya show kwa mara ya kwanza baada ya kutoka kwenye matibabu nchini Marekani.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, ametoa taarifa ya kufanya show Aprili 26,2025 nchini Kenya katika ukumbi wa ‘BND Kiambu Road’.

Akizungumza na waandishi wa habari alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi, msanii huyo mwenye umri wa miaka 45 alifunguka msimamo wake wa kuacha kabisa kutumia vilevi.

“Mungu amenipa nafasi nyingine, nimezaliwa nimekuwa mvutaji sigara maisha yangu yote. Lakini kwa ajili ya afya yangu, niliweka hayo kando. Sivuti tena. Sinywi tena. Basi. Nimebakisha miaka kadhaa nifikishe 50, kwa hiyo ni lazima nipunguze kasi,” amesema Chameleone.

Msanii huyo alirejea Uganda Aprili 12,2025 akitokea nchini Marekani alipokwenda kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya Kongosho (pancreatic complications), katika Hospitali ya Allina Health Mercy iliyopo Coon Rapids, Minnesota.

Taarifa ya kuumwa kwake iliwekwa wazi na mwanaye aitwaye Abba Marcus Desemba 2024, akieleza kuwa baba yake anasumbuliwa na maradhi hayo yaliyosababishwa na uraibu wa pombe kali kwa muda mrefu.

"Natamani kila mmoja afahamu kuwa kama baba yangu ataendelea na unywaji wa pombe kwa mujibu wa madaktari hatochukua miaka zaidi ya miwili kuishi. Hii inaniumiza sana kwa sababu huyu ndiyo baba yangu niliyemfahamu kwa muda wangu wa maisha," alisema Marcus.

Baada ya taarifa hiyo, Waziri wa Nchi Vijana na Masuala ya Watoto nchini Uganda, Balaam Barugahara, alipokea agizo la Rais Yoweri Museveni la kutaka msanii huyo apelekwe Marekani kwa ajili ya matibabu.

Mbali na kurudi kazini lakini pia msanii huyo inadaiwa anakwenda nchini Kenya kwa ajili ya ukaguzi wa kawaida wa kiafya (routine medical check-ups).

Chameleone ambaye alianza muziki kama DJ katika klabu ya usiku ya Missouri mwaka 1990, amewahi kutamba na ngoma kama Valu Valu, Wale Wale, Badilisha, Kipepeo, Jamila na nyinginezo.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags