Rapa wa Marekani, Lil Wayne (42) amelazimika kufuta tamasha lake huko Toronto nchini Canada kutokana na sababu zilizotajwa kama ugonjwa usiotarajiwa ambao umemkumba mwanamuziki huyo.
Mkali huyo wa kibao maarufu, Mirror (2011), mnamo Jumatatu, Agosti 11, alitarajiwa kutumbuiza katika jukwaa la Budweiser mjini Toronto lakini akajiondoa kutokana na changamoto hiyo ya kiafya.
"Kwa sababu ya ugonjwa ambao haukutarajiwa, onyesho la Wayne mjini Toronto usiku wa leo limeahirishwa," taarifa kwa umma ilieleza na kuongeza.
"Kama mashabiki wake mnavyojua, Wayne anapenda kutoa maonesho bora kabisa kwa wote wanaohudhuria, na alikuwa na msisimko mkubwa kuelekea onyesho hili."
"Tafadhali endelea kufuatilia hadi tarehe mpya itakapotangazwa hivi karibuni. Tiketi zote zilizokuwa zimenunuliwa zitatambulika pindi tarehe mpya itakapotangazwa," waandaaji walieleza kupitia X, zamani Twitter.
Hata hivyo, hakukuwa na maelezo zaidi kuhusu ugonjwa huo wa Lil Wayne kutoka kwake au timu yake licha ya jitihada kubwa zilizofanyika.
Kwa sasa Lil Wayne yuko katikati ya ziara yake ya Tha Carter VI, iliyoanza huko Virginia Beach, V.A. mnamo Agosti Mosi ikijumuisha miji kama Detroit, Los Angeles na Dallas.
Ziara ambayo imewaalika mastaa wengine kama French Montana, Tyga na NoCap, inatarajiwa kumalizika Oktoba 2 huko West Palm Beach, Fla, katika ukumbi wa iTHINK Financial Amphitheatre.
Hayo yanajiri baada ya Mei mwaka huu, mpenzi wa muda mrefu wa Lil Wayne, Denise Bidot kumtuhumu rapa huyo kwa unyanyasaji wa kimwili kisha kumuacha siku ya kina Mama Duniani kupitia ujumbe wa maandishi.
"Kumuacha mtu siku ya kina Mama ni ukatili wa hali ya juu. Maombi yanaendelee na Mungu hunivusha kila mara. Ninatembea kwa imani,” aliandika Denise kupitia Insta Story.
"Lil Wayne amenifukuza mimi na binti yangu siku ya kina Mama leo. Ndio tu nimepona kutoka kwenye upasuaji. Nimepita wiki tano tu baada ya kufanyiwa upasuaji wa kurekebisha mwili mzima. Siwezi hata kuinua chochote kile," alieleza Denise.
Denise alimtuhumu Lil Wayne kuwa na uhusiano na wanawake wengine wawili huko nje na ndio chanzo cha uamuzi huo ulimuachia majereha makali ya kihisia.
Ikumbukwe Lil Wayne alianza muziki mwaka 1997 baada ya Rapa Birdman kumsanini Cash Money Records na kuwa msanii mdogo zaidi katika lebo hiyo kwa wakati huo.
Chini ya Cash Money jina lake lilitambulika duniani hadi mwaka 2018 walipoachana rasmi akiwa tayari ameanzisha lebo yake, Young Money Entertainment.
Umaarufu wake ulikuwa juu zaidi baada ya kuachia albamu yake ya nne, Tha Carter (2004), na albamu yake ya sita, Tha Carter III (2008) ilimpa heshima zaidi kufuatia kushinda tuzo ya Grammy kama Albamu Bora ya Rap.
Albamu ya Tha Carter III ilikuwa na nyimbo kali kama A Milli, Got Money na Lollipop ambao uliandika rekodi kama wimbo wake wa kwanza kushika nafasi ya kwanza chati za Billboard Hot 100.
Leave a Reply