Hivi Diamond Naye Ni Bishoo

Hivi Diamond Naye Ni Bishoo

Ni mtoto wa kihuni. Hajali lolote. Na kutokujali kwake kumemfikisha alipo. Kifupi hasikilizi la mtu wala hana hofu watu watasema nini. Ogopa mtu wa hivyo. Huyo ndiyo Diamond Platinumz.

Kuna wakati unajiuliza ana moyo kama sisi wengine kweli? Jamaa hana habari. Kijana fulani aliyekuwa na hasira na maisha, halafu maisha yamepotea maboya yakatuama kwa mbavu zake. Ogopa.

Dunia ya sasa ukiogopa macho ya watu, utabaki gizani na wengine wakipasua anga. Ili utusue inabidi mishipa kadhaa ya soni, aibu na hofu uitoe kichwa na moyoni. Uwe mwehu mwehu kidogo.

Kuna wanamuziki wakali zaidi ya Mondi. Lakini anawazidi kwenye kujiongeza. Mondo anapita sehemu isiyopitika, anamvaa asiyevalika. Na zaidi aliye juu yake anatamani kumtikia fasta.

Watu wenye mioyo hii. Ni rahisi sana kukutana na ofisi kali kwenye ndege. Halafu baada ya wiki moja akiwa mmiliki na mimba juu. Ndo walivyokutana na Zari miaka ile akitokea kwa Madiba.

Wenye tabia hii huishi kwenye yale aliyokuwa anayaota kabla. Kamata sana watoto wazuri. Kifupi dogo anaishi maisha ambayo vijana wengi wanayaota kila siku mpaka vitanda vinaoza.

Mkwanja unabadili kila kitu katika maisha. Usiwaze kabisa kwamba kitatokea nini baada ya kupata pesa. Wewe zisake pesa kila siku kadiri uwezavyo, kwani pesa ndo kila kitu katika maisha.

Pesa itakupa madem wazuri, tena kwa wingi usiopimika. Mpaka kuna wakati nabishana na nafsi yangu. Kwamba pesa zipo kwa ajili ya kina dada. Maana wahuni tukizipata tu wazo la kwanza ni wao.

Huwezi kupata mawe ya kutosha na ukaendelea kuishi kilofa. Siku zote pesa hubadili kila kitu katika uso wa mwanadamu. Pindi ikiwepo pesa ya kutosha hata thamani ya utu wako huongezeka.

Kama wewe ni lofa usijiweke daraja moja na wenye pesa. Lofa hajawahi kuwa na nguvu kwenye mambo ya maana. Hata vikao vya ukoo mijini na vijijini, sauti yenye nguvu ni yenye pesa.

Hii ni hulka ya waswahili. Kuamini mwenye pesa ndiye ana akili nzuri ya kufikiri. Matokeo yake ni dharau kwa makapuku. Pesa ni zaidi ya utu na akili kwa mswahili.

Na mitaani nako kuna swaga zao. Mwenye pesa anaitwa majina ya ovyo ovyo na wenye njaa njaa zao. Na wenye njaa wanapewa majina ya ovyo na wenye nafuu. Maisha yetu kivyetu vyetu.

Unamfahamu Mond wa miaka 15 nyuma? Siyo huyu. Mond yule siyo Mond huyu. Mondo yule alitamani angalau kupanga chumba kimoja Sinza. Alitamani kufahamiana na Chegge.

Msela mmoja wa Tandale. Maisha mabovu kuanzia yeye hadi familia. Hasira zake zikiwa kwenye kutoka kisanii. Akitamani kuwa Daz Baba, Tuta Bushoke na wengineo wengi kipindi kile.

Mond yule hakuwa hata na uhakika wa nauli ya daladala. Asingeweza kumega hata milupo ya Ambiansi. Alipoona Ferouz akikatiza mitaa ya Morocco na Jeep, aliumia sana.

Akiwaza ni lini atakuwa yeye? Siyo kumiliki Jeep Chorekee. Hapana! Angalau kuwa karibu tu na Ferouz, aweze kuingia hata studio za pale Bamaga kwa Majani.

Leo hii amekata ramani. Yuko juu kama mbalamwezi. Kama Sinza siyo ndoto za kumiliki geto tena, bali anaweza kuwavua mikengo watu mtaa mzima. Mkwanja siyo wa kitoto.

Anapiga pesa kwa shoo. You Tube, TikTok na 'maplatifomu' yote. Siyo yule tena wa kuwaza nauli ya Sinza. Huyu anakodi pipa kutoka 'Joobegi mpaka Naii'. Uani kwake ndinga zimelala kama zote.

Wanaoishi leo 'laifu: aliyoishi yeye miaka 15 nyuma. Wanamtazama kama bishoo. Hawamtazami kama msela aliyetoboa maisha. Mondi wa sasa siyo bishoo. Bali pesa zake ni nyingi.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags